Wanyanyasaji wa wafungwa katika jela ya Abu Ghraib hadi sasa hajahukumiwa. / Picha: A A

Na Hamzah Rifaat

Imepita miaka 20 tangu kashfa ya unyanyasaji wa gereza la Abu Ghraib.

Picha za kuhuzunisha, na zisizo za kibinadamu za wanajeshi wa Marekani wakiwadhulumu na kuwadhalilisha wafungwa wa gereza la Abu Ghraib nchini Iraq zilileta mshtuko duniani kote.

Ukosoaji mwingi ulielekezwa kwa aliyekuwa Katibu wa Ulinzi wakati huo Donald Rumsfeld, kwa kuendeleza na kusimamia unyanyasaji wa wafungwa chini ya utawala wa Rais wa Marekani George W. Bush.

Haki hata hivyo imekuwa ikikosekana kwa wahasiriwa wa Abu Ghraib. Walalamikaji watatu walipigana vita vya muda mrefu vya kisheria na hatimaye walifikishwa kortini mwezi uliopita baada ya kufungua kesi ya madai dhidi ya Kituo cha Uchambuzi cha (CACI) chenye makao yake makuu Virginia.

Walidai kuwa unyanyasaji wa kutisha ulifanywa katika gereza hilo na wafanyikazi ambao walikuwa wakifanya kazi kwa jeshi la Marekani wakati huo.

Kesi hiyo hata hivyo, ilitupuliwa mbali na mahakama, jaji anayesimamia kesi hiyo alitangaza wiki iliyopita.

Hii ni dhulma .

Muktadha wa kesi hii

Ilianza baada ya uvamizi mwaka 2003 ulioongozwa na Marekani nchini Iraq na kuangusha utawala wa Saddam Hussein. Mwaka 2004, kipindi cha habari cha televisheni cha Marekani cha "60 Minutes" kilionesha picha za wanaume wa Iraq wakinyanyaswa kisaikolojia, kupigwa na kudhalilishwa na wasimamizi wa jela wa Marekani katika gereza la Abu Ghraib.

Hii ilikuja miezi 13 baada ya uvamizi wa Marekani dhidi ya Iraq na kuikalia nchi hiyo kwa mabavu Iraq.

Kashfa hiyo imeonyesha ishara ya ubeberu, na unafiki wa Marekani ikizingatiwa kwamba Marekani ilijitangaza kuwa ni ngome ya haki za binadamu na kudai "ukombozi wa Iraq," kabla ya jeshi lake kukutwa likiwapiga wafungwa wa Iraq na kuwaadhibu kimwili na ukatili wa kisaikolojia na wa kingono.

Kwa mujibu wa Kamati ya Kimataifa ya Msalaba Mwekundu (ICRC), asilimia 70 hadi 90 ya wafungwa huko Abu Ghraib walikuwa watu wasio na hatia ambao walikamatwa kimakosa na kukabiliwa na dhulma za kikatili, za wazi na zisizo na maana za wanajeshi wa Marekani.

Ripoti ya ICRC yenyewe mwaka 2004 ilisema kwamba mifano mingi ilikuwepo Abu Ghraib ambayo ilikiuka Mikataba ya Geneva iliyotekelezwa na wahoji, ikiwa ni pamoja na matusi, udhalilishaji, mateso ya kisaikolojia na kimwili.

Matokeo, picha na ripoti zilisababisha kilio cha kimataifa ambacho kilienda hadi Umoja wa Mataifa. Wakati huo, Kaimu Kamishna Mkuu wa Haki za Kibinadamu Bertrand Ramicharan alisema ya kwamba kashfa ya unyanyasaji wa wafungwa wa Abu Ghraib inaweza kuwa uhalifu wa kivita.

Kesi ya kwanza dhidi ya CACI iliwasilishwa 2008 na ilicheleweshwa kwa miaka 15 kutokana na mabishano ya kisheria na makanusho ya kampuni hiyo kwa madai kwamba wafanyakazi walikuwa na kinga na ulinzi wa kisheria walipokuwa wakifanya kazi na jeshi la Marekani. Mwaka mmoja baadaye, mahakama ya shirikisho ya rufaa ya Marekani ilitupilia mbali kesi iliyowasilishwa na Wairaqi 250 ambao waliteswa huko Abu Ghraib kulingana na kiegezo cha kisheria kilichoitwa "kuepushwa kwenye uwanja wa vita."

Hata hivyo licha ya ukali na ukubwa wa unyanyasaji uliofanywa, ni maafisa wachache wa ngazi za chini wa kijeshi waliofikishwa mahakamani.

