Na Coletta Wanjohi
Baada ya miaka mingi ya kuishi na kufanya kazi nje ya nchi, Shakur Shidane alirejea nyumbani kwa ajili ya kufanya mradi mmoja tu katika sekta ya mawasiliano nchini Somalia.
Hakujua kwamba angechagua sio tu kubaki nyuma, lakini pia kufanya kazi katika kujenga kitu ambacho kinaweza kubadilisha sekta ya fedha ya nchi yake.
"Mojawapo ya masuala niliyotaka kusuluhisha ni miundombinu ya fedha nchini," Shidane anaiambia TRT Afrika. "Tulichokusudia kufanya ni kusaidia kuunda jukwaa la kuwezesha malipo haraka iwezekanavyo."
Mnamo 2021, alianzisha jukwaa la kuhamisha pesa linaloitwa @Bixi.
"Katika mwaka uliopita pekee, tumeweza kusaidia watu kutumiana zaidi ya dola milioni sita. Tunatazamia kujenga lango la malipo kwa Somalia kwa sababu tunaona siku zijazo zitategemea kwa ukubwa majukwaa ya mtandaoni. Wasomali sasa wana uwezo wa kuanza hii ," Shidane anasema.
Idadi kubwa ya Wasomali wengine, ndani na nje ya nchi, wana matumaini kama ya Shidane wakati nchi yao inapoelekea katika hali ya kujitegemea baada ya miongo kadhaa ya hali mbovu ya uchumi.
Safari ndefu
Wakati Somalia ilijitahidi kujikwamua kutokana na vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyodumu kwa miaka 30, changamoto ya ugaidi kutoka kwa wanamgambo wa Al Shabaab ilizidi kuhujumu maendeleo.
Kwa sasa kuna takriban wakimbizi 687, 000 wa asili ya Kisomali katika nchi jirani za Kenya, Ethiopia, Uganda na Djibouti.
Jitihada za Somalia kutoka katika maafa ya vita vya wenyewe kwa wenyewe imevutia mashirika mengi yanayotaka kuunga mkono mchakato huu.
Lakini, kama wataalam wengi wa maendeleo wanavyoonyesha, tatizo la msingi ni kwamba kuna fedha nyingi zinazoonekana kutiririka Somalia kutoka nje, kwa miaka mingi lakini hakuna maendeleo mengi ambayo yanaonekana.
Benki ya Dunia inakubali kwamba Somalia inaelekea kwa "ukuaji wa haraka wa miji, matumizi yanayokua ya teknolojia ya kidijitali, na uwekezaji uliopangwa katika nishati, bandari, elimu na afya."
Ukuaji huu umekuja kinyume na matarajio, ikiwa ni pamoja na baadhi ambayo sio ya nchi yenyewe.
Madhara ya mabadiliko ya tabianchi yamesababisha ukame wa muda mrefu nchini Somalia.
Ingawa tayari kuna mashirika 335 yanayotoa msaada kwa zaidi ya watu milioni 8.25 wanaobeba msalaba wa ukame na njaa, bado kuna mengi ya kufanywa.
Umoja wa Mataifa unasema takriban dola bilioni 2.6 zinahitajika kwa ajili ya msaada unaofaa kwa walioathiriwa.
Mabwawa ya mawe
Fatima Jibrell mwenye umri wa miaka 75, ni mwanamazingira aliyezaliwa na kukulia Somalia.
Alianzisha "mabwawa ya mawe" kwa jamii katika maeneo ya Sool na Sanaag nchini humo ambayo yanakabiliwa na ukame mkali na kuenea kwa jangwa.
"Tulitoa mafunzo kwa jumuiya katika kitu ambacho tayari wanakijua (lakini pengine walikuwa hawakitumii)," Fatima anaiambia TRT Afrika
"Kusanya mawe yaliyo juu kabisa, yaweke kwenye njia ya mtiririko wa maji. Wakati wa mvua, miamba hii inapunguza mtiririko, na kwa sababu maji yatakaa hapo kwa muda wa saa moja, unyevu unashuka chini. Baada ya muda nyasi na miti huanza kuota na kumea," anasema.
