Mkenya Faith Kipyegon, mkimbiaji ambaye hajawahi kushindwa mwaka huu / Picha: AFP

Baada ya kushindania ubingwa katika makala 13 tangu mwezi Mei mwaka, huu, hatimaye mbio za Ligi ya Almasi 'Wanda Diamond League' 2023 zinaingia fainali wikendi hii huku mastaa wa riadha wakikutana kwenye Eugene, Oregon, Marekani wikendi hii tarehe 16 hadi 17.

Mkenya Faith Kipyegon ambaye hajashindwa mwaka huu analenga kuhifadhi rekodi hiyo ya kutopoteza hata mbio moja huko Eugene.

Mmiliki huyo wa rekodi mbalimbali za dunia atashiriki tu kitengo cha mbio za mita 1500 huku akitarajia ushindani mkali kutoka mshindi wa medali ya fedha duniani Diribe Welteji, Mshindi wa medali ya fedha ya Olimpiki Laura Muir, mmiliki wa rekodi ya Ireland Ciara Mageean, Waethiopia Freweyni Hailu, Birke Haylom, Hirut Meshesha na Worknesh Mesele, pamoja na wanariadha wa Australia Jess Hull na Linden Hall.

Aidha, Macho yote ya Afrika yatakuwa yakiangazia mbio za mita 100 wakati Ferdinand Omanyala, anayeshikilia rekodi ya Afrika, atakapokabiliana na bingwa wa medali tatu za Dhahabu mbio za Budapest Noah Lyles, mshindi wa medali ya fedha ya Dunia Letsile Tebogo, bingwa wa dunia Christian Coleman, na Wajamaika Kishane Thompson na Ackeem Blake

Ferdinand Omanyala, anayeshikilia rekodi ya Afrika katika mbio za mita 100. Picha: AFP

Ushindani mwingine upo kwenye mbio za mita 3000 kuruka viunzi na maji huku mshindi wa medali ya shaba Duniani. Abraham Kibiwot akikimbia dhidi ya George Beamish wa New Zealand, talanta chipukizi kutoka Kenya Simon Kiprop Koech, Getnet Wale wa Ethiopia na Ryuji Miura anayeshikilia rekodi ya Kijapani katika mbio hizo.

Hata hivyo bingwa wa dunia Soufiane El Bakkali wa Morocco na Lamecha Girma wa Ethiopia anayeshikilia rekodi ya dunia, hawatoshiriki mbio hizo.

Katika mbio za mita 3000 kuruka viunzi na maji upande wa wanawake, wanariadha walionyakua nafasi saba za kwanza mbio za riadha duniani Budapest, watatoana jasho Eugene.

Ushindani mkali unasubiriwa kati ya Beatrice Chepkoech mmiliki wa rekodi ya Dunia dhidi ya Wakenya wenzake Faith Cherotich ambaye alishinda medali ya shaba duniani, Jackline Chepkoech, Winfred Yavi, Zerfe Wondemagegn wa Ethiopia, na bingwa wa Olimpiki Peruth Chemutai wa Uganda.

Tuzo ya shindano hilo ni pamoja na pesa taslimu isiyopungua dola $30,000 zitakazoshindaniwa katika jumla ya fainali 32 zilizoratibiwa kufanyika ndani ya siku mbili ya Jumamosi na Jumapili.

TRT Afrika