Maafisa wa afya nchini Somalia wanapaswa kukabiliana na majeruhi wa ukosefu wa usalama na magonjwa Picha | AP

Na Charles Mgbolu

Dk Ahmed Ali Muse, umri miaka 33, ambaye ni daktari wa upasuaji wa majeraha katika mji mkuu wa Somalia, Mogadishu, alikuwa nyumbani wakati sauti ya mlipuko mzito ilipomshtua. Mlipuko huo, ambao ulitokea umbali wa kilomita 2, ulikuwa na nguvu sana kiasi cha kuharibu sehemu ya paa lake.

Alikuja kusikia baadae maafa yaliyoikumba Mogadishu siku hiyo - Oktoba 14, 2017 - wakati mabomu mawili yaliyokua ndani ya malori yakisababisha vifo, uharibifu na hofu katika jiji hilo lenye watu wengi. Maafisa wa afya waliripoti kuwa watu 587 walipoteza maisha na 316 walijeruhiwa. Kutokana idadi ya vifo kuwa kubwa, kundi la vijana wa Somalia, ikiwa ni pamoja na Dk Muse, walisaidia kwa sehemu kubwa katika kuhakikisha kwamba idadi ya majeruhi haiongezeki.

"Palepale nilikumbuka mafunzo yangu kama daktari wa upasuaji. Nilijua kwamba waathiriwa wa milipuko hiyo wangefurika hospitali katika mji mkuu na kungekuwa na hitaji kubwa la kuongezewa damu," Dk Muse anaiambia TRT Afrika kuhusu siku hiyo ya kutisha.

Wakati wa shambulio hilo, taifa hilo la Afrika Mashariki halikuwa na benki ya kitaifa ya uhifadhi damu. Dk Muse alijua alikuwa na dakika tu za kuchukua hatua. Hata kabla ya kukimbilia kitengo cha dharura cha hospitali, aliingia haraka kwenye ukurasa wa Facebook, akitoa wito wa kuchangia damu. Ndani ya dakika chache, makundi ya watu waliojitolea walikuwa wamefika katika hospitali karibu na eneo la mlipuko.

"Nilipofika hospitalini tayari watu walikuwa wanasubiri kuchangia damu, ilikuwa ni tukio lililoonyesha nguvu ya ubinadamu wetu, ingawa tulipoteza watu wengi siku hiyo, kitendo hiki kiliokoa maisha ya watu wengi," anakumbuka.

Waokoaji wa mitandaoni

Milipuko ya mara kwa mara ya bomu na masuala yanayohusiana na afya inamaanisha watu mara nyingi huhitaji kuongezewa damu. Picha. Kumbukumbu ya AP

Ukurasa wa Facebook unaoitwa ‘Wanaojitolea Kuchangia Damu Somalia’ unaonekana kuleta tofauti kati ya uhai na kifo huku Mogadishu ikipambana na uharibifu unaosababishwa na mashambulizi ya kigaidi. Ukurasa huo, ingawa umeanzishwa na Dk Muse, unaendeshwa na timu ya watu 12 wa kujitolea: mchanganyiko wa madaktari, wataalamu wa teknolojia ya habari, wataalamu wa fedha na wasimamizi wakuu.

"Lengo letu ni kuongeza kwenye mitandao ya kijamii sauti za watu wanaotaka wachangia wa damu," anasema Dkt Muse.

"Tunapokea maombi kutoka kila mahali - watu binafsi au hospitali za mikoa - na kusambaza taarifa hizo kwa nguvu kwenye mitandao yetu yote ya kijamii. Pia tunawahimiza wafuasi wa kurasa zetu kutangaza maombi kutoka kwa mtu yeyote anayehitaji damu. Katika ukurasa wetu, mtu ana akiomba, na mwingine anajitokeza kutoa."

Kundi hilo lilianzishwa mwaka wa 2015, mwaka mmoja baada ya Dk Muse kupata shahada yake ya matibabu katika Chuo Kikuu cha Kusini mwa Somalia.

