Na Charles Mgbolu
Akizunguka kwa furaha ndani ya vazi lake la Jumapili, Sonia Chukwu, mhitimu wa chuo kikuu, anatumia simu yake ya mkononi kupiga picha pamoja na rafiki zake.
Ndani ya muda mfupi, picha hizo za mnato zinasambaa kwenye mtandao wa Facebook, jambo linalomletea furaha Sonia.
Mtandao huo umetimiza miaka 20, toka kuanzishwa kwake na Mark Zuckerberg na wenzake watatu, ndani ya moja ya mabweni ndani ya chuo kikuu cha Harvard nchini Marekani.
Kama ilivyo kwa Sonia, jukwaa la Facebook limegeuka kuwa zaidi ya sehemu ya kukutania marafiki.
‘’Facebook imekuwa kama tulizo langu haswa ninapopitia nyakati ngumu maishani. Ni mahali pakukutana na marafiki, " Sonia anaielezea TRT Afrika.
''Kwa miaka mingi, mtandao wa Facebook umekuwa ni zaidi ya kitovu cha marafiki kukutana, kwa sasa, hata watengeneza maudhui wa Nigeria vile vile, wanatumia jukwaa hili kama sehemu ya kujitafutia kipato,’’ anasema Uhe Aitkins, mtumiaji wa Facebook kutoka Lagos, Nigeria.
Hadi kufikia 2022, bara la Afrika lilikuwa na watumiaji milioni 271 kati ya bilioni 2 wanaopatikana dunia nzima.
Hata hivyo, kulingana na utafiti uliofanywa na Statista, idadi hiyo inatarajiwa kufikia zaidi ya milioni 377, ifikapo mwaka 2025.
Hadi kufikia 2004, Facebook ndilo lililokuwa jukwaa pekee kutoka chuo kikuu cha Havard. Baada ya miezi michache, mtandao huo ukazidi kukua, huku watumiaji wa kwanza wakiwa ni wanafunzi ikifuatiwa na makundi mengine.
Mtandao huo ukaona haja ya kujitanua zaidi ilipofikia mwaka 2006, badaa ya wigo wa watumiaji wake kuongezeka.
“Wengi wa watumiaji wa mtandao huu hawapatikani hapa chuoni tena,” alisema Zuckerberg katika mahojiano yake na gazeti la York Times, mwaka 2006, mara baada ya jukwaa hilo kutanua wigo, kuhusisha watu wenye umri zaidi ya miaka 13.
“Kama tukifanikiwa, hata vijana wadogo wataanza kutumia mtandao huu,” alisema.
Kimsingi, Zuckerberg amefanikiwa kufikia malengo haya, haswa kwa kuimarisha uzoefu wa matumizi ya mtandao kipindi ambacho akili mnembo inaanza kuingia kwa kasi.
Ifeanyi Ewuzie, mfanyabiashara wa mitandaoni anafurahia neema ya biashara yake, kutokana na uwepo wa Facebook.
''Kama mmiliki wa biashara, jukwaa hili linahakikishia fursa za kutangaza na kuwafikia wateja wangu kirahisi,’’ Ifeanyi anaiambia TRT Afrika.
Mwaka 2021, Facebook iliitangaza kampuni yake mama ya ‘Meta’, nia iliyoakisi mpango wake wa kujitanua zaidi.
Hatua hiyo iliashiria azma ya Meta kuingia kwenye akili mnembo, kitu ambacho kimesaidia biashara ya Ifeanyi kuimarika zaidi.
‘’Facebook imenisaidia kukuza wigo wa wateja wangu na vile vile kutambua maendeleo yangu na kubuni njia mpya za masoko,’’ anasema Ifeanyi.
Hata hivyo, mtandao huu bado umegubikwa na kasha, masuala ya kiusalama na ukiukwaji wa haki za ushindani.
Mwaka 2023, Meta ilipigwa faini ya dola bilioni 1.2 na kuamriwa kusitisha zoezi la kuhamisha taarifa muhimu kutoka Umoja wa Ulaya kwenda Marekani.
Mwezi wa nane mwaka 2022, Facebook ilitangaza uamuzi wake kuchunguza madai ya kudukuliwa kwa akaunti za watumiaji wake zaidi ya milioni 50.
Pamoja na changamoto zote hizo, Facebook inaendelea kuwa Jukwaa la mfano katika matumizi ya mitandao ya kijamii.