Na Kudra Maliro
Melodi inayosisimua inasikika kupitia mitaa yenye shughuli nyingi ya Goma, mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, hasa wakati wa wikendi na katika shughuli za vijana.
Rhumba ya Congo, inayojulikana kienyeji kama rumba, ni wimbo wa kipekee wa utamaduni wa Kiafrika unaovutia wakazi na wageni kwa pamoja.
Kutoka asili yake iliyojikita sana katika historia ya nchi hiyo hadi kwa mageuzi yake ya kasi kwa muda, rhumba inaendelea kuwa nguzo ya muziki wa Kiafrika.
Salomon Ngima, mwanamuziki mwenye umri wa miaka 39 kutoka mji wa mashariki wa Beni, anasema amekuwa na mapenzi na rhumba tangu umri mdogo, na anadai kuwa ameongozwa na wasanii kama Werrason na J.B M'piana tangu mwaka 2000.
"Muziki wetu ni kiungo cha kijamii kati ya watu wa Congo kwa sababu unatupa fahari," alisema Salomon Ngima kwa TRT Afrika.
Asili
Ili kuelewa kiini cha rhumba, ni lazima kurudi nyuma hadi miaka ya 1930 wakati wanamuziki wa eneo hilo walianza kuchanganya midundo ya Kiafrika ya jadi na sauti za vyombo vya Magharibi kama gitaa na kinanda cha mkono.
Mchanganyiko huu wa kipekee ulizaa aina mpya ya muziki: Rhumba ya Congo, ambayo haraka ikawa ishara ya roho ya DRC.
Waasisi wa muziki huu ni pamoja na majina ya kihistoria kama Wendo Kolosoy na Franco Luambo. Nyimbo zao ziligusa mioyo ya taifa zima, zikileta furaha na matumaini kwa nchi ambayo mara nyingi imekumbwa na vita na kutokuwa na utulivu.
Rhumba imekuwa kama kipimo cha pamoja miongoni mwa watu mbalimbali wa Congo, ikiunda hisia ya umoja kuvuka mipaka ya kikabila.
"Naweza kusema kwamba rhumba ni utambulisho wetu wa kitaifa, kwa sababu ninapojitambulisha kama Mcongo, watu wanatambua moja kwa moja shukrani kwa rhumba. Nimekuwa mwanamuziki kwa takriban miaka 10 sasa na ninajipatia riziki kwa kucheza muziki wa Congo," anaongeza Bwana Ngima.
Kwa miaka mingi, Rhumba ya Congo imeendelea kujumuisha athari za Kiafro-Cuba, kutokana na ujio wa wanamuziki wa Cuba huko Kinshasa.
Kipengele cha Kuunganisha
Kuongezwa kwa midundo ya Kilatini kumeleta kipimo kipya kwenye muziki huu, ukipeleka zaidi ya bara la Afrika.
Wasanii kama Papa Wemba na Koffi Olomide wameboresha Rhumba kwa kuiunganisha na aina zingine za muziki wa kigeni kama soukous na zouk.
Wachambuzi wanasema muziki huu unachangia katika kuunganisha zaidi ya makabila 450 nchini.
Aboubakar Kalunga Jingo, mwandishi wa habari na mchambuzi wa muziki wa Congo katika Radiotélévision Muungano Beni, chaneli ya eneo hilo mjini Beni, alisema rhumba ndio muziki unaosikilizwa zaidi DRC, na kwamba unagusa vizazi vyote.
"Rhumba ni muziki usiozeeka, kwa sababu tangu miaka ya 1930 umebaki vile vile licha ya mchanganyiko kidogo wa noti za muziki," Kalunga anaiambia TRT Afrika.
Waandishi wa habari wa muziki kama Kalunga wanapiga nyimbo mia moja hivi kuwaburudisha mashabiki wa rhumba.
Ujumbe wa Kijamii na Kisiasa
Rhumba ni zaidi ya muziki tu. Ni kioo cha jamii inayobadilika kila wakati. Mashairi ya nyimbo hizi mara nyingi yanajumuisha ujumbe wa kijamii na kisiasa, yakishughulikia masuala kama mapenzi, umaskini, ufisadi na harakati za kutafuta haki.
Rhumba ni njia kwa wasanii wa Congo kutoa sauti kwa watu, kuonyesha matatizo ya jamii yao na kutafuta suluhisho.
Leo, rhumba ya KCngo inaendelea kuvuma, ikiungwa mkono na kizazi kipya cha wasanii wenye vipaji.
Tamasha zimejaa mashabiki, wakitamani kucheza kwa sauti ya gitaa za kuvutia na sauti zenye nguvu. Studio za kurekodi zimejaa muziki huku wasanii wakijaribu kuandika kibao kipya cha rhumba kila kukicha.
Rhumba ya Congo imevumilia majaribio ya wakati, ikiendelea kuwa chanzo cha msukumo kwa vizazi vyote. Inaakisi umoja na fahari ya watu, ikiwapa sauti wale ambao mara nyingi hawasikiki.
Ni muziki unaovuka vikwazo vya kitamaduni na kijiografia, ukiugusa mioyo ya mamilioni ya watu kote duniani.
Rhumba ya Congo ni zaidi ya wimbo tu, ni urithi wa muziki unaondelea kung'aa leo na kesho.
Iwe kwenye mitaa yenye shughuli nyingi ya Kinshasa au kwenye majukwaa ya kimataifa, mtindo huu wa muziki ni nguvu inayoishi ambayo ushawishi wake unaendelea kustaajabisha wengi.