Fatima anapendekeza kwamba ikiwa mashirika yasiyo ya kiserikali yanataka kusaidia jamii zilizoathiriwa na ukame nchini Somalia, yanapaswa kuwekeza katika miradi kama hiyo ya kuhifadhi maji.
"Je, mashirika yasiyo ya kiserikali yatashiriki katika hilo na kuwapa rasilimali za kununulia zana zinazohitajika, na kuruhusu jamii kusimamia mabwawa yao ya mawe? Ikiwa sivyo, fedha zinazotolewa kwa walioathirika na ukame zitatoweka ndani ya mwezi mmoja au miwili," anasema. .
Katika hafla ya tuzo za kimataifa za Kisomali zilizofanyika Istanbul Machi mwaka huu, Fatima alipokea tuzo ya mafanikio ya maisha kwa kutambua kwa juhudi zake.
Kupitia shirika linaloitwa Adeso, ameungana na bintiye kutetea "Afrika ambayo haitegemei misaada".
Wajibu ni kwa serikali ya Somalia kuanzisha na kutekeleza sera ambazo zitasaidia ukuaji wa viwanda na sekta binafsi, kulingana na Degan Ali, Mkurugenzi Mtendaji wa Adeso.
"Misaada imeanzisha utegemezi - imeundwa kwasababu hiyo," anaiambia TRT Afrika. "Tunahitaji kufikiria jinsi ya kuchukua suala hilo mikononi mwetu," Degan anasema.
"Hali ya watu kuwa wakimbizi wa ndani kwa miaka 20 na kutegemea misaada kutoka kwa jumuiya ya kimataifa sio endelevu."
Utajiri wa Somalia
Ripoti za serikali ya Somalia zinaonyesha mavuno ya kila mwaka ya rasilimali za uvuvi wa baharini nchini Somalia ni kati ya tani 180,000 na 200,000.
Ukanda wa pwani wa nchi, miamba muhimu ya matumbawe, maeneo spesheli za ndege wa baharini, na pwani zenye kasa wanaotaga zinaweza kuwa baadhi ya maeneo ambayo yana tija isiyotumika bado kwa uwekezaji barani Afrika.
Uwepo wa mafuta na gesi, nje ya nchi na katika maji ya Somalia, tayari umevutia makampuni mengi ya kimataifa ya uchunguzi.
Mnamo 2022, Somalia ilitia saini makubaliano ya uchunguzi wa mafuta ya petroli kwa vituo vya baharini na shirika la Coastline Exploration lenye makao yake Marekani.
Kulingana na Baraza la Kitaifa la Uchumi la Somalia, sekta ya uchimbaji wa chumvi na madini nchini humo ina uwezo wa kupanua sekta ya ufuaji.
Somalia inahesabiwa kuwa miongoni mwa nchi zinazoongoza kwa kuuza mifugo nje ya nchi, hasa ngamia.
Uwezo wa nishati ya jua bado haujatumiwa, kuanzia 5 hadi 7 kWh/m2 kwa siku, na zaidi ya siku 310 za jua kwa mwaka, au saa 3,000 za jua kwa mwaka.
Mpango wa Maendeleo wa Kitaifa wa nchi unaonyesha kuwa nchi ina takriban hekta milioni 8.9 za ardhi inayofaa kwa kilimo, ambapo karibu hekta milioni 2.3 zinazalisha au zinaweza kuzalisha mazao kwa kutegemea mvua.
Somalia inatumai kuwa wengi wa wanadiaspora watarejea nyumbani na kuwekeza katika uwezo wake usio na kikomo, na hivyo kupunguza utegemezi wake mkubwa wa misaada.