Profesa Jay, mbunge wa zamani aliachia wimbo mpya ‘Siku 462’ aliyomshirikisha mwimbaji kutoka Tanzania, Walter Chilambo.
“Nimepitia mengi katika siku 462 nilizolala kitandani, nimeona nimshukuru Mungu kwa ajili ya kipindi chote hicho na kunifanya niendelee kuwa hai hadi sasa na nawashukuru pia Watanzania kwa maombi na michango.”
Rapa huyo wa Tanzania, mwanasiasa na mbunge wa zamani wa Mikumi, ni mmoja wa wanamuziki wanaopendwa Afrika Mashariki.
“Januari 24, 2022 nilijisikia vibaya na kudhoofika mwili, mke wangu alinikimbiza hospitali ya Kitengule, baada ya huduma ya kwanza wakanikimbiza Lugale, hali ilikuwa mbaya wakanipima upesi upesi, nikakimbizwa Muhimbili kwa ambulensi ya jeshi. Nilipofika Muhimbili moja kwa moja ICU, ahsante sana Mungu kila wakati I see you,” amesema Profesa Jay.
Profesa Jay alikaa kwenye ICU kwa siku 127 na hata kuongeza kuwa alikuwa amepoteza matumaini.
Tatizo la figo limekuwa likimsumbua Profesa Jay kwa zaidi ya mwaka mmoja na miezi kadhaa kama alivyosimulia kupitia wimbo wa 462.
Profesa Jay amewashukuru viongozi wakuu mbalimbali wa Tanzania akiwemo Rais Samia Suluhu na watanzania, akisema, “utu wenu na upendo ndivyo vimenisaidia”.
“Ewe Mola nionyeshe nikufanyie kitu gani, maana upendo wako kwangu sio kitu cha kawaida,” amemalizia.
Profesa Jay amezindua taasisi yake ya ‘Profesa Jay Foundation’ kuchangia matibabu ya wagonjwa wa figo.