Israeli wamefikishwa mbele ya mahakama ya haki na Afrika Kusini kufuatia uhalifu wa vita dhidi ya Wapalestina. /Picha: Reuters

Na

Ihsan Faruk Kilavuz

"Ninasisitiza kwamba majaribio yote ya kuwatisha au kuwashawishi vibaya maafisa wa mahakama hii lazima yakome mara moja."

Mwendesha mashtaka mkuu wa Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC) alitoa onyo hili lisiloeleweka alipotangaza nia yake ya kutoa hati za kukamatwa kwa viongozi wa Israeli na Hamas.

Ingawa onyo hili mwanzoni lilionekana kama taarifa ya kawaida ya mahakama, uchunguzi mkubwa wa waandishi wa habari uliofanywa kwa pamoja na vyombo vitatu vya habari—The Guardian, +972 Magazine, na Local Call—ulifichua kwamba Karim Khan alichagua maneno haya kimakusudi na kuhutubia moja kwa moja wahusika.

Uchunguzi huo wa pamoja umebaini kuwa maafisa wakuu wa serikali ya Israeli na maafisa wa usalama waliandaa operesheni ya ufuatiliaji ya miaka tisa inayolenga ICC, ili kuzuia uchunguzi wa uhalifu wa kivita na uhalifu dhidi ya ubinadamu unaofanywa na viongozi wa Israel.

Tofauti na Mahakama ya Kimataifa ya Haki (ICJ), ambayo inashughulikia uhalali wa hatua za serikali, ICC inazingatia watu binafsi wanaoshukiwa kufanya uhalifu wa kivita.

Kwa hivyo, upande wa Israeli uliona juhudi za uchunguzi za ICC dhidi ya Israeli kama "tishio la haraka na dhahiri" na kuelekeza juhudi zake dhidi ya watu wanaowatishia, hasa ikilenga mwendesha mashtaka mkuu wa zamani Fatou Bensouda na Khan aliye madarakani kwa sasa.

Operesheni hiyo ya siri ilishirikisha ngazi za juu zaidi za serikali ya Israeli, zikiwemo Wizara za Sheria, Mambo ya Nje na Masuala ya Kimkakati, jumuiya ya kijasusi, na mifumo ya kisheria ya kiraia na kijeshi, ili kuzuia uchunguzi.

Mtu asiye karibishwa Israeli: Fatou Bensouda

Fatou Bensouda kwa muda mrefu amekuwa mlengwa wa kampeni za kashfa za Israeli, kwavile alieanzisha uchunguzi wa awali na rasmi dhidi ya uhalifu wa kivita unaofanywa na maafisa wa Israeli katika ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu na Israeli.

Bensouda alianzisha juhudi za kuanzisha uchunguzi wa uhalifu wa kivita dhidi ua vitendo vya Israeli wakati wa mzozo wa Gaza mwaka 2014, licha ya kukabiliwa na shinikizo kubwa na upinzani kutoka kwa Israeli na mshirika wake wakiwemo Marekani.

Pingamizi kuu la Tel Aviv kwa mahakama hiyo ni kwamba haikuwa na mamlaka juu ya Israeli. Tel Aviv imekuwa ikisema mara kwa mara kwamba ICC haina mamlaka ya kuwafungulia mashitaka maafisa wa Israeli kutokana na nchi hio kutokuwa mwanachama katika Mkataba wa Roma, ulioanzisha mahakama hiyo, na kwa sababu Palestina si nchi mwanachama kamili wa Umoja wa Mataifa.

Licha ya hayo, Palestina ilitambuliwa kama mwanachama wa ICC baada ya kutia saini mkataba huo mwaka 2015, kufuatia kupokelewa kwake katika Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kama nchi isiyo mwanachama kamili.

Makosa dhidi ya 'utendaji wa haki'

Karim Khan aligonga vichwa vya habari hivi majuzi kwa kutangaza ombi la kukamatwa kwa Waziri Mkuu wa Israeli Benjamin Netanyahu na Waziri wa Ulinzi Yoav Gallant.

Kwa kutangaza hatua hii muhimu ya kisheria dhidi ya viongozi wa Israeli, Khan pia alidokeza katika taarifa hiyo hiyo kwamba shinikizo na uingiliaji kati kwa mahakama unaendelea.

Alisema, "Sitasita kushtaki majaribio ya kuwazuia, kuwatisha, au kuwashawishi vibaya maafisa wa ICC!" Madai ya Khan yalikuwa ni kitendo cha kijasiri cha ukaidi kilichoegemezwa katika kanuni za kisheria.

Alionyesha kuwa mfumo wa haki wa kimataifa hautatishika na vitendo haramu na jinai vinavyotumiwa na Israel kupotosha njia ya haki.

Tel Aviv iligonga ukuta mgumu wakati huu na sasa inakabiliwa na hatari ya uchunguzi wa ziada chini ya Kifungu cha 70 cha Mkataba wa Roma.

Kifungu cha 70, chenye kichwa "Makosa dhidi ya utendaji wa haki," kinaona uingiliaji kati unaolenga kuzuia au kuathiri michakato ya uchunguzi na kesi kama uhalifu, kuhakikisha kupatikana kwa haki katika kesi hizi.

Katika muktadha huu, kampeni ya siri ya Israeli dhidi ya mahakama iko ndani ya mamlaka ya ICC, kama ilivyobainishwa katika kifungu hicho: vitendo kama vile kuzuia, kutisha, au kushawishi kwa rushwa afisa wa mahakama ili kuwazuia au kuwashurutisha kutekeleza majukumu yao ipasavyo huchukuliwa kuwa ni adhabu.

