Uhusiano wa Korea Kaskazini na Iran imekuwa chanzo cha wasiwasi kwa serikali za Magharibi.
Watunga sera Marekani na Ulaya wanaonya ushirikiano wa kijeshi kati ya Pyongyang na Tehran kama tishio kwa maslahi yao ya kijiografia.
Kufuatia ziara ya hivi karibuni ya ujumbe wa korea Kaskazini mjini Tehran, Idara ya Mambo ya nje ya Marekani imesema kuwa Washington "itatumia zana zake zote, ikiwa ni pamoja na vikwazo, kulishughulikia hilo.”
Kwa kiasi kikubwa, ushirikiano wa Iran na Korea Kaskazini umetokana na usawa wa malengo ya kimkakati na nia ya pamoja katika kutetea uwezo wao wa kufanya maamuzi huru, haswa kuhusu ulinzi wa kitaifa.
Kwa miaka mingi, Korea Kaskazini na Iran zimefanya ushirikiano wa kibiashara.
Kufahamu historia ya uhusiano huu wa nchi mbili huturudisha hadi vita vya Iran na Iraq (1980-88).
Tehran ilitafuta marafiki na washirika popote ilipoweza kufuatia mzozo huo wa kutisha.
Korea kaskazini ilijitokeza kama muuzaji wa silaha wa nchi Iran wakati mataifa mengi ya Magharibi na Kiarabu yaliunga mkono Baghdad.
Korea Kaskazini ilikuwa mojawapo ya nchi chache ulimwenguni zilizoisaidia Iran moja kwa moja wakati wa vita hivyo.
Pyongyang iliipa Iran makombora ya balistiki ya SCUD B, silaha za kawaida, mafunzo, na washauri wa kijeshi.
Mnamo 1989, Rais wa Wakati huo wa Iran (na Kiongozi mkuu wa Sasa) Ali Khamenei alifika Korea Kaskazini na kutangaza: "ikiwa nchi kubwa zinatishia nchi zinazoendelea, basi nchi zinazoendelea zinapaswa kuwatishia nchi kubwa...Umethibitisha kuwa Korea ina uwezo wa kukabiliana na Marekani.”
Uhusiano wa makombora
Vita vya Iran na Iraq vilipomalizika, nchi hizo zimeendelea kuwa na ushirikiano na uhusiano haswa katika maswala ya makombora.
Korea kaskazini imewasaidia Wairani kuunda makombora ya hali ya juu na Tehran imesaidia Pyongyang kwa makombora ya ziada.
Katika siku za nyuma, nchi hizo zilishirikiana kwenye manowari huku pia zikishiriki mikakati ya kukwepa vikwazo vya magharibi na kujadili uhamishaji wa mafuta ya Irani kufika Korea Kaskazini kupitia China.
Korea kaskazini na Iran ni mojawapo ya nchi chache mno zilizotoa msaada wa moja kwa moja wa kijeshi kwa Urusi katika vita vyake vya sasa nchini Ukraine.
"Ushirikiano huo ulikua ni wa maslahi, kwa vile nchi zote mbili ziko chini ya vikwazo na zimezuiwa kupata teknolojia kutoka kwa vyanzo vingine - na si ushirikiano wa itikadi, kwani Iran ni theokrasi Na Korea Kaskazini ina uhasama mkubwa kwa dini (isipokuwa ibada za kitaifa na kitamaduni)," John Feffer, mkurugenzi Wa Sera ya Nje Katika Focus, aliiambia TRT World.
"Nchi zote mbili zimeungana katika tuhuma zao dhidi ya Magharibi, ingawa sehemu kubwa ya idadi ya raia wa Iran, waunga mkono Magharibi kwa namna fulani.
Kwa ujumla, kutokana na hali tofauti sana ya nchi hizo mbili, ukosefu wa ushirikiano wa kiitikadi, na umbali wa kijiografia kati yao, ushirikiano wao wa kijeshi hautoi tishio kubwa kwa Marekani na Magharibi, ingawa uratibu juu ya masuala ya nyuklia, ikiwa ni pamoja na ICBMs (makombora ya balistiki ya Intercontinental), bila shaka ingebadilisha tathmini hiyo," aliongeza Feffer.
Kenneth Katzman, mshiriki mwandamizi wa Kituo cha Soufan, aliambia TRT World kwamba ukuaji wa ushirikiano wa kijeshi kati ya Korea Kaskazini na Iran kunaweza kupinga maslahi ya Magharibi.
