Na Kristian Alexander
Uhusiano kati ya afya ya akili na vita ni mkubwa, unaathiri wale wanaohusika moja kwa moja katika maeneo ya migogoro na wale wanaotazama kutoka mbali.
Katika kesi ya mashambulizi ya kikatili na ya muda mrefu ya kijeshi ya Israeli huko Gaza, ambapo raia wasio na hatia mara nyingi hunaswa katika mapigano, athari kwa afya ya akili inaweza kuwa mbaya.
Ripoti ya 2022 ya Save the Children, shirika lisilo la kiserikali la kimataifa lenye makao yake mjini London ambalo linahusika na masuala ya haki za watoto, linafichua madhara ya vita kwa watoto wa Kipalestina.
Utafiti huo, uliopewa jina la 'Trapped: Athari za miaka 15 kwa afya ya akili ya watoto wa Gaza', unaelezea athari mbaya za kizuizi kilichowekwa Gaza tangu 2007 na kugundua kuwa ustawi wa kisaikolojia wa watoto na walezi wao huko Gaza imepungua kwa kiasi kikubwa.
Kuondoa kizuizi kungemaliza baadhi ya mafadhaiko kwa watoto hawa, lakini rasilimali bado ingehitajika ili kuwajengea uwezo wa kukabiliana na athari za muda mrefu za kiwewe.
Hali mbaya
Nyaraka katika jarida la World Psychiatry iliyopewa jina la ‘Madhara ya ugonjwa wa afya ya akili iliyosababishwa na vita: matokeo mafupi ya utafiti inabainisha kuwa “Vita vimekuwa na sehemu kubwa katika historia ya ugonjwa wa akili kwa njia kadhaa. Madhara ya ugonjwa wa kiakili ya vita vya dunia ilisababisha hatua za kisaikolojia kuchukuliwa katika nusu ya kwanza ya karne ya 20.
Mshtuko wa mabomu umejulikana kama ugonjwa wa mfadhaiko wa baada ya kiwewe (PTSD) na ni moja tu ya shida kadhaa za kisaikolojia zinazoathiri watu wanaoishi katika maeneo yenye migogoro.
Huko Gaza, kwa mfano, watu kila mara huamshwa kwa vilio vya ving'ora na milipuko.
Muda wowote, familia zinaweza kulazimika kukimbia. Wanaweza kushuhudia vurugu au nyumba zao kuharibiwa. Hali hii ya kupigana au kukimbia mara kwa mara husababisha viwango vya juu vya homoni za mafadhaiko kama vile cortisol, ambazo zina athari mbaya katika kufanya maamuzi. Wasiwasi, unyogovu, na mfadhaiko imekuwa kawaida kati ya wale wanaothirika na vita.
Kifo ni tukio la kutisha sana, na vita huko Gaza vimeleta vifo vipya kila siku. Maumivu ya pamoja ya kupoteza wapendwa na kushuhudia uharibifu ulioenea inaweza kusababisha huzuni na dhiki.
Zaidi ya hayo, vita vinavyoendelea Gaza vinaendeleza mzunguko wa kiwewe, kwani kila kukiwa na duru mpya ya ghasia, hurudisha kumbukumbu za vita vya zamani na kuzidisha majeraha. Watu ambao wameokoka vita wanaweza kupatwa na hali ya kujilaumu, ambayo inaweza kusababisha hisia za kutofaa, aibu, na mfadhaiko.
Hata wale wanaotazama matukio ya vita nje ya nchi wanaweza kupata dhiki ya kisaikolojia. Mtiririko wa mara kwa mara wa habari na picha za mateso na uharibifu unaweza kusababisha jambo linalojulikana kama 'mfadhaiko wa pili wa kiwewe' au 'uchovu wa huruma'.
Hali hii huakisi dalili za PTSD na inaweza kuathiri mtu yeyote ambaye huwa na huruma kwa waathiriwa wa migogoro hii. Hisia ya kufadhaika kwa kutoweza kutoa usaidizi wa moja kwa moja au kushawishi kupatikana kwa amani inaweza kuzidisha hisia hizi.
"Kitendo cha kushuhudia kinaweza kuwa kizito…lakini kinaweza kuumiza na kusababisha uchovu ikiwa hakitadhibitiwa ipasavyo," anasema Dk. Hala Alyan, mwanasaikolojia wa kiafya wa Palestina na Marekani mwenye makazi yake New York ambaye ni mtaalamu wa kiwewe.
"Hasa katika kesi hii, wakati watu wanahisi kuwa hawana msaada sana, inasababisha kujaa na kiwewe."
Kwa wengine, huruma inaweza kusababisha uanaharakati au kazi ya hisani kama njia ya kujaribu kuleta matokeo chanya. Hata hivyo, hata jitihada hizo zenye nia njema zaweza kuwa vyanzo vya mfadhaiko na uchovu iwapo kutakosekana usaidizi wa kihisia.
