Tukio hilo limefanyika katika Hifadhi ya kitaifa ya Malkia Elizabeth, iliyoko katika wilaya ya magharibi ya Kasese / Picha: AP

Kundi la ndovu waliotoroka mbugani nchini Uganda, wamevamia kijiji jirani kiitwacho Kasandala na kuwaua watu wawili kabla ya kuharibu mazao.

Chifu wa kijiji hicho kilichovamiwa cha Kasandala, Augustus Muzimbi aliliambia shirika la habari la Anadolu kuwa watu hao wawili waliouawa ni Yoramu Mugisha ambaye alishambuliwa na tembo alipokuwa akifanya kazi katika shamba lake na Deo Mujuke aliyevamiwa akirejea kutoka ziwa jirani kuvua samaki.

Kulingana na polisi, tukio hilo limefanyika katika Hifadhi ya kitaifa ya Malkia Elizabeth, iliyoko katika wilaya ya magharibi ya Kasese, takriban kilomita 278 kutoka mji mkuu Kampala.

Mkuu wa Wilaya ya Kasese, Joe Walusimbi aliiambia Anadolu kuwa, Serikali itafanya tathmini ya uharibifu uliofanywa na kuwalipa fidia walioathirika.

Aidha, Msemaji wa Mamlaka ya Wanyamapori Uganda, Bashir Hangi, alithibitisha mauaji ya watu na uharibifu wa mazao na ndovu hao huku akitoa pole kwa waliopoteza wapendwa wao na kuahidi kuwa watasaidiwa na serikali.

TRT Afrika na mashirika ya habari