Macho yote ya wapenzi wa soka Tanzania yameelekezwa kwenye droo ya mechi za makundi ya kombe la AFCON litakayofanyika Abidjan, mji mkuu wa Ivory Coast.
Timu ya taifa ya soka ya Tanzania Taifa Stars ni miongoni mwa timu 24 zitakazoshiriki kwenye droo ya makundi ya makala ya 34 ya AFCON huku ikiwa ni timu pekee kutoka eneo la Afrika ya Mashariki.
Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania, TFF, Wallace Karia amesema mwaka huu umekuwa na mafanikio makubwa kwa Tanzania, huku akitaja kufuzu kwa Taifa Stars katika michuano ya AFCON, kuwa ni mojawapo ya mafanikio hayo.
“Tumejipanga kuhakikisha timu yetu inafanya vizuri,” alisema Karia.
Nchi zote 24 zilizofuzu hatua ya makundi ya michuano hii hivi sasa zinategea sikio kujua nani anatapangwa na nani.
Mbali na Tanzania, timu nyengine ni Ivory Coast, Senegal, Misri, Algeria, Tunisia, Afrika Kusini, Morocco, Nigeria, Zambia, DR Congo, Ghana, Cameroon, Burkina Faso, Mali, Guinea, Equatorial Guinea, Guinea Bissau, Angola, Msumbiji, Mauritania, Gambia, Namibia na Cape Verde.
Waziri Mkuu wa Tanzania Kassim Majaliwa amesema kuwa Watanzania wana matumaini kuwa timu yao itafika mbali na hata ina uwezo wa kushinda michuano hii.
“Lengo sio tu kushiriki, bali kufanya vizuri na kushinda taji hili,” Waziri Kassim Majaliwa alisema.
“Nchi nyengine wanaweza, iweje Watanzania tushindwe, sasa ni zamu yetu nyingine,” alisema wakati anakabidhi hundi wa kiasi cha shilingi milioni 500 za Kitanzania zilizotolewa na Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan kama motisha kwa timu hii baada ya kufuzu.
Katika michuano ya safari hii pia, Taifa Stars inaungana na nchi nyengine kama Guinea, Mali na Burkina Faso, ambazo kihistoria hazijawahi kabisa kutwaa taji la michuano hii mikubwa Barani Afrika.
Nchi hizi zitapambana na vigogo wengine kama vile bingwa mtetezi wa michuano hii Senegal inayoongozwa na kocha Aliou Cissé ambayo itawania taji hili kwa mara ya pili baada ya kushinda michuano hii kwa mara ya kwanza wakati wa michuano Iliyopita nchini Cameroon kwa kuwafunga Misri.
Ivory Coast, ambayo pia ilishinda michuano hii mara mbili mwaka 1992 na 2015 ni moja ya tishio jengine kwa Tanzania.
Mbali na hayo, washindi mara tatu Nigeria, ambao walitwaa ubingwa 1980, 1994 na 2013 ni timu zinazopigiwa upatu bila kuwasahau vigogo wengine Morocco, ambao wanashikilia rekodi ya kuwa taifa pekee Barani Afrika kufika nusu fainali ya Kombe la Dunia la 2022 nchini Qatar.
Boniface Pawasa ambaye ni beki mstaafu wa Taifa Stars na klabu ya Simba, anasema kuwa tofauti na zamani, Stars ya sasa haina hofu ya timu yoyote, zikiwemo zile zinazotoka Magharibi mwa Afrika.
"Kwa kweli, timu yoyote tutakayopangiwa nayo itakuwa ni kama marudio tu. Cha muhimu, Taifa Stars izidi kujiandaa vyema na kuuonyesha ulimwengu wa soka barani Afrika kuwa tuna kila sababu kwa Tanzania, Kenya na Uganda kuwa wenyeji wa AFCON ya mwaka 2027,” Pawasa alisema.
Pawasa, ambaye pia alikuwa katika kikosi cha klabu ya Simba kilichoshiriki michuano ya Klabu Bingwa Afrika CAF mwaka 2003 anasema ana imani kocha wa Stars pia atafanya utafiti kujua falsafa za walimu wa timu pinzani na kujua aina ya mfumo wanaocheza ili kukabiliana nao vilivyo.
“Wachezaji kama vile Kelvin John wa K.R.C Genk, Mbwana Samatta ( Paok ya Ugiriki), Simo Msuva (JS Kabylie ya Algeria) na Novatus Miroshi ( Shakhtar Donetsk ya Ukraine) ni miongoni mwa wachezaji wengine wanaocheza nje ambao ni muhimu katika michuano hii,”Pawasa amesema.
Taifa Stars imefuzu michuano hii ya Mataifa bora Afrika, maarufu kama AFCON kwa mara ya tatu.
“Kwa kweli Stars ina nafasi ya kufanya maajabu, licha ya timu nyingi kuwa na wachezaji wanaocheza soka la kulipwa barani Ulaya na Asia,” Pawasa amefafanua.
Tanzania ilifuzu mara ya kwanza kwa michuano hii mnamo 1980, wakati huo ikiwa chini ya kocha mzawa Joel Bendera, ambaye aliwahi pia kuwa Waziri wa Michezo.
Mara ya pili kufuzu ilikuwa mwaka 2019, ikiwa ni miaka 39 baadae ilipokuwa chini ya kocha Mnigeria Emmanuel Amunike na safari hii 2023 imeweza kufuzu tena ikiwa ni tofauti ya miaka 6 chini ya kocha Adel Amrouche mwenye asili ya Algeria.
Kuelekea upangaji wa makundi haya, mashabiki wa soka nchini Tanzania wanasema vyovyote itakavyokuwa, Taifa Stars haiangalii itapangwa na nani kwa sababu kufuzu tu pekee inamaanisha Stars ina uwezo pia wa kupambania taji hilo.
Droo ya Afcon itafanyika Oktoba 12 mjini Abidjan, mji mkuu wa nchi mwenyeji, huku CAF ikibainisha kuwa mashindano haya yatafanyika kati ya Januari 13 na Februari 11, 2024.