Burkinians protesting and carrying Russian flags after military staged a coup in the country/ AA

Faridah N. Kulumba

Ni takriban mwaka mmoja sasa, tangu Urusi ilivyo anzisha operesheni yake maalumu ya kijeshi nchini Ukraine mwezi Februari, tarehe 24 mwaka jana, sauti za milio ya vifaru zinaendelea kusikika mbali zaidi katika bara la Afrika.

Vita hivi kwa bara la Afrika vimekuja wakati mbaya mno, kwa sababu tayari bara hilo lilikuwa linauguza majeraha ya kiuchumi na kijamii yatokanayo na janga Uviko.

Mgogoro huu hauonyeshi dalili ya kuisha. Kama ilivyo kwa hali tete ya uchumi wa Afrika, ambao kwa asilimia kubwa unategemea nafaka kutoka nje.

Kupanda kwa bei ya gesi na mafuta kwa sababu ya vita kumechangia vile vile kupanda kwa bidhaa nyengine, hii ikiashiria kwamba jinamizi la kuharibu uchumi litaendelea kuiandama Afrika kwa muda mrefu.

Mafuta hadi moto

Uganda ni miongoni mwa nchi kadhaa za Afrika ambazo zimepata athari kubwa inayotokana na mgororo unaoendelea, ambao umeibuka mwezi mmoja tu wakati nchi hiyo ilikuwa inaanza kufunguka baada ya miezi kadhaa ya kuwepo kwa zuio la kutoka nje litokanalo na janga la Uviko.

Bidhaa ya kwanza kupata pigo la moja kwa moja ilikuwa ni bei ya petroli – lita moja ya petroli ambayo ilikuwa inagharimu kiasi cha dola za kimarekani 1.2 ilipanda mpaka kufikia dola 2 kuanzia mwezi Machi mpaka Disemba mwaka 2022.

Ingawa bei ya petroli baadae ilishuka kidogo na kufikia dola za kimarekani 1.5 kwa lita, lakini athari yake bado inaonekana kwa raia wa Uganda.

Uganda haidhibiti bei ya bidhaa tofauti na Kenya na Rwanda kwa sababu ya sera zake huru za kiuchumi.

Kwa hiyo, serikali haikuingilia kati kupanda kwa bei ya mafuta. Baadhi ya wanasiasa Afrika wamehusisha hali ngumu iliyopo Afrika na vikwazo alivyowekewa Urusi na mataifa ya magharibi.

Nchini Kenya, vita vinavyoendelea Ukraine pia vimekatiza mnyororo mzima wa uingizaji na usafirishaji wa bidhaa kutokana na vikwazo vilivyowekwa dhidi ya Urusi.

Hii imesababisha kupanda kwa bei ya mafuta, na kuathiri kwa kiasi kikubwa bei ya chakula na bidhaa nyengine zinazozalishwa ndani ya nchi.

Kizuizi cha usafirishaji bidhaa nje, kinakadiriwa kukaribia shilingi bilioni 10 za Kenya ($US 7.5 million) kila mwaka, imefuatia makampuni makubwa ya usafirishaji kusitisha shughuli zake kwa muda kuingia na kutoka Urusi, hii ni kutokana na vikwazo.

Takriban miezi miwili, baada ya kuanza kwa mgogoro wa Ukraine, Kenya ilikabiliwa na uhaba wa mafuta ambao haujawahi kutokea nchini humo.

Mgogoro huo ulisababisha vituo kadhaa vya mafuta kufungwa, huku bei ya bidhaa nayo kupanda maradufu.

Mwezi Juni, wazalishaji wa viwanda nchini Kenya, walilalamika kuhusu kiwango cha juu cha kubadilisha fedha za kigeni kitokanacho na upungufu wa sarafu ya dola.

Hali iliyosababishwa na vita vinavyoendelea, ambavyo vimeathiri kwa kiasi kikubwa hazina ya fedha za kigeni.

Usalama wa chakula

Bara la Afrika, kama ilivyo kwa nchi nyingi ulimwenguni, kwa kiasi kikubwa linategemea ngano kutoka Urusi na Ukraine.

Mgogoro wa Ukraine na vikwazo vya kiuchumi ilivyowekewa Urusi vimekatiza mnyororo wa usambazaji, na kusababisha matatizo katika nchi nyingi.

