Timu ya taifa ya soka ya Tanzania itafungua safari yake Kombe la Afcon dhidi ya Morocco tarehe 17 Januari 2024. Picha TFF

Washindi wa mataji mengi zaidi soka barani Misri, imetangaza kuwa itacheza mechi ya kirafiki dhidi ya timu ya taifa ya soka ya Tanzania 'Taifa Stars' tarehe 7 Januari mjini Cairo.

Mchuano huo mkubwa wa kirafiki utakaochezwa juma moja tu kabla ya pande hizo mbili kushuka dimbani nchini Ivory Coast kwa michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika, Afcon 2024, utatumika na timu hizo kama harakati za mwisho za kujinoa kabla ya Afcon Côte D'ivoire kuanza tarehe 13 Januari.

Timu ya taifa ya soka ya Misri imejumuishwa kundi B kwenye mechi za hatua ya makundi Afcon ikiwa kundi moja na Ghana, Cape verde na Msumbiji.

Wakati huo huo, taifa stars ya Tanzania iko katika kundi F pamoja na Morocco, DRC, na Zambia.

Misri inaorodheshwa nafasi ya tano barani Afrika kwenye orodha ya viwango bora FIFA nayo Tanzania ikishikilia nafasi ya 32 Afrika na nambari 121 duniani.

Mafarao wa Misri wataanza safari yao ya Afcon 2024 dhidi ya Msumbiji mnamo tarehe 14 Januari 2024 huku nayo Tanzania ikikwatuana na Morocco tarehe 17 Januari.

Timu ya taifa ya soka ya Tanzania inaongozwa na kocha raia wa Algeria Adel Amrouche nayo Misri, ikiongozwa na Mreno Rui Vitoria wa Ureno.

AFCON
TRT Afrika