Havijawai kutokea vita kama hivi
Mzingiro na vizuizi vya kutoka Gaza vinasababisha mafadhaiko ya kipekee. Eneo hilo ni mojawapo ya eneo yenye watu wengi zaidi duniani, na maeneo kama haya, hasa katika wakati wa mashambulizi ya mara kwa mara ya mabomu, yanaweza kuwafanya wananchi wahisi wamekwama.
Sehemu kubwa ya wakazi wa Gaza ni chini ya umri wa miaka 18, na wengi wao hawana uthabiti wa kukabiliana na migogoro hiyo ya vurugu na ya muda mrefu. Hii inaweza kuwa na athari za muda mrefu baada ya vita, haswa ikiwa vita vinaendelea.
Vita vya wenyewe kwa wenyewe vya Syria, Vita vya Bosnia vya 1992-1995, na mauaji ya halaiki ya Rwanda mwaka 1995 vinafanana na Gaza leo. Katika migogoro yote hii, nyumba, shule na hospitali zilipigwa mabomu.
Kuharibika kwa miundombinu huvuruga maisha ya kila siku ya raia, na kadri utaratibu wa kawaida unavyovunjwa, ndivyo inavyokuwa vigumu kuanza upya. Vita pia husababisha uhamiaji na hivyo kuvunja jamii, ambayo ni muhimu kwa utulivu wa kisaikolojia.
Madhara ya muda mrefu wa ugonjwa wa akili inayosababishwa na vita hutegemea uzoefu wa mtu binafsi. Ukali wa vita, urefu wa vita, na idadi ya vifo.
Utafiti wa 2019 wa vita vya Bosnia uligundua kuwa "athari za kiwewe za vita kwenye mfadhaiko wa akili ziliendelea zaidi ya muongo mmoja baada ya vita na hata kuhama."
Victoria Uwonkunda, aliyenusurika wa mauaji ya halaiki ya Rwanda, alielezea "ugonjwa usioonekana" kwa BBC mwaka wa 2021. "Inanisababisha hofu ambayo inaweza kutokea wakati wowote na ambayo hunipa shida ya kupumua. Kwa kawaida mimi hutokwa na jasho jembamba baridi linapopungua, huku nikijaribu kurudi kwenye hali yangu ya kawaida’.”
Hii si mara ya kwanza kwa wakazi wengi wa Gaza kukabiliwa na vita. Baadhi ya waliopitia matukio kama vile Maandamano Makuu ya Kurudi au Vita vya Gaza vya 2008-2009 au 2014 walitengeneza mikakati ya kukabiliana na hali hiyo, lakini wengi walio na PTSD wataathirika kufuatia na kuanzishwa upya kwa vurugu.
Madaktari wanahitaji kutibiwa
Vita vinavyoendelea Gaza vimeangamiza kabisa mfumo wa afya. Hospitali zimegeuzwa kuwa vifusi, na vifaa vya matibabu vimezuiwa wakati ambapo mahitaji ya huduma za ugonjwa wa akili ni ya juu zaidi.
Madaktari na wataalamu wengine wa afya, na wafanyakazi wa kibinadamu hufanya kazi katika hali hatari, katika mfumo ambao haufadhiliwi na katika hali ya kuzidiwa.
Mgogoro wa sasa umezidisha tu mahitaji haya, huku watoa huduma za ugonjwa wa akili wakikabiliwa na changamoto mbili za kukabiliana na majeraha yao wenyewe huku wakijaribu kusaidia wengine.
Médecins du Monde, pia inajulikana kama Madaktari wa Dunia, ni shirika la kimataifa la kibinadamu linalojitolea kutoa huduma za matibabu kwa watu walio katika mazingira magumu.
Shirika hilo limeonya kuwa Wapalestina wana kiwango cha juu cha maswala ya afya ya akili, huku sehemu kubwa ya watu, haswa watoto, wakihitaji sana huduma za afya ya akili na kisaikolojia.
Kusitishwa kwa mapigano kunaweza kuunda mazingira ambapo wataalamu wa afya ya akili wanaweza kufanya kazi kwa uhuru na usalama zaidi, kuruhusu upanuzi wa huduma na ufikiaji kwa wale wanaohitaji sana.
Mafunzo ya kutoka maeneo yaliyokumbwa na vita, kama vile Balkan na Rwanda, yanaonyesha umuhimu wa kupeleka kwa haraka huduma za afya ya akili na kisaikolojia baada ya kusitishwa kwa vita.
Huduma hizi lazima ziwe za kitamaduni, zinatoa taarifa za kiwewe, na ziweze kufikiwa na makundi yote ya watu, hasa watoto ambao wameathirika kwa njia isiyo sawa.
Mwandishi, Kristian Alexander, ni Mfanyakazi Mwandamizi na Mkurugenzi wa International Security & Terrorism Program at Trends Research & Advisory. Yeye ni mshauri katika Uchanganuzi wa Mataifa ya Ghuba, mshauri wa hatari wa kijiografia na kisiasa Washington. Amefanya kazi kama Profesa Msaidizi katika Chuo cha Humanities and Social Sciences at Zayed University huko Abu Dhabi, UAE.
Maoni yaliyotolewa na mwandishi si lazima yaakisi maoni au sera za uhariri za TRT Afrika.