NA NURI ADEN
Ulimwengu hii leo unaadhimisha siku ya Kimataifa ya Misaada ya Kibinadamu huku ikikadiriwa watu milioni 406.6 wanaoishi katika nchi 82, zikiwemo za bara la Afrika, wanahitaji misaada ya kibinadamu.
Kwa muda mrefu, bara la Afrika limehusishwa na umaskini uliokithiri, migogoro na hali ya kukosa matumaini kwa jumla. Hata hivyo, Uturuki, imefika na wazo tofauti ikiamini kuwa Afrika inastahili kuangaziwa kwa ubora zaidi na kutambulika kama taifa lenye huruma.
Kwa mujibu wa Uturuki, mtazamo huu wake, ni katika sera zake barani Afrika zainazotoa kipaumbele kwa maslahi ya kibinaadamu pekee na zimeundwa kwa manufaa ya pande zote mbili bila mawazo ya kinyonyaji.
Uhusiano huu wa kibinaadam na manufaa kwa pande zote mbili unaonekana kuzaa matunda kutokana na ongezeko la balozi za mataifa ya Afrika nchini Uturuki na uwepo wa Uturuki katika mataifa mengi Afrika.
Mnamo 2002, Uturuki ilikuwa na balozi 12 pekee Afrika lakini kufikia 2022, Balozi za Uturuki barani Afrika zilikuwa zimefikia 44. Wema wa Uturuki na ufikiaji wa kidiplomasia wa Uturuki, ulipokewa vizuri huku idadi ya balozi za Afrika mjini Ankara ikiongezeka kutoka 10 mwaka 2008 hadi 37 mwaka 2021.
Rais wa Uturuki, Recep Tayyip Erdoğan, ndiye kiongozi wa dunia kutoka nje ya bara hilo kufanya ziara nyingi zaidi barani Afrika. Kufikia sasa amefanya zaidi ya ziara 50 za kiserikali katika nchi 31 kote barani ndani ya kipindi chote cha uongozi wake kama waziri mkuu na rais.
Barani Afrika, Uturuki inahusika kwa utoaji wa misaada kupitia sekta ya elimu, taasisi za kidini, sekta ya afya, utoaji matibabu, michezo na Sanaa, utamaduni na kuwafikia wahasiriwa wakati wa majanga.
Uturuki inajitofautisha na mataifa mengine makubwa na misaada ya Uturuki inakaribishwa haswa na nchi za Kiafrika kwani inakuja bila masharti ya kisiasa au kiuchumi.
Uturuki pia inafanya shughuli mbalimbali kama vile kuchimba visima vya maji, kufadhili shule, Madrasa (taasisi ya elimu ya kidini) na vituo vya watoto yatima, usambazaji wa chakula, haswa usambazaji wa nyama ya wanyama katika sherehe tukufu ya Eid al Adha (sikukuu ya dhabihu), huduma ya afya bila malipo, na upasuaji uliofanywa na madaktari bingwa wa kujitolea.
Uturuki inasisitiza kuwa kutokuwa na nyayo za ukoloni wa zamani Afrika imekuza uhusiano wake wa kindugu na wa kihistoria na bara la Afrika.
Mfumo huu mbadala wa misaada ya kibinadamu ya Uturuki inayozingatia maendeleo imewafikia mamilioni ya watu Afrika.
Uturuki imetekeleza miradi kwa ushirikiano na wizara za serikali za nchi, mashirika yasiyo ya kiserikali, sekta ya kibinafsi, mashirika ya kujitolea, wakfu, vyama na taasisi za serikali.
Kupitia mashirika mbalimbali kama Shirika la Ushirikiano na Uratibu la Uturuki (TIKA), Mamlaka ya Usimamizi wa Dharura (AFAD) na Hilali Nyekundu ya Uturuki, Uturuki imekuwa ikitoa misaada ya dharura kwa majanga yanayosababishwa na shughuli za wanadamu na majanga ya asili, na msaada wake wa dharura umekuwa ukiongezeka katika miaka ya hivi karibuni.
Uwepo wa madaktari wa Kituruki na wafanyakazi wa misaada moja kwa moja mashinani hutofautisha Uturuki na watendaji wengine wa nje na kuwezesha Uturuki kutumia vyema rasilimali zake chache kufikisha msaada wake.
Shirika la Ushirikiano na Uratibu la Uturuki (TIKA) - shirika la kituruki la utoaji wa misaada ya maendeleo - inaendesha ofisi 22 barani Afrika na hadi sasa imefanya zaidi ya miradi 7000 ya maendeleo.