Kenya - ambayo inaagiza asilimia 30 ya ngano kutoka Urusi na Ukraine- imekabiliwa na uhaba mkubwa uliotokana na wafanyabiashara kuhodhi bidhaa hiyo.

Pia mataifa mengine mengi ya Afrika yanategemea ngano kutoka nje.

Mataifa kama vile Cameroon, Djibouti, Burundi, Togo, Senegal, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Tanzania, Rwanda, Togo, Libya, Mauritania, na Namibia yote yanaagiza kuanzia asilimia 50 mpaka 70 ya ngano.

Huku Madagascar na Misri wakitumia asilimia 70 mpaka 80 ya ngano inayotoka nje, Somalia inaagiza zaidi ya asilimia 90. Eritrea ni miongoni mwa nchi zilizoathirika zaidi kwa sababu inaangiza asilimia 100 ya nafaka kutoka Urusi na Ukraine.

Cha ajabu, Eritrea ni moja ya nchi tano zilizopiga kura dhidi ya uamuzi wa Umoja wa Mataifa wa kulaani uamuzi wa rais wa Urusi Vladimir Putin wa kuyafanya majimbo manne ya Ukraine kuwa chini yake.

Ethiopia haikushiriki katika kupiga kura. Siku moja baadae, Waziri Mkuu Abiy Ahmed amesema migogoro katika nchi yake inaonyesha wazi namna gani jamii, familia, maisha na uchumi unavyoweza kusambaratishwa kutokana na vita.

“Wakati athari za mali zitokanazo na vita zinaweza kurekebishika kwa urahisi, ni athari ya muda mrefu kwa jamii ambayo inatia doa kwa taifa,” amesema Abiy.

Usalama wa chakula ni muhimu kwa waafrika, na uhaba unaosababishwa na vita ni changamoto kubwa kwa nchi ambazo bado zinakabiliana na ukame utokanao na mabadiliko ya tabia nchi, migogoro na athari za janga la korona.

Mataifa mengi ya Afrika hutegemea kilimo kwa kujikimu, vita vya Ukraine pia vimeathiri upatikanaji wa mbolea kutoka Urusi.

Ghana, ikiwa ni moja wapo, inaagiza asilimia 50 ya mbolea kutoka Urusi.

Diplomasia ya kuokoa maisha

Mwaka jana, Shirika la Mpango wa Chakula Duniani (WFP) limetoa msaada wa chakula na msaada wa ruzuku kwa nchi nyingi za Afrika zilizoathirika.

Hii inafuatia kuwepo kwa kidiplomasia ya kuvutia ya Uturuki iliyohakikisha kuna makubalino ya nafaka kati ya Urusi na Ukraine yaliyotiwa saini mwezi Julai tarehe 22 mwaka jana ili kusaidia zaidi ya raia milioni mbili wa Ethiopia waliokuwa na uhaba wa chakula.

Ni kutokana na diplomasia hiyo ya Uturuki, zaidi ya tani za nafaka 23,000 ziliwasilishwa kwa WFP kusaidia Ethiopia.

Pia kupitia kampeni yao, iliyopewa jina la Pan-Africa Zero Hunger Initiative, Shirika la Msalaba Mwekundu na lile la Mwezi Mwekundu yamesaidia nchi kadhaa za Afrika zilizoathirika kwa msaada wa kibinadamu, moja wapo ikiwa ni Senegal.

Senegal huagiza zaidi ya asilimia 50 ya nafaka kukidhi mahitaji yake ya ngano kutoka Ukraine na Urusi.

Vita hivi, vimeonyesha umuhimu wa kuimarisha mifumo ya kiuchumi ya Afrika kuliko kujikita zaidi katika kuimarisha sekta za ulinzi na usalama.

Muda umefika kwa viongozi wa Afrika kuweka mkazo katika ushirikiano wa kibara na kijumuia kama vile Umoja wa Afrika, Jumuia ya Afrika Mashariki, Jumuia ya Kiuchumi ya Nchi za Afrika Magharibi-(ECOWAS), na nyenginezo ili kuinua maendeleo endelevu na uchumi jumuishi.

Vita nchini Ukraine bado vinaunguruma, na gharama za maisha katika nchi za Afrika bado inazidi kupanda. Hali hii itaendelea kuathiri maendeleo ya nchi nyingi katika bara.

TRT Afrika