Pande hizo mbili zimekutana mara 14, ambapo Super Eagles imefanikiwa kwa kuwa na sehemu kubwa ya ushindi 7 dhidi ya 2 kwa Afrika Kusini, huku zikitoka sare mechi 5.
Mechi hiyo imepangwa kuchezwa Stade de La Paix, mjini Bouake Jumatano.
Bafana Bafana wanakabiliana na maadui wa zamani, Nigeria, katika kile kinachotarajiwa kuwa marudio ya nusu fainali ya 2000 ambapo Super Eagles iliwashinda mabingwa hao wa 1996 kwa mabao 2-0 mjini Lagos yakifungwa na Tijani Babangida.
Afrika Kusini inaongozwa na mbelgiji Hugo Broos, mshindi wa AFCON 2017 , ambaye aliwaongoza Simba wasiofugika wa Cameroon kushinda kombe hilo miaka mitano iliyopita.
Kipa wa Afrika Kusini Ronwen Williams ambaye aliokoa penalti nne kati ya tano na kuisaidia Afrika Kusini kutinga nusu fainali ya Afcon, ni mmoja wa nyota wa kutegemewa wa Bafana Bafana.
Afrika Kusini imecheza bila kufungwa mechi nne mfululizo kwenye Kombe la Mataifa ya Afrika kwa Mara yao ya kwanza.
Super Eagles imejizolea heshima kwa kuwa timu ya kutisha zaidi iliyobaki kwenye mashindano, wakijivunia kuwa na washambuliaji wanaoongozwa na mchezaji bora wa sasa Afrika, Victor Osimhen, na mkakati thabiti wa ufungaji uliotekelezwa na kocha Jose Peseiro.
Nigeria imepata ushindi mara nne mfululizo bila kufungwa mabao yoyote.
Katika idara ya ulinzi, kipa wa Nigeria Stanley Nwabali, naye amekuwa tegemeo kwa timu kwa amedumisha mechi nne bila kufungwa bao hadi sasa katika kampeni ya Kombe la Mataifa ya Afrika 2023.
Aidha, baada ya kuweka rekodi hiyo, Nwabali mwenye umri wa miaka 27 amekuwa kipa wa kwanza wa Eagles kuandikisha ufanisi huo katika mashindano makubwa kwa miaka 44, huku akipiku rekodi ya kutofungwa mechi tatu ya Alloy Agu ya mnamo 1990.