“Ilikuwa vigumu kuwaza kwamba iko siku nitafanya kazi katika mazingira haya. Ni wazi kama daktari-mpasuaji nilijua kungekuwa na wakati utiaji-damu mishipani wa dharura utahitajika. Lakini bila kuwapo hifadhi ya damu ya kitaifa tutawezaje kupeleka damu hospitali kwa haraka ili kuokoa maisha? Itakuaje pale damu ya wanafamilia wa karibu haifanani na ya mgonjwa? Nini kitatokea? Niliogopa sana "anasema.

Tangu mwaka 2015, kikundi kimetengeneza mfumo wa kuhifadhi taarifa (database) na ukurasa wake wa Facebook una wafuasi zaidi ya 40,000. Pia waliunda vikundi maalum vya WhatsApp kwa aina zote nane za damu. Vikundi hivi vina wachangiaji 14,000 wa damu kwa pamoja, wakijumuisha wanafunzi wa vyuo vikuu, wanajeshi, wafanyikazi wa hospitali, na wanachama wa vikundi husika.

"Sasa hivi tunajulikana sana na tunapata maombi moja kwa moja kutoka hospitali. Ikiwa kuna aina maalum ya damu inayohitajika, tunaingia tu kwenye ukurasa wa kikundi cha WhatsApp na kufanya ombi huko na mtu atajibu," anasema Dk Muse kwa majivuno.

Somalia ni mojawapo ya nchi zenye viwango vya juu vya vifo vya uzazi na watoto duniani. Picha/Reuters

Haikuwa kazi rahisi kukuza kiwango cha ufahamu na mwitikio

"Mara ya kwanza tulipopata wachangiaji kutokana na mwito wetu kwenye mitandao ya kijamii ilikuwa tarehe 7 Februari 2016. Sitasahau tarehe hiyo. Hii ilikuwa ni baada ya miezi mingi ya kuweka ujumbe ambao ulikuwa mchanganyiko wa maombi ya wachangiaji na uhamasishaji wa umma, pasipo mwitikio hata mmoja," anasimulia Dk Muse.

Harakati pia ilikabiliwa na vikwazo vya kifedha.

"Tulihitaji na bado tunahitaji programu madhubuti za kompyuta ambazo zinaweza kutusaidia kuhifadhi taarifa za wachangiaji, lakini kama unavyojua kulipia na kutunza programu hizi za uhifadhi ni ghali."

Msalaba wa taifa

Kulingana na ripoti ya Utafiti wa Takwimu za Afya ya Somalia wa 2020, nchi hiyo inashika nafasi ya 6 duniani, ikiwa na viwango vya juu zaidi vya vifo vya uzazi vya 692 kwa kila watoto 100,000 wanaozaliwa wakiwa hai.

Ukosefu wa upatikanaji wa damu salama ni sababu kuu ya vifo vya uzazi. Kila mwaka, wanawake 5,000 wa Somalia wanakufa kutokana na matatizo ya uzazi, kulingana na ripoti ya Umoja wa Mataifa ya 2017.

Mnamo Agosti 2022, Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Huduma za Miradi (UNPOS) ilitangaza kuwa inaunga mkono Serikali ya Somalia katika ujenzi wa benki ya kwanza ya kitaifa ya damu nchini humo. Kwa kutumia zaidi ya dola milioni 3 zilizotolewa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Idadi ya Watu, UNOPS inapanga, kubuni, kujenga hifadhi ya taifa ya damu pamoja na kununua vifaa vyake kulingana na mwongozo wa kitaalam kutoka Shirika la Afya Ulimwenguni.

Hatua hio ilipongezwa na wafanyakazi wa kada ya kitabibu kote Somalia, ambao kwa miaka mingi wamefanya kazi katika mazingira magumu sana.

"Itasaidia sana kupunguza ugumu tumeokuwa tunaupata," anasema Dk Muse. “Lakini mimi na timu yangu tutaendelea kufanya kazi ambayo tunaifanya hata baada ya kuanzishwa benki ya taifa ya damu, tuna jumuiya inayojitolea, na tutaendelea kufanya tuwezalo katika kuhakikisha damu inafika kwa anayeihitaji kwa njia tunayojua zaidi, na hiyo ni kwa kutumia nguvu ya mitandao ya kijamii."

TRT Afrika na mashirika ya habari