Suala la uchaguzi wa vyama vingi limekuwa la kawaida barani Afrika tangu miaka ya 1990, kufuatia wimbi la demokrasia katika bara zima. Kwa mujibu wa Umoja wa Afrika, kumekuwa na zaidi ya chaguzi 70 zilizofanyika barani Afrika kati ya mwaka 2015 na 2022.
Licha ya ongezeko hili la chaguzi, ubora wa demokrasia yenyewe umesalia kuwa swali ambalo ni nadra kujibiwa bila kuumiza kichwa.
Sasa hivi, nchi kadhaa zinajiandaa kufanya chaguzi muhimu ambazo zitaathiri hali ya kisiasa ya bara hilo. Chaguzi zilizopangwa kufanyika mwaka wa 2023 zina uwezo wa kutengeneza mustakabali wa nchi husika na bara la Afrika kwa ujumla.
Chaguzi kwa kawaida hupangwa na tume huru za uchaguzi, huku waangalizi wa kimataifa wakifuatilia mchakato huo ili kuhakikisha kuwa ni huru, wa haki na uwazi. Mataifa ya Afrika mara nyingi yanakabiliwa na changamoto mbalimbali wakati huu, ikiwa ni pamoja na vurugu za kisiasa, udanganyifu katika uchaguzi, ukandamizaji wa wapiga kura, na mivutano ya kikabila.
Hata hivyo, nchi nyingi za Afrika zinaendelea kufanya maendeleo katika kuboresha michakato yao ya uchaguzi na kukuza demokrasia.
Chaguzi Mwaka 2023
Mwaka huu, nchi kadhaa za Kiafrika zitafanya uchaguzi wa rais ambao utaamua mustakabali wao na kuathiri uhusiano wa kikanda na kimataifa. Waangalizi wa ndani na wa Kimataifa watatazama kwa karibu baadhi ya chaguzi hizi kwa athari zake katika demokrasia, amani na maendeleo.
Nigeria, nchi yenye wakazi wengi zaidi barani Afrika, tayari imefanya uchaguzi wake mkuu Februari 25. Iliweka rekodi ya aina yake kwa kuwa na wagombea kumi na wanane walijitokeza kuwania kiti cha urais, huku wapiga kura wakipiga kura kwa maseneta na wajumbe wa Baraza la Wawakilishi. Uchaguzi huo ulikuwa muhimu kwa demokrasia, usalama na maendeleo ya Nigeria.
Uchaguzi huo umeondoa dhana kadhaa za muda mrefu kuhusu Nigeria kuhusu matokeo yao. Sio tu kwamba uchaguzi huo ulikuwa huru na wa haki, lakini pia ulivuka mipaka na vikwazo vya kiimani.
Mshindi wa uchaguzi wa urais alikuwa Bola Tinubu, gavana wa zamani wa Jimbo la Lagos na mteule wa chama tawala cha All Progressives Congress (APC).
Macho sasa yanageukia bara zima.
Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC)
Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) itafanya uchaguzi wa Urais na wabunge mnamo Desemba 20, 2023, kulingana na kalenda ya uchaguzi iliyotolewa na Tume Huru ya Uchaguzi ya Kitaifa ya (CENI) mnamo Desemba 20, 2022.
Rais wa sasa wa DRC, Felix Tshisekedi, ambaye aliingia madarakani Januari 2019 baada ya kushinda uchaguzi wa Desemba 2018 kwa asilimia 38 ya kura. Chama chake, Union for Democracy and Social Progress (UDPS), kilishinda viti 32 kati ya 500 katika Bunge la Kitaifa, baraza la chini la bunge.
Viti vingi vilienda kwa chama cha Common Front. Chama kikuu cha upinzani nchini DRC ni Lamuka, ambao ni muungano ulioundwa na wagombea wanne wa urais ambao walipinga matokeo ya uchaguzi wa 2018 na kumshutumu Tshisekedi kwamba aliingia makubaliano na Rais Kabila ili kupata ushindi wake. Muungano huu haukudumu kwa muda mrefu.
DRC imekuwa na historia ya ghasia za kisiasa na ukosefu wa utulivu tangu ilipopata uhuru wake kutoka kwa Ubelgiji mwaka 1960. DRC imejitahidi kufanya uchaguzi huru na wa haki tangu ilipoingia kwenye demokrasia mwaka 2006. Chaguzi za kwanza za kidemokrasia mwaka 2006 zilikumbwa na ghasia, udanganyifu na ukosefu wa vifaa na kupelekea Kabila kutangazwa mshindi dhidi ya Jean-Pierre Bemba. Duru ya pili ya uchaguzi, mwaka 2011 ilikosolewa vikali kwa kukosa uaminifu, uwazi na usalama.
