Na Firmain Eric Mbadinga
Majani yake yana vitamini na madini, mbegu zake zina mafuta yenye afya, protini, na antioxidant, na mizizi yake hutumiwa kwa madhumuni ya dawa.
Gome lake linajulikana kuwa na misombo ya bioactive. Mbegu zake zilizokandamizwa zinaweza kutenga maji machafu kwa kuzuia uchafu na kuyatuliza maji hayo.
Faida yake ni nini? Mti hukua haraka, na kuifanya kuwa rasilimali bora kwa upandaji miti na kilimo endelevu. Uwezo wake wa kustawi katika hali kame ni nyenzo ya ziada katika maeneo yenye ukame kama yale ya Afrika.
"Moringa oleifera" au mmea wa tumba, spishi asili ya bara Hindi, inayotambuliwa kama "mti wa miujiza".
Kwa mjasiriamali huyo wa kutoka Mali, Rokiatou Traoré, ufichuzi kuhusu sifa nyingi za moringa ulikuja wakati aliishi na marehemu mumewe huko Uturuki karibu miaka kumi iliyopita.
"Nilifanya utafiti na kugundua kuwa moringa ina manufaa kwa mazingira, jamii, na afya kwa ujumla," mwanmke huyo mwenye umri wa miaka 32 anasimulia TRT Afrika.
"Mimi na mume wangu tulitaka kurejea nyumbani na mradi wenye uwezo wa kuleta manufaa ya kiuchumi kwa wanawake, huku pia ukiwa na athari za kimazingira katika kupambana na kuenea kwa jangwa, ukataji miti, na mabadiliko ya hali ya hewa. Moringa ilikua chaguo bora kwa mradi huo."
Biashara iliyoleta mabadiliko
Shirika la Rokiatou la Herou, amblao linatambulika kama "mnyororo wa thamani wa moringa kwa athari za kiuchumi, kimazingira na kijamii", unalenga kulima mashamba na kutumia majani kutengeneza chakula na vitu vingine vyenye manufaa ya kiafya.
"Nikiwa nje ya uwanja, naona kila siku madhara ya kuenea kwa kasi kwa jangwa na athari zake kwa mazingira na uzalishaji," anaelezea Rokiatou.
Uhamiaji ni athari nyengine. Wanawake wengi zaidi wanaamua kuhamia maeneo mengine kufanya kazi na kuishi, kwani hali ya jangwa inaharibu kilimo na kuongeza joto katika maeneo yao.
"Shughuli za kiuchumi katika baadhi ya maeneo ya kilimo nchini Mali zimeshuka," Rokiatou anaiambia TRT Afrika.
Shirika la Herou linatafuta kusawazisha usawa wa biashara na ikolojia kupitia upandaji miti upya. Biashara hio inalenga kupanuliwa eneo lote la Sahel.
Ili kustawisha mradi huo, Rokiatou na mumewe, ambaye alifariki miezi michache tu baada ya kuzindua mradi huo, walichagua wilaya ya Koulikoro, ambayo ina wakazi karibu 18,000.
Kila kipengele kilizingatiwa kwa makini kwa ajili ya kuzinduliwa kwa Shirika la Herou mwaka wa 2020, kuanzia vifaa vya kiufundi hadi ubadilishanaji wa mawazo.
Uwasilishaji wa faida za mti huu na umuhimu wa kiuchumi na kimazingira ulikuwa jambo la msingi katika majadiliano na wakazi wa jamii wa wilaya hiyo.
"Miongoni mwa wataalam tulioshauriana nao ni bwana mmoja ambaye alijenga nyumba yake, kuoa, akapata watoto, akanunua gari lake na kufanya uwekezaji kwa kuuza moringa. Hivyo, warsha hizi zote ziliwawezesha wanawake kuelewa kikamilifu faida na umuhimu wa kutumia mfumo wetu ili kufaidika na mti huu," anasema Rokiatou.
Zoezi endelevu
Shilrika la Herou hulichakata morenga kuwa vimiminiko, unga, sabuni, mafuta, viungo, asali, na uji wa watoto, vyote huuzwa katika soko la kitaifa, kikanda na kimataifa.
Wanawake, ambao ndio sehemu kubwa ya wafanyikazi kwenye shamba hilo, wamefunzwa mbinu za kukuza, kutunza, na kuvuna majani. Katika mwaka wa kwanza, miti 5,000 ya moringa ilipandwa kwenye shamba la hekta tano.
"Waziri wa Ajira na mafunzo ya ufundi wa Mali wakati huo alikuja na timu yake kupanda miti ya kwanza ya moringa. Lilikuwa tukio la kukumbukwa mnamo Agosti 18, 2020," anasimulia Rokiatou.
Kuathirika kwa biashara
Mnamo Novemba mwaka huo huo, baada ya kifo cha mumewe, Rokiatou alipitia kipindi cha msukosuko ambacho kiliathiri biashara pia. Kwa bahati nzuri kwake na watu kadhaa anaowaajiri, familia na marafiki walimsaidia kusalia kidete.
Muda mfupi baadaye, mjasiriamali huyo kijana alianza safari ya kujenga ujuzi kupitia mafunzo.
"Kwa kuwa mume wangu alikuwa amefadhili shughuli zote, ghafla nilijikuta sina za kuendeleza biashara. Ndipo nilipoanza kutuma maombi ya ufadhili wa kimataifa, ikiwa ni pamoja na Tony Elumelu Foundation," anasema Rokiatou.
Wakfu huo, ambao uliendesha mpango wa ufadhili wa US $2,500, ulichagua Shirika la Herou, na hatimaye kurudi kustawi.
Moyo wa ujasiriamali wa Rokiatou tangu wakati huo umepata umaarufu mkubwa kutoka kwa umma, mamlaka, na mashirika yasiyo ya kiserikali.
Tuzo zake nyingi ni pamoja na kuwa Balozi wa Kijani wa Hali ya Hewa barani Afrika na "Shujaa wa Ardhi" na Umoja wa Mataifa katika Siku ya Dunia ya Kupambana na Kuenea kwa Jangwa na Ukame.