Patrick Wanjohi na Tsitsi Chakonza
Ripoti ya hivi majuzi ya uchumi iliyotolewa na Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) inaonyesha nchi kumi na moja za Afrika zimeorodheshwa kati ya nchi ishirini bora za kiuchumi wa kimataifa na viwango vya ukuaji wa haraka zaidi.
Kwa udhahiri hii ni habari njema kwa sekta ya fedha ya bara. Lakini badp kuna kizuizi.
Nchi nyingi za Kiafrika ziko nyuma katika ukuzaji wa ujuzi wa ziada, kama vile mawasiliano, ubunifu na uwezo wa kutatua shida.
Ujuzi huu muhimu unakubaliwa katika tasnia kama ufunguo wa kufungua ukuaji wa siku zijazo.
Mtu anaweza kusema kuwa wasimamizi wa fedha za umma katika uchumi wa Afrika wamepokea mafunzo ya kihistoria katika ujuzi wa kiufundi unaohusisha masomo mbalimbali, kama vile usimamizi wa bajeti, utabiri wa mapato na uchambuzi, ukaguzi, na mengine mengi.
Hata hivyo, kuna pengo katika kile tunaloliita kama ujuzi wa ziada, ambao mara nyingi hupuuzwa na kuwa na athari isiyo ya moja kwa moja katika kufikia malengo ya kifedha ya nchi.
Tunazungumza kuhusu mawasiliano madhubuti, uongozi na usimamizi wa kimkakati, ambao unaweza kusaidia kudhibiti misukosuko ya kiuchumi ya ndani na nje kama vile soko la fedha la kimataifa lisilo thabiti, kero la madeni na migogoro ya kijamii na kisiasa.
Kutoa nafasi
African Capacity Building Foundation, wakala maalumu wa Umoja wa Afrika kwa ajili ya kukuza uwezo, ilizindua mpango wa miaka minne wenye mwelekeo wa ufumbuzi na wa ubunifu wa ngazi ya juu wa maendeleo ya uongozi, unaoitwa Kuimarisha Uongozi na Utawala katika Usimamizi wa Fedha za Umma, wakati wa mkutano wa kila mwaka wa AfDB hivi majuzi mjini Nairobi, Kenya.
"Utafiti umeonyesha kuwa moja ya sababu kuu za kushindwa kwa marekebisho ya kiufundi - kushughulikia matatizo ya kiuchumi/kijamii bila kuzingatia mienendo ya utawala inayowaathiri katika nchi zinazoendelea, ni kwamba wanapuuza utamaduni na usimamizi bora," katibu mkuu wa wakfu huo, Mamadou Biteye, alisema wakati wa hotuba yake wakati wa uzinduzi wa programu hiyo.
Mpango huo unalenga kutoa mafunzo kwa maafisa wa ngazi za juu katika wizara za fedha na usimamizi wa fedha za umma, kuhusu taratibu za utawala bora na utendaji bora wa uongozi.
Nchi sita - Côte d'Ivoire, Ghana, Kenya, Nigeria, Senegal, na Zimbabwe - zimechaguliwa kwa awamu ya majaribio.
Kama sehemu ya programu, maafisa wanaohusishwa na mashirika ya usimamizi wa fedha za umma lazima wachukue ujuzi ambao utawezesha kutoa huduma bora na zinazopatikana kwa urahisi kwa umma.
Eneo la biashara huria
Afrika inataka kufikia lengo kubwa la soko moja, linalojumuishwa na mataifa 55 kupitia Eneo Huru la Biashara la Bara la Afrika (AfCFTA).
Mpangilio huo unakadiriwa kuboresha biashara ya ndani ya bara la Afrika kwa asilimia 52.3% kwa kuondoa ushuru wa bidhaa.
Hii inaweza kusababisha uchumi wa Afrika kupanuka kwa kiasi cha dola trilioni 29 za Marekani ifikapo mwaka wa 2050.
Wataalamu wa fedha za umma wanaweza kuwa mstari wa mbele katika kinyang'anyiro cha kufikia malengo haya, mara tu programu ya maendeleo itakapowapa ujuzi unaohitajika ili kupata kuendesha AfCFTA, kupitia kuimarishwa kwa utawala bora na uwajibikaji, usimamizi bora wa rasilimali, kuimarisha uwezo wa taasisi, kuongeza imani ya wawekezaji, na kuwezesha ushirikiano wa kikanda.
Kusimamia deni la Afrika
Uchumi wa nchi nyingi za Kiafrika bado unatatizika kujikwamua kutokana na kuzuka kwa majanga, na dhiki ya madeni ni sababu kuu inayozuia ukuaji na maendeleo yao.
Hata hivyo, pamoja na ujuzi uliopatikana kutoka kwa programu ya mafunzo, kama vile kukuza fikra za kimkakati, majadiliani na mawasiliano yenye ufanisi, uchumi wa Afrika unaweza kunufaika kutokana na uongozi bora katika kusimamia madeni ipasavyo, kujadili masharti bora zaidi kama vile viwango vya riba na muda wa ulipaji wa deni, na kuondoa rushwa.
Lengo kuu ni kuwezesha sekta ya fedha ya bara hili kufikia Ajenda kabambe ya 2063 na kuzipa nchi za Kiafrika faida zinazohitajika ili kufikisha raia wao katika bara la Afrika wanalotaka na wanalostahili.
Waandishi hao ni wataalam kutoka Taasisi ya African Capacity Building Foundation, wakala maalumu wa Umoja wa Afrika kwa ajili ya kukuza uwezo.