Licha ya Jean-Pierre Bemba kuteuliwa kama Waziri wa Ulinzi, mazingira yanaweza kubadilika sasa.
Kadri uchaguzi uliopangwa kufanyika mwishoni mwa 2023 unakaribia, bara la Afrika litatazama kwa matumaini na hamu ya mapambazuko mapya ya uchaguzi huru na wa haki nchini DRC.
Gabon
Rais wa Gabon, Ali Bongo Ondimba, aliingia madarakani Oktoba 2009 baada ya kushinda uchaguzi wa Agosti 2009 kwa asilimia 42 ya kura. Alimrithi babake, Omar Bongo Ondimba, ambaye alitawala Gabon kwa miaka 42 hadi kifo chake Juni 2009.
Chama chake, Gabon Democratic Party (PDG), kilishinda viti 98 kati ya 120 katika Bunge la Kitaifa, katika uchaguzi wa Oktoba 2018. Kulingana na hesabu yake, chama kikuu cha upinzani ni Muungano wa Jamhuri Mpya (CNR), unaoongozwa na Jean Ping, ambaye anadai alishinda uchaguzi wa urais wa 2016 kwa 50.3% ya kura.
Ping amekataa kutambua ushindi wa Bongo na ametoa wito wa mabadiliko ya kisiasa.
Gabon imekuwa na historia ya utulivu wa kisiasa tangu ipate uhuru wake kutoka kwa Ufaransa mwaka 1960. Imepitia majaribio mawili tu ya mapinduzi ya kijeshi, mwaka 1964 na 2019, ambayo yote yalishindikana. Pia imedumisha uhusiano wa karibu na Ufaransa, ambayo inatoa msaada wa kijeshi na kiuchumi.
Mustakabali wa kisiasa wa Gabon unategemea jinsi Serikali na upinzani watakavyosimamia uhusiano wao na kushirikiana katika masuala muhimu yanayohusu nchi hiyo.
Mnamo Januari 2019, Bongo alirejea Gabon baada ya kukaa kwa miezi mitatu nchini Morocco kwa matibabu kufuatia kiharusi alichopata Oktoba 2018. Afya yake imezua maswali kuhusu uwezo wake wa kutawala na mipango ya nani ataridhi nafasi ya Uraisi. Upinzani umetoa wito wa kufanyika kwa mazungumzo ya kitaifa kutatua mzozo wa kisiasa na mageuzi ya mfumo wa uchaguzi, lakini Serikali imekataa ombi hili.
Uchaguzi ujao wa rais umepangwa kufanyika wakati fulani mwezi wa Oktoba 2023. Ni tumaini la wengi kuwa historia nzuri ya utulivu wa kisiasa nchini Gabon itaendelea baada ya uchaguzi.
Liberia
Rais wa Liberia na nyota wa zamani wa soka, George Weah, aliingia madarakani Januari 2018 baada ya kushinda uchaguzi wa marudio wa Desemba 2017 kwa 61.5% ya kura. Chama chake, Muungano wa Mabadiliko ya Kidemokrasia (CDC), kitachuana na Vyama Vishiriki vya Siasa (CPP), muungano wa vyama vinne:
· The UP
· Chama cha Uhuru (LP)
· Chama Mbadala cha Taifa (ANC)
· Chama cha All-Liberian (ALP)
CPP imekuwa ikipinga uhalali na kukosoa uwezo wa kufanya kazi wa Weah na imetaka mageuzi ya uchaguzi na mazungumzo ya muafaka wa kitaifa.
Liberia imekuwa ikikumbwa na ghasia za kisiasa tangu ipate uhuru wake kutoka kwa Jumuiya ya Ukoloni ya Marekani mnamo 1847. Imekumbwa na vita viwili vya wenyewe kwa wenyewe, kutoka 1989 hadi 1997 na 1999 hadi 2003, ambavyo viligharimu maisha ya watu wapatao 250,000 na wakimbizi zaidi ya milioni moja.
Pia ilikabiliwa na majaribio kadhaa ya mapinduzi ya kijeshi, hasa mwaka 1980, wakati Samuel Doe alipopindua na kumuua William Tolbert, na hivyo kufuta tabaka la watawala waliokua madarakani.
Mnamo Desemba 2020, Weah alinusurika katika kura ya maoni kuhusu marekebisho ya katiba ambayo yangepunguza muhula ya urais kutoka miaka sita hadi mitano lakini pia kumruhusu kuwania muhula wa tatu. Kura hiyo ya maoni ilisusiwa na upinzani na mashirika ya kiraia, yaliyodai kuwa ni kinyume cha sheria na udanganyifu.
Uchaguzi ujao wa urais unatarajiwa kufanyika mwaka huu mwezi Oktoba. Unatajaiwa kuwa uchaguzi wenye kutia na hofu ya mvutano mkubwa nchi nzima.
