Na Dayo Yussuf
Julai 17 ni siku ya kuadhimisha emoji duniani. Vijisura au ishara zinazotumika katika mawasiliano katika mitandao ya kijamii hasa kuashiria hisia.
Mabingwa wa utumiaji wa emoji katika mitandao wanasema kuwa emoji zimewasaidia sana katika kujieleza. Sharon Machira ni mmoja wao jijini Nairobi anayesema kuwa hawezi kuchati bila kutumia emoji.
‘’Emoji ni ishara za mazungumzo mtandaoni. Unapotuma ujumbe mfupi, humuoni unaye chati naye kwa hiyo hujui anavyokuelewa,’’ ameambia TRT Afrika. ‘’Kuchati bila emoji ni sawa na kuzungumza bila ishara ya mikono.’’ Anasema Sharon.
Emoji zinatofautiana kwa michoro yake japo matumizi yake yanaweza kutofautioana kutoka sehemu moja hadi nyingine, au utamaduni mmoja hadi mwingine.
Emoji kama njia ya kujieleza
Sharon anasema kuwa emoji inasaidia kusukuma ujumbe wake vyema zaidi.
‘’Mambo mengi sana yanaweza kupotea katika chati usipotumia emoji. Lakini unapoongeza emoji nasema aaaah.... nimeelewa anamaanisha nini,’ anaongeza Sharon.
Lakini jambo lile moja linalosifiwa emoji linaweza kugeuka kuathiri jamii. Mwana sosholojia Dkt Kennedy Ong’aro anasema kuwa emoji zimeathiri ufasaha wa lugha kwa vizazi vya sasa.
‘’Watu wamejitumbukiza katika utamaduni wa kufuata njia za mkato kwa kila kitu,’’ anasema Dkt On’garo. ‘’Lugha ni njia ya mawasiliano. Unapotumia emoji, unakwepa kuandika maneno na hivyo unapoteza utaalamu wa uandishi, ambayo hatimaye tutaishia na vizazi vinavyotegemea vipicha au visura kujieleza badala ya lugha fasaha.’’ Anaongeza Dkt Ong’aro.
Emoji na Utamaduni wa Afrika
Mawasiliano ya mtandao ni jambo linalovuka mipaka yote. Kijana anapochati jijini Arusha ni sawa na kijana anayechati mjini Tokyo au Misri.
Kwa hivyo kwa kiasi kikubwa mbinu za kuchati na utumiaji wa teknolojia zinafanana
Lakini baada ya utumiaji wa emoji kushika kasi, malalamiko yalianza kutokea kuwa emoji zilizoko hazijumuishi watu wa tamaduni mbali mbali hasa wa Kiafrika.
Ni wazi kuwa waafrika hawawezi kuzungumza bila kutumia ishara au tanakali za sauti.
‘’Eee!, Alaa! Aka!?‘’ Utajua mtu ameshangaa, au ‘’Heheeeee, mmmmmh,’’ utahisi kufanyiwa kejeli. Ila kama Mwafrika usitake kuambiwa ‘Mscheeeew.’’ Hapo umeshamuudhi mtu.
Lakini maneno haya utayaelezaji katika chati? Ndio maana Waafrika wakadai kuwekewa emoji zao zinazohusiana na wao
Mwaka 2018, Msanii wa Ivory Coast O’Plerou Grebet azindua Emoji za Kiafrika.
“Lengo langu ni kuunda Emoji ambazo Waafrika wanaweza kujihusisha nazo .” anasema Grebet katika mtandao wake wa Twitter.
Ukipekua mtandao ukurasa wake utafurahishwa na sura za kiafrika zingine za kuchekesha, kama mtoto mwafrika aliyevaa hereni kubwa kubwa, au kikatuni cha mchawi aliyevalia sketi ya kushonwa kwa nyasi.
Lakini sio kuchekesha na kufurahisha tu. Grebet anasema katika mtandao wake kuwa nia yake ni kuweka Utamaduni wa Kiafrika katika jukwaa la kimataifa.
‘’Afrika ina utamaduni wa kuvutia na mapambo mengi, ambayo hayaonyeshwi katika emoji zingine. Watu wanafikiria Afrika ni matatizo tu na si hivyo kabisa.’’ Anasema Grebet.
Sasa ukitazama program tumishi yake Gebret kwa jina @Zouzoukwa kuna zaidi ya emoji 390 ambazo ameunda mwenyewe, kama mishangao ya Kiafrika, micheko ya Kiafrika, vyakula vya Kiafrika na mavazi.
Lakini ukizungumza na wataalamu wa masuala ya kijamii, hasa wa kizazi tofauti, utasikia baadhi wakielezea wasiwasi wao juu ya utumiaji wa emoji hizi.
Dkt Ong’aro, ambaye ni mkuu wa kitivo cha sayansi ya jamii katika chuo kikuu cha Daystar, Nairobi anasema kuwa utumiaji wa emoji unazima ubunifu wa vijana katika mawasiliano.
‘’Kwa mfano, ukitaka kuonyesha furaha kuna emoji ya ‘Smiley’ (tabasamu), lakini huu ni ubunifu wa mtu mmoja. Hatari ni kuwa kila mtu anajifunga nayo bila kufikiria njia zaidi za kuelezea hisia hiyo. Inaleta uvivu kwa vijana,’’ anasema Dkt Ong’aro.
Lakini umuhimu wa emoji pia unatofautiana kati ya vizazi.
Sharon, anayewakilisha kizazi cha gen Z (vijana wasiozidi miaka 30) anasema ‘’Emoji zimeunda lugha mpya yenye utamaduni wake mpya mtandaoni.'' Anasema. Kwa mfano emoji ya Jeneza kuchukuliwa kumaanisha kifo au msiba. Lakini ninapochati na rafiki zangu kisha tuweke emoji ya jeneza, inamaanisha, ‘waniua kwa vichekesho vyako’. Anasema Sharon.
‘’Emoji ya kidole gumba ina maana ‘ndio’ au ‘sawa’. Lakini hatujui kidole gumba kitageuka kumaanisha nini katika miaka mitano au kumi ijayo. Na hii ndio inafanya mawasiliano ya emoji kuwa na raha ya kipekee,’’ anaongeza.
Kwa upande wake Dkt Ong’aro anasisitiza kuwa emoji inawatenga baadhi ya watu katika mawasiliano.
‘’Ni watu wagapi wanazo simu mpya za smart. Je watakuelewa ukitumia hizi emoji? La!’’ anasema Ong’aro. ‘’kwasababu emoji nyingi zinatumika zina maana tofauti kulingana na tamaduni. Kwa hiyo ujumbe unaweza kupotoka hasa kati ya vijana na wazee.’’
Kwa sasa kuna zaidi ya emoji 4000 zinazotumika zikijumuisha dini, utamaduni, jeografia na umri tofauti duniani.
Lakini usimshangae mzee akikuambia haelewi unamaanisha nini kwa emoji uliyotuma. Kwa kuendelea kubuniwa emoji mpya kila uchao, pengine sisi wa vizazi vya sasa, hatutawaelewa vizazi vijavyo katika utumiaji wa emoji zao.