Mahakama moja iliyoko katika mji wa Kismayu katika eneo la Jubba, nchini Somalia, imemhukumu kifo mshtakiwa Hassan Abdullahi Abdi aliyemuua mama yake, Halimo Mohamed Omar, tarehe 11 Juni 2023 katika mji huo.
Hassan Abdullahi Abdi alimuua mamake mwenye umri wa miaka 61, kwa kutumia kisu, kama ilivyoripotiwa awali na maafisa wa usalama wa Jubbaland.
Juhudi za awali za muuaji za kujaribu kutoroka baada ya kumuua mamake, hazikufanikiwa kwani alikamatwa na polisi wa Jubbaland.
Kilichowashtua wengi ni hatua ya mshukiwa huyo kufika mbele ya mahakama na kukiri kumuua mama yake kwa kukusudia jambo ambalo liliwashangaza viongozi waliokuwa eneo la tukio.
Aidha, Hassan aliiambia mahakama kuwa alikuwa na akili timamu na wala hakuwa na maumivu yoyote alipotekeleza unyama huo dhidi ya mama yake.
Hii leo, mahakama ya Kismayu ilitoa hukumu ya kifo kwa Hassan Abdullahi Abdi, baada ya kufanya vikao kadhaa vya kuskiza kesi kuhusu mtu huyo, ambayo ilikuwa ikifuatiliwa kwa karibu na raia wa Somalia.
Wakati huo huo, Mahakama hiyo pia imeahidi kuwa hukumu ya kifo iliyotolewa dhidi ya mtu huyo itatekelezwa ndani ya siku zijazo.
Hukumu ya kifo dhidi ya mtu huyo inatarajiwa kupokewa vyema na raia wa Somalia kwani ukatili wa mtu huyo awali ilizua hofu miongoni mwa raia wa Somalia hasa watu wa Kismayo, na imekuwa ikisambazwa sana kwenye mitandao ya kijamii nchini humo.