Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan amezungumzia mabadiliko madogo aliyoyafanya hivi majuzi na kuathiri baraza la mawaziri na makatibu mbalimbali nchini Tanzania.
Akiwahutubia viongozi hao wakiwemo Mawaziri, Naibu Mawaziri, Makatibu Wakuu na Mabalozi mara tu baada ya kumaliza kuwaapisha katika Ikulu ndogo ya Tunguu Zanzibar, Mama Samia amefafanua uamuzi wake wa kuwahamisha kutoka wadhifa moja hadi nyingine ni kwa minajili ya kuboresha utoaji huduma kwa Watanzania.
"Nataka nisisitize ya kuwa, mabadaliko haya sio adhabu, ni mabadiliko ya kawaida ya kuboresha na kutia nguvu. Maendeleo lazima yawe na bandika, bandua. Ndio maana ya mabadiliko haya." Alisema Rais Samia.
Miongoni mwa walioathirika na mabadiliko ya awali ni Mawaziri, Naibu Mawaziri na Makatibu Wakuu watatu na Naibu Makatibu Wakuu.
Aidha, rais huyo ametoa wito kwa baadhi ya maafisa wapya walioteuliwa kufanikisha walichokuwa wakikitetea wakiwa bungeni kwani uteuzi wao unawapa nafasi ya kutoa huduma kwa wananchi wa Jamhuri ya muungano wa Tanzania.
"Mmekuwa mkipaza sauti kubwa kwa mawaziri kule bungeni. Sasa nendeni mkafanye yale mabadiliko mliyokuwa mkiyahoji na mkapaze. Yale mliyokuwa mkiwapazia sauti, mtaende mfanye nini. Ukitaka kujua uhondo wa ngoma, sharti uingie ucheze!" Rais alifafanua.
Rais Samia amewakumbusha viongozi hao kuwa ni watumishi wa watu.
"Sisi ni watumishi wa watu. Mahusiano ni jambo muhimu katika kuwatumikia watu. Upole sio Ujinga, ndio maarifa wakati mwingine. Naomba mtulie mkatumikie watu. Mmechukua kiapo cha kuwahudumia wananchi na mnapowaahidi umma, naomba mkafanye hivyo." Mama Samia aliongeza.
Rais alifanya mkutano na maafisa hao baada ya hafla hiyo ya kihistoria ya kuwaapisha mawaziri iliyofanyika kwa mara ya kwanza kwenye ikulu ya Zanzibar.
Aidha, aliyekuwa Naibu Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania Dkt. Bernard Yohana Kibese ameapishwa kuwa Balozi mpya wa Tanzania Nchini Kenya.
Aliyekuwa Mkurugenzi mkuu wa idara ya usalama wa taifa Balozi Said Hussein Massoro ambaye amempisha Balozi Iddi Ali Siwa, naye amekula kiapo kuwa Balozi pamoja na maafisa wengine.