Afrika Kusini ilitoa mojawapo ya mishtuko mikubwa zaidi katika Kombe la Mataifa ya Afrika la Afcon 2023 baada ya kuiondoa Morocco kwa ushindi wa 2-0 katika hatua ya 16 bora.
Kipindi cha kwanza kilishuhudia nafasi chache za mabao zikitengenezwa.
Atlas Lions ya Morocco walipata nafasi nzuri zaidi kipindi cha kwanza lakini wakaona bao lao likikataliwa na VAR.
Kipindi cha pili kilikuwa kinyume na kile kipindi cha kwanza kwani kilijaa msisimko na shambulio la mikiki na mabao.
"Katika kipindi cha kwanza, tulijaribu kuwazuia na kukata njia zao za kupita. Katika pili, mchezo ulifunguliwa na tukafunga,'' alisema Hugo Bross, meneja wa Bafana Bafana. ''Tulijua kuwa yeyote atakayefunga bao la kwanza kwenye mechi atakuwa na faida kubwa." aliendelea kusema.
Afrika Kusini walichukua uongozi katika dakika ya 57 wakati mshambuliaji Evidence Makgopa alipounganisha pasi ndani ya eneo la 18 na kugonga mpira kwenye kona ya chini ya kulia ya wavu.
'Ova di bar' Hakimi auza penalti
Baada ya kuchapwa chini, Morocco ilikuwa na misheni moja tu ya kusawazisha. Hii ilisababisha kucheza mfumo wa kushambulio zaidi.
Morocco walipata penalti dakika ya 83 baada ya mpira kugonga mikono ya Teboho Mokoena ndani ya eneo la 18 la Afrika Kusini na penati ikatolewa baada ya ukaguzi wa VAR.
Achraf Hakimi alijitokeza kubadilisha lakini aliishia kuupiga mpira wavuni na juhudi zake zikatoka nje ya uwanja.
"Tulipigana hadi mwisho na silaha zetu. Nimesikitishwa na wafuasi wetu ambao walistahili bora zaidi,'' alisema meneja wa Morocco Walid Regragui baada ya mechi. ''Binafsi, nilihisi tunaweza kuleta kombe hili nyumbani. Lakini hilo halikutokea. Natumai wachezaji wangu watajifunza, haswa wale makinda," aliongeza.
Afueni kubwa ilikuwa kwa Afrika Kusini baada ya kukosa lakini presha bado ilikuwa juu yao.
Sofyan Amrabat alionyeshwa kadi nyekundu baada ya kumchezea rafu Beki Mokoena , baada ya ukaguzi wa VAR na mwamuzi Mahmood Ismail.
Afrika Kusini ilichukua fursa ya utofauti wa idadi uwanjani na kuongeza bao la pili na kumaliza mchezo kutokana na mpira wa adhabu uliopigwa na Teboho Mokoena.
Afrika Kusini itacheza na Cape Verde Jumamosi, Februari 3 kwenye Uwanja wa Charles Konan Banny mjini Yamoussoukro kwenye robo-fainali.