Serikali ya DR Congo hatimaye imetimiza ahadi yake ya kumuenzi Papa Wemba, ambayo ilikuwa ni kujenga sanamu kama kumbukumbu ya nyota huyo wa Rhumba DRC na nje ya mipaka ya nchi hiyo.
Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Félix Tshisekedi alizindua sanamu hilo la Papa Wemba (Jules Shungu Wembadio Pene Kikumba), aliyefariki Aprili 2016.
Bi Marie Rose Luzolo "Amazon," mjane wa nyota marehemu Papa Wemba, alikuwa miongoni mwa waliohudhuria hafla ya uzinduzi, idadi kubwa pia ya wananchi na wasanii walishiriki katika uzinduzi huo.
Mnara huo umejengwa katika wilaya ya Matonge, kwenye makutano ya barabara za Stade na Oshwe.
Jules Shungu Wembadio Pene Kikumba 'Papa Wemba' ni mmoja wa waimbaji walioiweka DRC kwenye ramani ya muziki duniani kupitia muziki wa Rhumba.
Mnamo Desemba 2021, Rhumba ya Kongo ilipata hadhi ya kuingizwa na UNESCO katika orodha ya Urithi wa Utamaduni usioonekana wa ubinadamu.
Mapema mwaka huu, serikali ya DRC ilitimiza ahadi yake ya awali, ambayo ilikuwa ni kuikabidhi nyumba ya marehemu Papa Wemba iliyopo Kinshasa kwa taasisi ya makumbusho ya kitaifa ya Kongo, ili igeuzwe kuwa nyumba ya Rhumba ya Kongo.