Hii ni kwa sababu ya uzoefu wa Pyongyang wa makombora ya masafa marefu na uwezo wa teknolojia ya Korea Kaskazini kuwezesha Tehran kuendeleza shughuli zake za makombora kwa njia ambazo zinahangaisha serikali za Magharibi.
"Ni tishio halisi kwani Korea Kaskazini ina uzoefu zaidi na makombora ya masafa marefu. Iran ilifanya uamuzi wake wa kutovuka umbali wa kilomita 2,000. Lakini, ni wazi Korea Kaskazini imejaribu makombora ya masafa marefu zaidi, sila nzito zaidi, na yenye uwezo wa nyuklia. Kwa hivyo, kuna hofu kwamba ushirikiano huu unaweza kuiwezesha Iran kukwepa vizuizi kadhaa ambavyo vimepunguza uwezo wake, " Alisema Katzman.
Vigezo vya sera za kigeni za Marekani na Urusi
Iran imezoea kuzoroteka kwa uhusiano wake na Marekani na Wanachama wa EU tangu Washington ilipoharibu mpango wa Pamoja wa utekelezaji unaofahamika kama (Mkataba wa nyuklia wa Iran) miaka sita iliyopita na kuweka tena vikwazo vingine vikali dhidi ya Tehran.
Ili kuepuka shinikizo la magharibi iwezekanavyo, Iran imefuatilia mkakati wake wa "kutoelekea upande wowote". Korea kaskazini iko chini ya uangalizi wa msingi huu rasmi wa sera ya Kigeni ya Jamhuri ya Kiislamu.
"Ni wazi, tunaona ujumuishaji wa kambi ya mataifa-inayojumuisha Iran, Uchina, Urusi, na DPRK —Jamhuri ya watu wa Kidemokrasia ya Korea) - ambao masilahi yao duniani yanapingana kabisa na yale ya Washington na washirika wake, na ambao wanaanza kupata ujasiri na ushawishi wa kiuchumi na kijeshi ili kupanua misuli yao. Walakini vyovyote itakavyo angaliwa, hii sio changamoto rahisi, " Dk Mehran Kamrava, profesa wa Serikali Katika Chuo kikuu Cha Georgetown Huko Qatar, aliiambia TRT World.
Kulingana na Feffer, mustakabali wa uhusiano wa Korea Kaskazini na Iran utategemea jinsi ushindani mkubwa wa nguvu unavyotokea na hatua za Urusi ulimwenguni, Kremlin inatafuta kuunganisha nchi zaidi katika "muungano mpana wa kupambana na Magharibi" unaojumuisha Pyongyang na Tehran.
"Ushindi Ukraine, ingawa Urusi inataja 'ushindi,' ingepiga jeki muungano kama huo, ambayo ingemaanisha uratibu mkubwa kati ya Iran na Korea Kaskazini ndani ya mtandao mkubwa.
Lakini pia inawezekana kwamba kwa diplomasia ya ustadi, Ulaya na Marekani zinaweza kuirejesha Iran katika ushirikiano na Magharibi.
Kurudi kwa utawala wenye nia ya mageuzi pia kungebadilisha hesabu. Lakini kwa kweli, kurudi kwa Donald Trump Ikuluni pia kungeleta pamoja Iran, Korea Kaskazini, na Urusi karibu zaidi, " alisema Feffer.
Tukizingatia tabia za mirengo na ushirikiano, hakuna uhakika kabisa kuwa uhusiano wa DPRK-Iran ni thabiti.
Hata hivyo, kusalia kwa vikwazo dhidi ya Pyongyang na Tehran italeta nchi hizo mbili kuwa karibu zaidi.
Kufuatia hali hii, viongozi wa Korea Kaskazini na Iran wote watatumia uhusiano huu wa nchi mbili kwa maslahi yao.
Mafunzo kutokana na mashambulizi ya Iran dhidi ya Israeli
Wataalam wanakiri Korea Kaskazini ilikuwa na mengi ya kutazama mnamo Aprili 13 na 14, Iran ilipofanya mashambulizi dhidi ya Israeli ikilipiza kisasi shambulio la kituo cha kidiplomasia cha Tehran huko Damascus, siku 12 zilizopita.
Iran ilipofyatua mamia ya makombora na ndege zisizo na rubani katika eneo la Israeli, Israeli—kwa msaada wa Marekani, Uingereza, Ufaransa, na Jordan—ilikata makali mashambulio hayo.