Polisi nchini Kenya inawashikilia watu wawili kwa kuhusika na mauaji ya mwanariadha wa Uganda, Benjamin Kiplagat mwishoni mwa wiki.
Mmoja ya washukiwa wa tukio hilo alikutwa na kisu, kinachodaiwa kutumika katika mauaji ya mwanamicheo huyo, kamanda wa polisi wa eneo hilo Stephen Okal amesema.
Kwa mujibu wa Kamanda Okal, watuhumiwa hao, wanaosadikiwa kuwa na umri wa miaka 30, walikamatwa nje kidogo ya mji maarufu wa Eldoret.
Taarifa zaidi, zinasema mwanariadha huyo, mzaliwa wa Kenya anayewakilisha Uganda, alipatikana ameuawa barabarani alipokuwa njiani kuelekea nyumbani kwake nje kidogo ya Eldoret, magharibi mwa Kenya.
Eldoret ni mji uliojizolea umaarufu wa muda mrefu, kama kitovu cha kulea na kukuza vipaji vya wanariadha wanaotajwa katika ukanda wa Afrika.
Mwili wa mwanariadha huyo, mwenye umri wa miaka 34, ulipatikana ndani ya gari Jumamosi usiku ukiwa na jeraha la kisu shingoni.
Kiplagat aliiwakilisha Uganda katika mashindano mbalimbali, ikiwemo Jumuiya ya Madola Delhi, India mnamo 2010; Mashindano ya Riadha Duniani Daegu, Korea Kusini 2011; na Michezo ya Olimpiki London, Uingereza 2012.
Aidha, Kiplagat, ndiye mshindi wa medali ya fedha katika mashindano ya wanariadha chipukizi duniani 2008, yaliyofanyika mjini Bydgoszcz nchini Poland.
Kiplagat aliwahi kufika hatua ya nusu fainali katika mbio za Olimpiki 2012 mjini London na pia alishiriki riadha Rio mnamo 2016.
Kiplagat ni mwanariadha wa nne kuuawa katika eneo hilo hivi karibuni, wengine wakiwa ni pamoja na bingwa wa dunia wa mbio Agnes Tirop, Damaris Muthee, mwanariadha wa Bahrain aliyezaliwa Kenya ambaye mwili wake ulipatikana katika nyumba ya mwanariadha wa kiume wa Ethiopia mnamo 2022.
Mwanariadha wa Rwanda Rubayita Siraji aliuawa mwezi Agosti 2023.