Libya
Mohamed al-Menfi alichukua madaraka Machi 2021 kama rais wa Baraza la Urais, chombo cha watu watatu kinachowakilisha mikoa mitatu ya Libya: Tripolitania, Cyrenaica, na Fezzan.
Alichaguliwa na Baraza la Mazungumzo ya Kisiasa la Libya (LPDF), jukwaa au chombo chenye wanachama 75 ambacho kiliundwa na Umoja wa Mataifa Novemba 2020 kuwezesha mabadiliko kwa njia ya amani nchini Libya. Mkuu wa Serikali wa sasa ni Abdul Hamid Dbeibeh, ambaye aliingia madarakani Machi 2021 kama waziri mkuu wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa (GNU). Baraza hili la mawaziri linajumuisha wawakilishi kutoka vyama na mirengo mbalimbali ya kisiasa.
Tangu Libya ilipojinyakulia uhuru wake kutoka kwa Italia mwaka 1951,mekumbwa na mapinduzi kadhaa, hasa mwaka 1969 wakati Muammar Gaddafi alipompindua Mfalme Idris na kuanzisha utawala wa kisoshalisti uliodumu kwa miaka 42 hadi alipofariki mwaka 2011 wakati wa uasi ulioungwa mkono na vikosi vya NATO.
Libya ilikuwa imefanya chaguzi chache za kidemokrasia tangu 2011, wakati baraza la mpito lilipochukua nafasi baada ya Gaddafi kuanguka. Uchaguzi wa kwanza ulifanyika mwaka wa 2012 kwa GNC, ambayo ilipaswa kuandaa katiba mpya na kupiga kura ndani ya miezi 18 Hata hivyo, GNC ilishindwa kufanya hivyo na kuongeza muda wake wa mamlaka, na hivyo kuzua maandamano na mapigano na wanamgambo wapinzani.
Uchaguzi ujao unalenga kuunganisha Libya chini ya mamlaka moja ya utendaji. Umoja wa Mataifa unashinikiza kufanyika kwa uchaguzi mpya nchini Libya, ambao bado haujapangiwa tarehe.
Madagascar
Andry Rajoelina, rais wa Jamhuri ya Madagascar, alishinda uchaguzi wa urais wa 2018 kwa 55.66% ya kura dhidi ya mpinzani wake Marc Ravalomanana, aliyewahi kuwa rais wa nchi hio tangu 2002 hadi 2009. Rajoelina pia alikuwa rais kutoka 2009 hadi 2014 baada ya kuongoza mapinduzi ya kijeshi yaliyomng’oa Ravalomanana.
Alijiuzulu mnamo 2014 ili kuruhusu Serikali ya mpito kuandaa uchaguzi mpya, ambao Hery Rajaonarimampianina aliibuka kidedea na kuwa rais kwa kipindi cha 2014 hadi 2018.
Kiongozi wa Serikali sasa ni Christian Ntsay, ambaye aliingia madarakani Juni 2018 kama waziri mkuu wa Madagascar baada ya kuteuliwa na Rajaonarimampianina kufuatia uamuzi wa mahakama ulioamuru serikali ya maafikiano kumaliza mgogoro wa kisiasa uliosababishwa na sheria tata za uchaguzi.
Wakiwa wamezama katika historia ya machafuko ya kisiasa na vurugu tangu uhuru wake kutoka kwa Ufaransa mwaka 1960, mapinduzi kadhaa, hasa mwaka 1972, wakati Didier Ratsiraka alipompindua Philibert Tsiranana na kuanzisha udikteta wa kisoshalisti uliodumu kwa miaka 17 hadi kushindwa katika uchaguzi wa rais wa 1991 na Albert Zafy. Bado kuna wasiwasi juu ya uchaguzi wa rais mwaka huu iwapo utaleta matokeo mapya yasiyo na vurugu.
Sierra Leone
Uchaguzi wa urais nchini Sierra Leone umepangwa kufanyika Juni 24, 2023. Rais wa sasa, Julius Maada Bio, anatoka chama tawala cha Sierra Leone People's Party (SLPP).
Chama chake kimemuidhinisha kwa muhula wa pili. Chama kikuu cha upinzani, All-People Congress (APC), kimemteua Samura Kamara mgombea wake. Kamara alikuwa mshindi wa pili katika uchaguzi uliopita wa urais mwaka wa 2018.
Sierra Leone imekumbwa zaidi na ghasia za kisiasa, hasa vita vya wenyewe kwa wenyewe kutoka 1991 hadi 2002. Mivutano ya kikabila, ufisadi, umaskini, na kugombania wa maliasili ndio vichocheo vikubwa vya vita.