Kwenye mgogoro wa Sudan unaoendela, hivi majuzi, Wakfu wa Misaada ya Kibinadamu wa IHH, shirika la msaada lenye makao yake makuu mjini Istanbul lilituma kontena 15 za meli zilizojaa vifaa vya misaada ya kibinadamu kwa Sudan. Hii ni pamoja na Chakula, bidhaa za usafi, na blanketi zilizotumwa nchini humo kwa njia ya bahari kuwafikia takriban watu 200,000.
Uturuki pia inaendesha hospitali tatu barani Afrika.
Nchini Somalia, Uturuki imejenga Hospitali ya Recep Tayyip Erdogan ya Elimu na Utafiti ya Kituruki-Kisomali, kituo kikubwa zaidi cha matibabu Afrika Mashariki.
Aidha, ndani ya mwaka huo wa 2011, Erdogan alikuwa kingozi wa kwanza wa nchi ya kigeni kutembelea Somalia ambayo wakati huo ilikumbwa na njaa na vita, akihusisha kikamilifu mamlaka ya umma ya Uturuki na wajasiriamali katika juhudi za ujenzi wa taifa lililokumbwa na changamoto mbalimbali.
Kama nchi inayofahamu matatizo ya Afrika pamoja na uwezo wake mkubwa, tunasimama na Afrika katika majukwaa yote na tutaendelea kufanya hivyo
Katika taifa la Sudan, mnamo 2014, Hospitali ya Utafiti na Mafunzo ya Nyala, katika mji wa jimbo la Darfur Kusini, ilifunguliwa na Shirika la Uratibu na Ushirikiano la Uturuki (TIKA) Chini ya uongozi wa Rais Recep Tayyip Erdogan.
Hospitali hiyo ilijengwa kwa ombi la Waziri Mkuu Erdogan kwa gharama ya dola milioni 35. Hospitali hiyo ina uwezo wa kubeba vitanda 196 na jumla ya eneo la mita za mraba elfu 50 ikiwa na vyumba vitatu vya upasuaji, vyumba viwili vya kujifungulia, kitengo cha radiolojia kilicho na vifaa kamili na maabara.
Kipindi cha janga la Uviko-19, coronavirus, Uturuki ilinyoosha mkono wa msaada kwa nchi 161 na mashirika 12 ya kimataifa, huku ikiwa kiongozi wa ulimwengu katika suala la usaidizi wa kimatibabu na konyesha umuhimu inayoweka katika kusaidiana na mshikamano.
Katika sekta ya Elimu, Uturuki imetoa ufadhili wa masomo ya ngazi ya juu kwa zaidi ya wanafunzi wapatao 12,600 kutoka nchi 54 za Afrika tangu 1992 kupitia mpango wa ufadhili wa Uturuki.
Utoaji wa madarasa ya lugha ya Kituruki kupitia taasisi ya Yunus Emre
Tangu kuanzishwa kwake mwaka wa 2009, taasisi ya Yunus Emre imetoa madarasa ya lugha ya Kituruki kwa zaidi ya watu 99,000 katika angalau nchi 45. Taasisi hiyo sasa ina zaidi ya vituo 63 vya kitamaduni kote ulimwenguni vinavyotoa programu za kisanii, kijamii na kisayansi.
Shirika la Hilali Nyekundu la Uturuki mwanzoni mwa 2017, lilizindua kampeni ya nchi nzima ya "Umudu Ol" nchini Uturuki kusaidia nchi za Afrika Mashariki zinazokabiliwa na ukame.
Ili kuzuia athari za vita vya Ukraine na Urusi kwa mataifa ya Afrika, Erdogan aliongoza juhudi za kuhakikisha nafaka imefika barani Afrika.
"Tunafanya juhudi za dhati kuhakikisha kwamba nafaka inawafikia wale wanaohitaji zaidi, hasa ndugu na dada zetu barani Afrika," Erdogan alisema katika kikao cha pili cha mkutano wa kilele wa Jumuiya ya Ushirikiano ya Shanghai (SCO) huko Samarkand, Uzbekistan.
Hata hivyo, moyo huu sio kwa bara la Afrika pekee, kwani, Uturuki pia ni nchi yenye ukarimu zaidi kwani inatenga takriban 1% ya mapato yake ya kitaifa kwa misaada ya kibinadamu. Aidha, Uturuki pia inahifadhi idadi kubwa zaidi ya wakimbizi duniani wakiwa karibu milioni 4 wa Syria kulingana na takwimu rasmi za serikali.