Mambo machache sana yalifahamika juu ya taratibu za kuuhifadhi mwili enzi za kale miongoni mwa watu wa Afrika lakini hilo limebadilika baada ya wanasayansi kugundua kaburi la mtoto aliyezikwa miaka 78,000 kwenye pango liitwalo Panga ya Saidi nchini Kenya.
Utafiti ulibaini kuwa mtoto huyo alizikwa akiwa na umri wa miaka mitatu 3 kwenye chimbo katika pango hilo na kufanya ugunduzi huo kuwa wa kwanza wa kaburi la Mwafrika. Wanasayansi walimpa jina mtoto huyo “Mtoto.”
Ugunduzi huu ni matokeo ya utafiti wa muda mrefu wa Taasisi ya sayansi ya Max Planck juu ya historia ya binadamu kutoka Ujerumani kwa ushirikiano na Makumbusho ya Kitaifa ya Kenya; ushirikiano ulioanza mwaka 2010 wakati uchimbaji katika eneo la ugunduzi uling’oa nanga.
Muungano huo wa wanasayansi ulichimbua baadhi ya mifupa ya mtoto huyo mwaka wa 2013 na 2017 lakini ikachukua muda kwa wao kuweza kufahamu umuhimu wa walichokuwa wamechumbua kuendana na madhumuni ya utafiti.
“Wakati huo hatukuwa na uhakika juu ya tulichokipata. Hali ya mifupa yenyewe haikuturuhusu tuseme lolote wakati huo,” alisema Dkt Emmanuel Ndiema wa Makumbusho ya Kitaifa ya Kenya. “Kwa hivyo tulichokipata kilitufanya kufurahi – lakini ingechukua muda kabla ya kuelewa umuhimu wake.”
Baada ya uchimbaji, mifupa na mabaki mengine yalipelekwa Burgos, Uhispania kufanyiwa utafiti na wanasayansi wa CENIEH.
“Tulianza kwa kuchambua fuvu na sehemu za uso na baadhi ya meno yaliyokuwa yamechakaa,” alisema Profesa Maria Martinon-Torres, Mkurugenzi wa taasisi ya Utafiti ya CENIEH.
“Hali ya uti wa mgongo na mbavu ilikuwa bado ipo vizuri pamoja na sehemu za kifua, kumaanisha kuwa mwili wa mtoto ulizikwa pasi na kuharibiwa chochote na kuoza kwa mwili kulianza ndani ya chimbo tulipoukuta mwili wake.”
Taarifa mpya kuhusu taratibu za kale
Ugunduzi huo sio wa kale kabisa duniani, lakini ni wa kale kabisa Afrika, sehemu ambayo ‘Homo Sapiens’ walitokea.
Namna kichwa cha mtoto kilivyokuwa kimewekwa kwa kuinuliwa kama kwenye mto kulionesha kuwa huenda palikuwepo na hafla ya mazishi. Taasisi ya Max Planck inasema kuwa inawezekana ya kwamba mazishi yalikuwa yakifanyika enzi hizo hususan mtoto alipoaga dunia,
Ugunduzi huo ulichochea fikra kuwa binadamu tangu zamani waliheshimu wafu. CENIEH walisema kuwa binadamu wa enzi hizo Afrika waliambatanisha umuhimu mkubwa na kutamatika kwa uhai wa mtu, na sio tu kuutupa mwili.
“Kinachofanya ugunduzi kuwa kuwa wa kipekee, tunaona tabia kuwa binadamu walijitambua kama muhimu na wa kipekee – kwa kubuni uhusiano na wafu.” Alieleza Profesa Martinon Torres.
Vifaa vya kale pia vilikutwa kwenye mabaki ya mwili – ugunduzi uliombatanishwa na aina ya viumbe wa hominini, kudokeza kuwa maziko huenda yalifanyika enzi wakati binadamu alikuwa tayari ameanza kutumia vifaa vyenye teknolojia endelevu.
“Uhusiano wa kuzikwa kwa mtoto huyu na vifaa-kazi vya kale kunaonesha kuwa Homo Sapiens alikuwa aina ya kiumbe mbunifu aliyeweza kutengeneza vifaa mbalimbali, kinyume na hominin.’’ Alisema Ndiema