Kocha wa Cote d'Ivoire, Emerse Fae, anasema timu yake ilihisi "kufufuka" baada ya kuishinda Mali 2-1 katika pambano lao la robo fainali Jumamosi jioni.
Cote d'Ivoire walitoka nyuma na kunyakua ushindi na kutinga nusu fainali licha ya matokeo duni katika mechi zao za Hatua ya Makundi.
Katika mchezo wa robo fainali, Mali walitangulia kufunga katika dakika ya 71 kwa bao la Nene Dorgeles, lakini upepo ukabadilika na kuwapendelea Tembo.
Simon Adingra alisawazisha dakika ya 90 na Oumar Diakite akafunga bao la ushindi katika muda wa nyongeza.
Mwanzo dhaifu
The Elephants walikuwa wamevuka hatua ya makundi wakiwa moja ya timu bora zilizoshika nafasi ya tatu baada ya kushindwa na Equatorial Guinea na Nigeria.
Kocha Jean Louis alitimuliwa baada ya kushindwa kwa mabao 4-0 na Equitorial Guinea, na Gasset Fae aliteuliwa kuinoa timu hiyo kwa muda.
Fae alikiri kukumbwa na kimbunga cha hisia wakati wa ushindi huo mnono wa Mali. "Nilikuwa na hisia zote kichwani mwangu, nikijaribu kutafakari ili kuona mbadala bora," alisema.
Huku Tembo wakifanya vyema baada ya kufutwa kazi, Faé anasema hachukui chochote kirahisi kabla ya kukabiliana na DR Congo katika mpambano wa nusu fainali siku ya Jumatano, Februari 7.
“Ukifika nusu fainali unacheza na timu zenye ubora wa hali ya juu, hivyo tunaenda kujiandaa,” alisisitiza kocha huyo.
Mashabiki waliokatishwa tamaa
Ghasia zilizuka mjini Abidjan, Côte d'Ivoire baada ya wenyeji wa AFCON 2023 kuchapwa 4-0 na Equatorial Guinea katika mechi ya mwisho ya Kundi A.
Maelfu ya mashabiki waliondoka kwenye Uwanja wa Alassane Ouattara kabla ya kipenga cha mwisho.
Baadhi ya mashabiki wa Côte d'Ivoire waliokata tamaa waliharibu magari na kuvunja vioo vya mabasi, waandishi wa TRT Afrika walishuhudia.