Kwa hivyo, Khan alisisitiza uwezo wa mahakama wa kuzuia, na kutangaza kwamba itasimama dhidi ya makosa dhidi ya usimamizi wa haki.

Ni kwa kiasi gani vitendo vitaambatana na matamshi kama haya bado haijulikani, lakini angalau Israeli ilifichuliwa kwa jinsi ilivyo: Nchi Potofu.

Muda mfupi baada ya kujiunga na mahakama hiyo, Mamlaka ya Palestina (PA) iliiomba ofisi ya mwendesha mashtaka kuchunguza uhalifu uliofanywa huko Gaza, Ukingo wa Magharibi unaokaliwa kwa mabavu na Jerusalem Mashariki.

Fatou Bensouda, mwendesha mashtaka mkuu wa wakati huo, alianzisha uchunguzi wa awali ili kubaini ikiwa vigezo vya uchunguzi kamili viliafikiwa.

Kitendo cha Bensouda kilizua taharuki mjini Tel Aviv na kuifanya Israeli kuchukua hatua, kuhamasisha wataalam wa masuala ya kijeshi na raia, pamoja na ujasusi, ili kuzuia uchunguzi wake.

Juhudi hizi zilizoratibiwa zilisimamiwa na Baraza la Usalama la Kitaifa la Israeli (NSC), linalofanya kazi chini ya mamlaka ya Ofisi ya Waziri Mkuu.

Imefichuliwa kuwa mkuu wa zamani wa Mossad Yossi Cohen alikuwa kiini cha operesheni za siri zinazomlenga Bensouda, ambazo zilianza hata kabla ya kuamua kuanzisha uchunguzi rasmi wa madai ya uhalifu wa kivita katika maeneo ya Palestina yanayokaliwa kwa mabavu.

Baadhi ya vitendo hivi vilijumuisha mikutano ya siri kati yao.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, operesheni hiyo ya siri inaripotiwa kupata kibali kutoka kwa viongozi wa ngazi za juu wa serikali ya Israeli, na ushiriki wa Cohen katika uchunguzi huo uliongezeka zaidi ya kuingilia tu hadi kumtishia moja kwa moja mwendesha mashtaka mkuu.

Alitumia uonevu, usaliti, na mbinu za vitisho dhidi ya Bensouda na familia yake. Zaidi ya hayo, jasusi huyo aliripotiwa kuendeleza vitisho dhidi ya mwendesha mashtaka mkuu na familia yake kwa vitendo, akidaiwa kumuoneysha picha za siri za mumewe alipokua mjini London.

Hata hivyo, licha ya kampeni ya siri ya Tel Aviv, Bensouda alibaki imara.

Mnamo Machi 2021, alipokua kwenye ukingo wa kukabidhi majukumu yake, alitangaza kuanzishwa kwa uchunguzi rasmi.

Baadaye, muda wa Bensouda kama mwendesha mashtaka mkuu uliisha Juni 2021, na akapitisha jukumu la kuwawajibisha maafisa wa Israeli kwa uhalifu wa kivita na uhalifu dhidi ya ubinadamu uliofanywa katika maeneo ya Palestina kwa Karim Khan.

Mahakama ya haki ya kimataifa inahitaji kusimama kidete

Vita haramu vya Israeli dhidi ya Wapalestina kwa muda mrefu vimebadilika na kuwa "vita dhidi ya sheria za kimataifa zenyewe".

Hali halisi ya Tel Aviv kua "juu ya sheria" inazidi kutiliwa shaka. Kwa hivyo, dola ya Kiyahudi imeongeza shughuli zake ambazo zinadhoofisha sheria za kimataifa.

Kulingana na mantiki ya Israeli ni: "Ikiwa hakuna sheria ya kimataifa, basi hakuna ukiukwaji wa sheria." Katika suala hili, Israeli, ambayo hapo awali ilijaribu kuthibitisha kwamba vitendo vyake vilikuwa "ndani ya mipaka ya sheria" katika kujibu madai ya "ukiukaji", sasa haioni tena hitaji la kuthibitisha hilo, na hata "kupuuza" taasisi ya kisheria ya kimataifa, na kuendelea katika mauaji yake ya hivi karibuni huko Rafah licha ya uamuzi wa mahakama ya ICJ.

Bila shaka, ujasiri wa Tel Aviv unatokana na kutokuadhibiwa kwake na uungwaji mkono usio na mpaka ambao imepokea kutoka kwa washirika wake wa Magharibi kwa miongo kadhaa.

Hata hivyo, kuedelea kushinikiza kwa Tel Aviv na mahakama ya ICC na ICJ inaonyesha kuwa mambo yanabadilika, na kiburi cha Israeli hatimaye kufikia kikomo.

Baada ya yote haya, taasisi za kimataifa za mahakama zinapaswa kubaki na ujasiri dhidi ya Israeli licha ya vitisho hivyo.

Hawapaswi kusita kutumia njia zote za kisheria walizonazo kukuza heshima kwa sheria za kimataifa na wawakilishi wa sheria hizo.

Shinikizo la kisiasa pamoja na mahakama yenye nguvu ndiyo njia ya kukomesha dhuluma hii iliyovumiliwa kwa muda mrefu.

Mwandishi: Ihsan Faruk Kilavuz ni mtafiti wa Kituo cha TRT World Research Centre aliyebobea katika sheria za kimataifa za haki za binadamu na migogoro ya silaha.

TRT Afrika