Mwanaharakati wa mazingira wa Uganda amevunja rekodi ya dunia ya Guinness kwa muda mrefu zaidi wa kukumbatia mti.
Faith Patricia Ariokot, mwenye umri wa miaka 29, alifanya hivyo tarehe 16 Januari alipokumbatia shina la mti kwa saa 16 dakika na 6.
Guinness World Records ilithibitisha rekodi hiyo Ijumaa.
"Mti na mimi tumefika kwenye tovuti ya Guinness World Records. Rasmi ni ajabu. Panda mti pia," alisema katika ukurasa wake wa X, iliyokuwa Twitter, baada ya rekodi kuthibitishwa.
Jaribio la Tatu
Hii ilikuwa mara ya tatu ndani ya kipindi cha mwezi mmoja ambapo Faith alijaribu kuweka rekodi, kwani kamera yake ilishindwa kurekodi sehemu kubwa ya jaribio lake la kwanza, na jaribio lake la pili lilikatizwa ghafla kwa sababu ya dhoruba ya radi.
"Miguu yangu kwa zaidi ya saa 16 mfululizo iliniuma," aliiambia Guinness World Records.
"Mti ukiwa mgumu ulikata kwenye ngozi yangu na kusababisha maumivu mengi kusema ukweli, na bado nililazimika kuendelea kushikilia."
Faith anasema kwamba kuchagua mti wa kukumbatia kwa jaribio hili la rekodi "ilikuwa kama kuchagua gauni la harusi".
"Mti ulinichagua mimi, na ilikuwa kama mapenzi ," alieleza.
Changamoto hiyo ilikusudiwa "kuhamasisha wengine kupanda miti na kuonyesha haja ya binadamu kuwalinda".
Faith hakuwa na ruhusa ya kupumzika – mikono yake haikuruhusiwa kuachiliwa kutoka kwenye mti wakati wowote, na alitakiwa kusimama kwa muda wote wa jaribio la rekodi.
Anatumai mafanikio yake yatahamasisha wengine kutoka nje na kupanda miti.
"Nataka kuzungumzia kuhusu upendo. Upendo kwa ardhi. Upendo kwa dunia. Upendo kwa kila mmoja. Hakuna sayari nyingine tunayoweza kuiita nyumbani," ananukuliwa akisema.