Wakati Chris Hughton anatangaza majina ya wachezaji 27 watakaosafiri kwenda Ivory Coast kushiriki fainali za Mataifa ya Afrika (AFCON) wiki tatu zilizopita, Abdul Fatawu Issahaku hakuwemo kwenye orodha hiyo.
Hii ni kwa sababu kinda huyo aliamua kubakia na klabu ya Leicester City, inayoshiriki championship nchini Uingereza, wakati wachezaji wenzake wakielekea kwenye michuano hiyo mikubwa barani Afrika.
Hata hivyo, siku moja kabla ya kikosi cha Ghana, maarufu kama Black Stars kushuka dimbani dhidi ya Cape Verde na kukubali kipigo cha magoli mawili kwa moja katika uwanja wa Felix Houphouet-Boigny mjini Abidjan, winga huyo alikuwa anaitumikia Leicester City iliyokuwa inapepetana na Coventry.
Matokeo katika ligi hiyo yalikuwa 3-1, kwa upande wa Coventry.
Pamoja na kupoteza mchezo huo, bado ilikuwa ni siku mbaya ofisini kwa Issahaku, baada ya kuzawadiwa kadi nyekundu kwa kumfanyia madhambi Jake Bidwell.
Adhabu hiyo itamuweka kinda huyo nje ya uwanja kwa takribani mechi tatu, mpaka Februari 13.
Hii ina maana kuwa, Issahaku atakuwa nje ya uwanja kwa kipindi chote ambacho wenzake watakapokuwa wanaipambania bendera ya Ghana.
Kwa maana nyingine, Issahaku atakuwa mtazamaji tu, kama walivyo mamilioni ya watu wengine wanayoifuatilia michuano hiyo moja kwa moja kutoka Abidjan.