Muamuzi mzaliwa wa Rwanda, Salima Rhadia Mukansanga. Picha: Getty

Kati ya marefa 68 waliotajwa na CAF, watano ni ndio wanawake.

Muamuzi mzaliwa wa Rwanda, Salima Rhadia Mukansanga, aliweka historia alipokuwa mwanamke wa kwanza kusimamia mechi katika fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika nchini Cameroon.

Kabla ya hayo, mnamo Januari 10, 2022, Mukansanga aliandikisha historia kwa kuwa mwanamke wa kwanza kuwa miongoni mwa waamuzi wa mechi ngarambe za AFCON wakati alipoteuliwa kuwa msaidizi wa refa wa nne katika mchezo kati ya Guinea na Malawi huko Bafoussam.

Salima alikabidhiwa jukumu hilo na kuongoza mechi ya hatua ya makundi kati ya Zimbabwe na Guinea, ambapo alisaidiwa na marefa wengine wa kike, Carine Atemzabong (Cameroon), Fatiha Jermoumi (Morocco) na refa wa VAR Bouchra Karboubi (Morocco).

Bouchra Karboubi kutoka Morocco ambaye pia aliweka historia ya kuwa mwanamke wa kwanza katika ulimwengu wa Kiarabu kusimamia fainali ya soka ya wanaume. nchini Morocco, naye ndio refa pekee wa kike atakayechezesha mechi kwenye Afcon.

Bouchra Karboubi aliweka historia hiyo kwenye mechi ya fainali nchini Morocco mnamo 2022 kati AS FAR na Moghreb Atletico de Tetouan.

Aidha, wakati wa mechi ya fainali ya Afcon, kati ya Senegal na Misri, Karboubi alishiriki katika fainali hiyo kama muamuzi wa video (Msaidizi wa VAR).

Muamuzi huyo raia wa Morocco ambaye pia ni afisa wa polisi, alishiriki Kombe la Dunia la Wanawake 2023 kama refa mkuu pia.

Marefa wengine waliochaguliwa ni Diana Chicotesha wa Zambia, Rivet Maria Pakuita Cinquela wa Mauritius na Akhona Zennith Makalima wa Afrika Kusini.

TRT Afrika na mashirika ya habari