Wachezaji wa Gor Mahia wakipokea kombe kutoka kwa Waziri wa Habari, Eliud Owalo | Picha: Gor Mahia

Gor Mahia iliifunga City Stars 4-1 kwenye mchuano ulioandaliwa uwanjani Moi Kasarani, jijini Nairobi na kufikisha jumla ya pointi 70 zilizotosha kuzoa taji hilo.

Samuel Kapen aliipa Nairobi City stars uongozi dakika ya 48 na kuvunja nyoyo za mashabiki wa Gor Mahia na kufufua kumbukumbu ya mwaka wa 2012 walipoinyima Gor Mahia kombe hilo.

Hata hivyo dakika chache tu baadaye, Gor Mahia ilitoka nyuma na kuwazaba Simba wa Nairobi magoli manne yaliyotosha kuwapa ubingwa huo. Mabao ya Gor Mahia yalitiwa kimiani na Benson Omalla dakika ya 50, Peter Lwasa dakika ya 62, Austine Odhiambo dakika ya 79, na Alpha Onyango dakika ya 89.

Magoli hayo yalitosha kumaliza ushindani kati ya Gor Mahia na mabingwa watetezi Tusker iliyoitesa Vihiga Bullets 4-0.

Baada ya ubingwa wake, Gor Mahia sasa imefuzu kucheza kombe la vilabu bingwa barani Afrika, CAF.

Waziri wa habari, mawasiliano, teknologia na masuala ya dijitali, Eliud Owalo alionekana kujaaa na furaha huku akiwaongoza mashabiki wa Gor Mahia kwenye sherehe za kuadhimisha kutwaa taji la 20 kwenye historia ya timu hiyo.

Baadhi ya mashabiki wa Gor Mahia | Picha: Gor Mahia

"Hongera Gor Mahia kwa kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu ya FKF 2023 baada ya kuilaza Nairobi City Stars 4-1 ugani Kasarani." Aliandika mtandaoni.

Nahodha Philemon Otieno aliiongoza Gor mahia kulinyanyua taji hilo mbele ya mashabiki waliofurika Kasarani

Wakati huo huo, straika wa Kenya Police, Elvis Rupia alijinyakulia Kiatu cha Dhahabu cha Ligi Kuu ya FKF kwa kuvunja rekodi ya ufungaji magoli kwenye msimu baada ya kufikisha idadi ya magoli hadi 27.

Magoli ya Rupia kwenye sare ya Polisi 2-2 na KCB yalimwezesha kufuta rekodi ya nyota wa zamani wa Gor Mahia Maurice Ochieng Sonyi aliyetinga mabao 26 mnamo mwaka wa 1976

Ubingwa wa Gor Mahia wa taji lake la 20, limezidisha umaarufu wa klabu hiyo iliyotwaa ubingwa mnamo 2013, baada ya ukame wa miaka 18 na kuzidisha idadi ya mataji ya ligi kuu kwa kushinda tena mnamo mwaka wa 2014, 2015, 2017, na 2018.

Timu hiyo inayoongozwa na kocha Jonathan McKinstry, sasa inatarajiwa kujiandaa kwa mashindano ya vilabu bingwa barani Afrika, CAF kuwakilisha Kenya.

Kwa upande mwingine, timu ya Tusker FC chini ya mkufunzi Robert Matano, sasa imeweka matumaini yake kwenye fainali ya kombe la FKF itakapaochuana na Kakamega Homeboyz.

Hata hivyo kutokana na changamoto za ligi, mshindi wa ligi hapokei kiwango chochote cha fedha. Kiongozi wa upinzani nchini Kenya, Raila Odinga aliwapa timu hio milioni 1.5 Kshs (takribani 11, 000 USD) ili kuwapa wachezaji motisha.

Rais wa Shirikisho la soka nchini Kenya, Nick Mwendwa, aliongoza hafla ya kuwatunuku washindi wa ligi Gor Mahia.

TRT Afrika