Kipyegon amefuzu katika orodha ya wanariadha 5 bora wa kike duniani.
Kipyegon ni mmoja wa wanariadha watano, kutoka nchi tano tofauti waliofanya maonyesho ya kuvutia katika mashindano mbalimbali ya riadha ndani ya mwaka 2023, huku wakishinda mataji na kuvunja rekodi za dunia kwenye riadha.
Awali alikuwa miongoni mwa wagombea 11 walioteuliwa kabla ya orodha kuopunguzwa hadi kufikia wanariadha watano.
Katika mbio za ligi ya Diamond huko Florence, Kipyegon alivunja rekodi ya dunia ya mita 1500 kwa kukimbia muda wa 3:49.11.
Aidha, Kipyegon alivunja rekodi ya dunia kwa mara nyingine katika mbio za mita 5000 mjini Paris, Ufaransa kwa kumaliza katika muda wa 14:05.20.
Wakati huo huo, Kipyegon alifanikiwa kujinyakulia ushindi mara dufu kwenye mashindano ya riadha duniani, akishinda mbio za mita 1500 na mita 5000.
Mwanariadha bora wa kike duniani atatangazwa tarehe 11 Disemba mwaka huu kama sehemu ya tuzo za Dunia za Mwanariadha bora wa kike na kiume, 2023.
Wengine walioteuliwa pamoja na Faith Kipyegon ni Tigist Assefa wa Ethiopia, Femke Bol wa Uholanzi, Shericka Jackson kutoka Jamaica, na Yulimar Rojas Venezuela.