Sakinah Musafiri  amelenga kufungua fursa zaidi za ajira kwa vijana.

Na Firmain Eric Mbadinga

Watu wengi mjini Goma, wanavutiwa na kazi zinazofanyika katika karakana ya useremala inayomilikiwa na Sakinah Musafiri.

Japokuwa mji wa Goma, unaopatikana mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo unafahamika kwa machafuko ya kisiasa na milipuko ya mara kwa mara ya mlima Nyiragongo, kazi za Sakinah zinaleta tafsiri tofauti ya eneo hilo.

Mwanamke huyo ameiita sehemu yake ya biashara ''La Mano'', lenye maana ya mkono katika lugha ya Kihispaniola kama heshima kwa mafundi seremala wanaopatikana katika karakana hiyo.

Wingi wa samani ndani ya karakana hiyo ni matokeo ya muda mrefu ya mapenzi ya Sakinah kwenye kazi za sanaa na ubunifu kupitia mbao, anaiambia TRT Afrika.

Kazi zinazofanyika katika karakana na Sakinah zimevutia wateja wengi.

''Nilikuja kugundua kuwa nchi yetu imejaliwa mbao nzuri na za kipekee lakini hazikutumika kwa matumizi sahihi. Ndipo nilipoamuwa nijikite zaidi kuzifahamu aina zote za mbao na namna ya kuzitumia ili kupata kitu kitakachokuwa na manufaa kwetu, bara la Afrika kama sio dunia kwa ujumla," Sakinah anaimbia TRT Afrika.

Wakati wa kuanzisha kampuni ya "La mano", Sakinah alitegemea akiba ya fedha aliyokuwa anajiwekea ili aweze kununua baadhi ya vifaa pamoja na kukodisha eneo la biashara, kabla ya kuwatafuta watu ambao aliwapa mafunzo na hatimaye ajira.

Kwa kuanzia, kiwanda cha Sakinah kilitengeneza chemli kwa kutumia mbao ambazo ziliwavutia wananchi wengi wa Goma.

Moja za kazi zilizowavutia wakazi wengi wa Goma ni chemli iliyotengenezwa kwa mbao.

Ingawa hakuwa amelenga kupata faida, mapato yaliyotokana na kazi zake zilimpa Sakinah ari zaidi ya kuwekeza kwenye biashara hiyo.

"Tuliazimia kuwapa mafunzo vijana zaidi ya kitaalamu ili kukuza bidhaa zetu, hususani zile zinazotokana na miti.

"Tulitaka kuwahimiza wakongomani wote kutimia bidhaa za ndani. Kuhusu faida, hilo ni suala la muda mrefu," anasema Sakinah.

Kampuni ya La Mano imeajiri jumla ya wafanyakazi 40 katika nafasi mbalimbali, kama vile uhasibu, useremala, usimamizi na uchomeleaji. Pia, kuna idara ya uchongaji na ushonaji.

Mafundi seremala katika karakana na Sakinah hutengeneza bidhaa tofauti kwa kuzingatia maono na vionjo vyao wenyewe, pia kwa kutegemea matakwa ya wateja wao. Kazi zao huleta uwiano kati ya uasilia na usasa.

Wateja hupendekeza muonekano wa samani zao.

Pamoja na kutumia bidhaa zitokanazo na mbao, Sakinah pamoja na wafanyakazi wake hutumia muda wa mwezi mmoja kupanda miti kwa ajili ya vizazi vijavyo.

Ndani ya kipindi cha miaka mitatu tu, Sakinah amefanikiwa kujijenga kibisahara, huku asilimia 90 ya wateja wake wakiwa ni wa Congo wakati asilimia 10 iliyobakia ni ya waafrika, watu wa Ulaya na Amerika.

''Hilo ndio lengo letu na tunafurahi kuona kwamba tunafikia hilo lengo," anasema Sakinah.

Binti huyo, mwenye miaka 27, na mhitimu wa shahada kwenye usimamizi wa maendeleo hana nia ya kuishia hapo tu, ila amelenga kujitanua zaidi kibiashara, hata ikibidi nje ya DRC.

TRT Afrika