Jinsi msanii wa kike wa midundo ya ‘HipHop’ alipata umaarufu Afrika ya Kati bila ya Mtandao

Jinsi msanii wa kike wa midundo ya ‘HipHop’ alipata umaarufu Afrika ya Kati bila ya Mtandao

Mwimbaji kwa jina ‘Cool Fawa’ mwenye umri wa miaka 27 ameweza kuwaleta pamoja mashabiki kwa wingi kuziimba nyimbo zake. Mamake mzazi amewapa kisogo wakosoaji akisema kuwa anajivunia mafanikio ya mwanae.

Mlaghabishi kutokea Afrika ya Kati Cool Fawa amefanikiwa kuchangamsha watu wengi kupitia nyimbo zake huku akiwa kapendeza kwa kuvaa kawaida kabisa ‘akitinga’ vazi la ‘jump suit’ na viatu vya kisanii.

Msanii huyu wa midundo ya Hip-hop akifahamika kwa wimbo wake maarufu “Valide” yaani (“Imehakikishwa”).

Cool Fawa mara nyingi hupata ‘mchongo’ kwenye baa jijini Bangui, Jamhuri ya Afrika ya Kati – moja kati ya mataifa duniani ambayo ni vigumu kwa msanii wa kike wa midundo ya Hip-Hop kustawi.

Ni aina ya muziki ambao ni maarufu katika mataifa tajiri na hutegemea sana nguvu ya mtandao ili kufikia wafuatiliaji. Hakika Afrika ya Kati haikidhi vigezo vya mahitaji ya kuukuza muziki huo. Ni taifa lenye changamoto zake hasa vita vya wenyewe kwa wenyewe kwa zaidi ya miaka 9 sasa.

Raia wake ni moja kati ya watu fukara zaidi ulimwenguni. Takriban asilimia 10 tu ya watu ndio wenye uwezo wa kufurahia huduma za mitandao ya kijamii kati ya idadi ya takriban watu milioni 5 wa taifa hili.

Lakini changamoto hizi hazijamsimamisha Cool Fawa kufanya akipendacho.

Tangu kuanza kwa safari ya muziki mwaka 2012, Cool Fawa amefanikiwa kupata wafuatiliaji 4,500 kwenye mtandao wa Instagram huku waliotazama kazi yake ya 2018 iitwayo “On ya se marier” (“Tutafunga ndoa”) kwenye mtandao wa YouTube ikifikia wafuatiliaji 50,000.

Idadi hii ya wafuatiliaji inaweza kuonekana kuwa finyu ukilinganisha na wasanii nyota kama vile Adele, Beyonce na Taylor Swift lakini kwa mazingira aliyoko Cool Fawa ya Afrika ya Kati, bila shaka ni mafanikio ya kutambuliwa.

“Napenda nyimbo zake. Zinanipa tumaini ya kufanikiwa siku moja.” Alisema shabiki wake mmoja wa miaka 16.

“Cool Fawa, anatikisa.” Alisema shabiki mwengine.

Cool Fawa----Jina halisi ni Princia Plisson----mara nyingi huimba kwa Kifaransa huku akichanganya na lugha rasmi za taifa hilo, Sango na Kiingereza.

Wakati akiingia kwenye ulingo wa usanii hakukuwa na wasanii nyota wa kike nchini humo.

“Nilikuwa shabiki mkubwa wa Diams’s,” alisema Cool Fawa, hapa akimaanisha rapa wa Ufaransa, Melanie Georgiades, aliyevuma na albamu iitwayo, “Brut de Femme,” iliyosifika sana miongoni mwa mashabiki wa kiume.

Kupitia ndoto yake hiyo kinda huyo alifanikiwa kuwa rapa mwanamke wa pekee katika tasnia iliyokuwa ikitawaliwa na wanaume kipindi hicho.

“Kwa kuanzia hawakunichukulia kwa uzito ila baadae wakaishia kunikubali.” Alisema Cool Fawa.

Aidha pia aliongeza kuwa, “baadhi ya wazazi hawakuufagilia muziki wangu kwa kuwa hawakutaka watoto wao wa kike kuniiga na kujitosa kwenye usanii.”

Pambana siku zote

Kazi yake ya muziki hatahivyo ilipata pigo kulipozuka vita katika Jamhuri ya Afrika ya Kati kufuatia kupinduliwa kwa Rais Francois Bozize.

“Hatukuweza kutoka nje tena. Tuliogopa kupigwa risasi au kutekwa nyara.” Anasema Fawa.

Baada ya kurejea kwa Amani Cool Fawa alirudi kazini na kuzingatia zaidi midundo ya “zouk-love” yenye asili ya Carribean.

“Hio inauza zaidi.” Alisema kwa hisia za majuto.

“Watu wengi hapa Afrika ya Kati wanafikiri muziki wa rap ni kwa ajili ya waliofeli kwenye maisha.”

Kuishi kunakupasa kupambana kwani kupata pesa nako ni pambano la kila siku.

Cool Fawa amepata uungwaji mkono kutoka kwa baadhi ya wanafamilia wake licha ya kuwa hatokei kwenye familia yenye uwezo mkubwa. Aidha ameungwa mkono kwa kiwango fulani kutoka kwa Wizara ya Sanaa.

Cool Fawa vilevile anayo biashara yake ndogo anayoendesha kwa usaidizi wa dadake.

“Tunanua mawigi, viatu na begi kutoka nje na kuziuza hapa. Hilo hunisaidia kurekodi nyimbo zangu katika taifa jirani la Cameroon.”

Ndoto yake ni kuachia albamu yake ya kwanza.

Cool Fawa hupata kipato pia kupitia tamasha mbalimbali lakini nyimbo zake zilizoko kwenye YouTube bado hazijampa kipato kutokana na changamato ya watu wake kufurahia mtandao kiurahisi.

“Watu wanaonizunguka hutoa kauli hasi kuhusu anachikifanya mwanangu,” alisema Mama mzazi wa Cool Fawa, Cecile Yohoram, ambaye ni mwalimu wa Kiingereza katika shule ya sekondari.

“Lakini pindi tu napomskia akiimba, binafsi najivunia.”

TRT World