Rais wa Rwanda Kagame akizungumza katika ufunguzi rasmi wa kongamano la Women Deliver 2023. | Picha: Ikulu Rwanda 

Maelfu ya wanawake, wanaharakati na viongozi wamejumuika katika kongamano kubwa zaidi duniani ya wasichana na wanawake maarufu, Women Deliver 2023, linalofanyika Afrika kwa mara kwanza chini ya kaulimbiu "Nafasi, Mshikamano na Suluhu".

Marais Rais Macky Sall wa Senegal, Rais Sahel-Work Zewde wa Ethiopia na Rais Katalin Novak wa Hungary, pia walioshiriki, pamoja na Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umoja wa Mataifa linalohusika na masuala ya wanawake 'UN Women' Sima Bahous, Mkurugenzi mtendaji UNFPA, Dkt Natalia Kanem na Mwenyekiti wa Women Deliver Phumzile Mlambo-Ngcuka.

Rais Kagame akiwa na Rais Macky Sall mjini Kigali.| Picha: Ikulu Rwanda

Rais Sall aliwataka Marais wote katika bara la Afrika kuondoa kodi kwenye pedi za wanawake.

Rais Paul Kagame, ambaye ni mwenyeji wa mkutano huo, amesema kuwa ni furaha kuwa mwenyeji wa kongamano la kwanza la Women Deliver barani Afrika na kuungana na maelfu yenu katika ufunguzi wa mkutano huu wenye matokeo.

"Historia yetu kama taifa la Rwanda, imetuonyesha kuwa mabadiliko hayafanyiki mara moja, lakini kwa kujitolea, mshikamano na juhudi endelevu, tunaweza kufikia usawa wa kijinsia. Wanaume washiriki katika matunzo ya watoto (kazi ya ulezi bila malipo) ili kupunguza ukatili wa kijinsia Majumbani." Alisema Rais Kagame.

Rais Sahel-Work Zewde wa Ethiopia akiwa na Rais Paul Kagame wa Rwanda. Picha | Ikulu Rwanda

Aidha, Mkutano huo pia umewaleta pamoja Mawaziri na maafisa wakuu wa serikali mbalimbali, ukiwa mojawapo ya majukwaa makubwa zaidi duniani kuhusu mazungumzo ya ustawi wa wasichana na wanawake, usawa wa kijinsia, afya, na haki.

Kongamano la Women Deliver, litakaloendelea mpaka Alhamisi, tarehe 20, linalenga kuweka nafasi za uwezeshaji kwa vuguvugu la utetezi wa haki za wanawake, huku ukiwataka viongozi kuwajibika na kukuza msingi wa sauti za usawa wa kijinsia.

Viongozi katika kongamano la Women Deliver. Picha | Ikulu Rwanda

TRT Afrika