Na Lynne Wachira
Mbio za masafa marefu za Chicago Marathon zimemalizika kwa kishindo baada ya Mkenya Kelvin Kiptum kuvunjilia mbali rekodi ya dunia iliyokuwa inashikiliwa na Mkenya mwenzake Eliud Kipchoge.
Kiptum ameandikisha rekodi hiyo mpya baada ya kumaliza kwa muda wa 2:00:35.
Ameboresha rekodi ya Eliud Kipchoge ya 2:01:09 kwa sekundee arobaine na nne.
Kipchoge aliweka rekodi hiyo mwaka uliopita mjini Berlin.
Kevin Kiptum ambaye amekimbia mbio tatu za marathon katika maisha yake alijawa na raha tele baada ya mafanikio haya yasiyo kifani, "Nilikuwa na ndoto ya kukimbia muda wa Kasi lakini sikutarajia kuivunja rekodi ya dunia, ninaona raha sana,'' alisema baada ya kuvuka utepe wa mwisho.
Kiptum alijitambulisha kama mwanariadha hodari mwenye kipaji cha kipekee alipotwaa ushindi wa mbio za Valencia mwaka uliopita kwa muda wa kazi wa 2:01:53 na vilevile akaibuka mshindi wa mbio za London Marathon mapema mwaka huu ikiwa ni katika muda wa kasi kwa mara nyinginne tena ( 2:01:25)
Hii ni Mara ya kwanza tangu mwaka wa 1999 kwa rekodi ya dunia ya upande wa wanaume kuvunjwa katika Mashindano ya Chicago.
Pongezi zimemiminwa kwake Kiptum baada y akuandikisha rekodi hiyo mpya ikiwemo kutok akwa Rais William Ruto aliyemshukuru kwa ''kuandikisha historia katika mbio za marathon.''
Aliongezea kumsifu kama 'Mfamle wa Marathon'
Mkenya mwingine Benson Kipruto ambaye alikuja Kwenye mashindano kama bingwa mtetezi alimaliza katika nafasi ya pili katika muda wa 2:04:02 huku Bashir Abdi wa Ubelgiji akiwa wa tatu
Upande wa wanawake
Katika mbio za wanawake, Bingwa mtetezi Ruth Chepngetich wa Kenya alilazimika kuridhika na Nafasi ya pili huku Sifan Hassan wa Uholanzi akiibuka MSHINDI katika muda wa 2:13:44.
Sifan aliandikisha rekodi mpya ya bara Ulaya huku ikiwa ni mara yake ya pili kukimbia na kushinda mbio za Marathon.
Sifan ambaye ni bingwa wa olimpiki wa mbio za mita elfu kumi na mita elfu tano alijitosa katika mbio za marathon mapema mwaka huu na akaibuka mshindi katika mbio za marathon za mji wa London.
Megertu Alemu wa Ethiopia alikamilisha orodha ya tatu bora kwa muda wa 2:17:09