Shirikisho la Soka barani Afrika (CAF) limetangaza kufika makubaliano na Shirikisho la Soka la Saudi Arabia (SAFF) na kuitunuku Saudi Arabia kuwa mwenyeji wa makala ya mwaka huu ya fainali ya kombe la TotalEnergies CAF Super Cup 2023, itakayofanyika tarehe 15 Septemba.
Mapema mwaka huu, CAF na SAFF zilitia saini Mkataba wa kihistoria wa miaka mitano (MoU) unaolenga kuandaa mashindano na kukuza fursa za ukuaji kwa soka Afrika na Saudia.
Akizungumza baada ya makubaliano, Katibu Mkuu wa CAF, Veron Mosengo-Omba, alisema: “Tunafurahia kupeleka fainali ya CAF Super Cup katika eneo jipya nchini Saudi Arabia, nchi ambayo imekuwa ikipiga hatua kubwa katika soka la kimataifa."
"Afrika ni miongoni mwa maeneo bora zaidi katika soka duniani hivi sasa, na inastahili, haswa katika zama ambazo nyota wengi wa kimataifa wanaelekea Saudi Arabia, Soka la Afrika pia ni sehemu ya harakati hii." Mosengo-Omba aliongeza.
"Kwa niaba ya Rais wa SAFF, Yasser Al Misehal, tunaishukuru CAF kwa nafasi hii na tunatazamia mechi ya kipekee kwa wahusika wote." Ibrahim Alkassim, Katibu Mkuu wa SAFF alisema.
Klabu ya Al Ahly ya Misri iliifunga Wydad Casablanca ya Morocco na kutwaa taji la ubingwa wa Afrika CAF kwa mara ya 11 na kuzidisha rekodi yake ya ubingwa wa kombe hilo.
USMA ya Algeria iliweka historia kwa kutwaa taji lao la kwanza kabisa la bara baada ya kuwashinda Young Africans ya Tanzania (Yanga) kwa kanuni ya bao la ugenini katika fainali ya kusisimua ya Kombe la Shirikisho la CAF TotalEnergies msimu wa 2022-23.
Mechi hiyo ya fainali itachezwa katika uwanja wa King Fahd ulioko katika mji wa Taif.