Mke wa rais wa Uturuki amesema kuwa amewasilisha "masikitiko" yake kwa mke wa waziri mkuu wa Uswidi kutokana na kisa cha hivi majuzi cha kuchomwa kwa kitabu kitakatifu cha Waislamu huko Stockholm. Alisema:
"Nilielezea masikitiko yangu kwa Bi. Ed kuhusu kutoheshimiwa kwa kitabu chetu kitakatifu, Quran, nchini Uswidi," Emine Erdogan aliandika kwenye Twitter Jumatano baada ya kumpokea Birgitta Ed kando ya mkutano wa kilele wa NATO wa wiki hii nchini Lithuania.
Mwezi uliopita, jamaa mmoja aliyetambuliwa kuwa raia wa Iraq, aliteketeza nakala ya Quran mbele ya Msikiti wa Stockholm nchini Sweden, akiwa chini ya ulinzi wa polisi.
Kitendo hicho cha uchokozi kilipangwa kufanyika sambamba na sherehe za Eid al Adha, mojawapo ya sherehe kuu za dini ya Kiislamu zinazosherehekewa na Waislamu kote ulimwenguni.
"Nilifurahi kwamba makubaliano yalifikiwa juu ya hatua madhubuti za kupambana na kuongezeka kwa ubaguzi wa rangi na chuki dhidi ya Uislamu barani Ulaya," Erdogan pia alisema katika ukurasa wake wa Twitter baada ya mkutano huo.
Erdogan pia alisema wakati wa mkutano wao katika mji mkuu wa taifa la Baltic Vilnius, kuwa yeye na Ed walijadili miradi yao ya kijamii na jinsi ya kuboresha ushirikiano wa kitamaduni kati ya nchi hizo mbili.
Viongozi 31 wa muungano wa kijeshi wanakutana katika mji mkuu wa Lithuania Vilnius kujadili mzozo wa Ukraine, ombi la NATO la Uswidi, na hatua za kuimarisha ulinzi na kuzuia mashambulio.