Kuwa mfano wa hatari

Ukosefu wa uwajibikaji kama huo ni shida. Mashtaka ya 2024 yanakuja wakati ulimwengu unashuhudia migogoro isiyoweza kusuluhishwa ya idadi kubwa.

Inaweka kielelezo cha hatari kwamba unyanyasaji wa wafungwa unaweza kuendelea bila kuchukuliwa hatua za kisheria au ulinzi wa haki kwa waathiriwa. Hii ni pamoja na unyanyasaji wa Wapalestina katika jela za Israeli na wafungwa wa Ukraine nchini Urusi.

Maelfu ya wafungwa wa Ukraine katika jela za Urusi tangu uvamizi huo ulipoanza mwaka 2022, huku Umoja wa Mataifa ukisema kwamba wanajeshi wa Urusi waliwatesa kwa kuwapiga shoti ya umeme, kupigwa mara kwa mara, kunyongwa kwa dhihaka, na vitisho mbali mbali.

Vile vile, madaktari wa Israeli wameelezea hali ya kutisha kwa wafungwa wa Kipalestina kutoka Gaza katika jela, ambayo ni pamoja na, kufumbwa macho na kuadhibiwa kimwili, kudhalilishwa na kunyanyaswa.

Mashtaka ya 2024 huko Virginia yanatoa ishara kwamba hali ya unyanyasaji kama ilivyo sasa ni sawa na kinachoendelea katika nchi kama vile Israel na Urusi, ikizingatiwa kutokuwepo kwa uwajibikaji kwa Marekani kwa kudharau Mkataba wa Geneva wa mwaka 2004.

Inatoa uhalali kwa Tel Aviv na Moscow kuelezea kile kinachojulikana kama "msingi wa maadili ya juu" wa Marikani, ambayo inaruhusu mashirika yao ya usalama na wanajeshi kufanya vitendo viovu dhidi ya wahasiriwa wengi wasio na hatia gerezani.

Kesi ya kihistoria

Hata hivyo, uwajibikaji umekosekana lakini kesi ya hivi majuzi huko Virginia ilikuwa ya kihistoria. Kwa mara ya kwanza kabisa, walalamikaji watatu wa Iraq waliyofungwa huko Abu Ghraib walipata fursa ya kutoa ushahidi mbele ya majaji nchini Marekani.

Nao ni Suhail Najim Abdullah Al Shimari, Salah Al-Ejaili na As'ad Al-Zuba'e. Al-Ejaili alikuwa mwandishi wa habari kabla ya kukamatwa na majeshi ya Marekani na alitoa ushahidi kwamba alipigwa kikatili, amefungwa kamba na kuwekwa katika hali ya kunyimwa hisia licha ya kwamba hakuwahi kushtakiwa kwa uhalifu wowote. Walalamishi wenzake walisema waliteswa sawa na Al-Ejaili.

Kesi ilianza kwa walalamikaji wakidai kuwa CACI inawajibika kwa unyanyasaji licha ya kutokuwa na uwezo wa kuthibitisha kuwa walihusika moja kwa moja kwa kuwadhulumu wafungwa. Ushahidi ulikuja kwa njia ya ushuhuda wa wahasiriwa na majenerali wawili wa jeshi la Marekani waliostaafu ambao walirikodi unyanyasaji wa Abu Ghraib na kuihusisha na CACI.

Baada ya siku nane ya mashauriano, jaji alitangaza kutupilia mbali kesi isiyo na hatia au kutokamilika baada ya mahakama ya kiraia yenye wanachama wanane huko Alexandria kushindwa kukubaliana na hukumu. Hili lilikuja moja kwa moja baada ya CACI kudai kuwa haifai kuwajibikia vitendo vinavyofanywa na Jeshi la Marekani na uwajibikaji unapaswa kubandikwa kwa serikali badala yake.

Uwezekano wa kusikilizwa upya upo, lakini kushindikana kwa mahakama kunaonyesha kwamba haki inaweza kwa mara nyingine tena kukosekana kwa waathiriwa wa kashfa ya unyanyasaji wa wafungwa wa Abu Ghraib ambayo iliutikisa dunia, kukiuka Mikataba ya Geneva na kufichua upendeleo na unafiki wa Marekani.

Je, haki itapatikana?

Hamzah Rifaat alipata digrii za Mafunzo ya Amani na Migogoro huko Islamabad, Pakistani na katika Masuala ya Dunia na Diplomasia ya Kitaalamu kutoka Taasisi ya Mafunzo ya Kidiplomasia ya Bandaranaike huko Colombo, Sri Lanka. Hamzah pia alishiriki katika South Asian Voices katika Kituo cha Stimson huko Washington, DC mnamo 2016.

Maoni yaliyotolewa na mwandishi si lazima yaakisi maoni au sera za uhariri za TRT Afrika.

TRT Afrika