Vita vilimalizika kwa makubaliano ya amani ambayo Umoja wa Mataifa, Umoja wa Afrika, na wahusika wengine wa kikanda na kimataifa walisimamia. Tangu wakati huo, Sierra Leone imepata maendeleo makubwa katika kuimarisha amani na demokrasia, lakini bado inakabiliwa na changamoto kama vile ukiukwaji wa haki za binadamu, utawala mbovu, ukosefu wa usawa wa kijamii, na kuyumba kwa uchumi.
Uchaguzi ujao unatarajiwa kuwa na ushindani mkubwa na wenye utata kati ya SLPP na APC. Matokeo yatategemea mambo kama vile idadi ya wapiga kura, hali ya usalama, utendaji wa kiuchumi, kura za maoni ya umma, n.k.
Somaliland
Uchaguzi wa urais wa Somaliland hapo awali ulipangwa kufanyika Novemba 2021, lakini umeahirishwa mara mbili kwa sababu kadhaa, kama vile janga la COVID-19, ukame, vikwazo vya kifedha na masuala ya usalama. Baraza la juu la bunge liliidhinisha kuahirishwa kwa hivi punde zaidi mnamo Oktoba 1, 2022, na kuongeza muda wa rais aliye madarakani Muse Bihi Abdi kwa miaka miwili hadi Julai 2023.
Uamuzi huu umekosolewa na baadhi ya vyama vya upinzani na mashirika ya kiraia kuwa ni kinyume cha katiba na kidemokrasia.
Rais wa sasa, Muse Bihi Abdi, anatoka chama tawala cha Kulmiye (Chama cha Amani, Umoja na Maendeleo), ambacho kimekuwa madarakani tangu 2010. Alishinda uchaguzi wa urais wa 2017 kwa 55% ya kura dhidi ya wapinzani wawili wakuu: Abdirahman. Mohamed Abdullahi Irro kutoka Waddani (Chama cha Kitaifa) na Faysal Ali Warabe kutoka UCID (Chama cha Haki na Ustawi).
Uchaguzi wa 2017 ulisifiwa sana kuwa wa amani, uwazi, na wa kuaminika na waangalizi wa kimataifa. Hata hivyo, ulighubikwa na baadhi ya changamoto, kama vile ucheleweshaji, migogoro, vurugu na masuala ya kiufundi.
Ghasia za kisiasa zilianza wakati wa harakati zake za kupigania uhuru kutoka kwa Somalia. Pia imekabiliwa na migogoro ya ndani kati ya koo na mikoa kuhusu kugawana madaraka na rasilimali. Baadhi ya migogoro hii imesababisha mapigano ya silaha na ukiukwaji wa haki za binadamu. Hata hivyo, Somaliland pia imepata maendeleo makubwa katika kujenga amani na utulivu kupitia mazungumzo na maridhiano. Imefanya chaguzi kadhaa za kidemokrasia tangu 2002 ambazo zimekuwa za amani na ushindani.
Zimbabwe
Uchaguzi ujao wa rais nchini Zimbabwe utakuwa wa pili tangu Emmerson Mnangagwa achukue madaraka kutoka kwa aliyekuwa kiongozi wa kimabavu, Robert Mugabe katika mapinduzi ya kijeshi ya mwaka 2017. Mnangagwa ndiye rais wa sasa na kiongozi wa chama tawala cha Zanu PF, ambacho kimekuwa madarakani tangu 1980.
Chama kikuu cha upinzani ni Muungano wa Movement for Democratic Change (MDC), unaoongozwa na Nelson Chamisa, ambaye alishindwa kwa kura chache na Mnangagwa katika uchaguzi wa 2018. Hivi karibuni Chamisa ameunda chama kipya kiitwacho Chama cha Wananchi (CCC) ambacho kimeshinda viti 19 kati ya 28 katika uchaguzi mdogo wa hivi karibuni.
Vyama vingine vya upinzani ni pamoja na Forum Party of Zimbabwe (FPZ), kikiongozwa na Jaji Mkuu wa zamani Enoch Dumbutshena, na United Parties, kinachoongozwa na Waziri Mkuu wa zamani wa Rhodesia ya Zimbabwe, Abel Muzorewa.
Vurugu, vitisho na madai ya ulaghai ni mambo yanayotajwa kuathiri uchaguzi wa 2018. Tangu nchi hio ipate uhuru, makabidhiano ya madaraka imekuwa ni changamoto kubwa. Je, tunaweza hatimaye kuona uchaguzi wa amani nchini Zimbabwe mwaka huu?
Chaguzi hizi kote barani Afrika ni muhimu kwa utulivu wa kisiasa wa nchi hizi, ukuaji wa uchumi, usawa wa kijamii, na pia una umuhimu mkubwa kikanda na kimataifa. Mchakato wa kidemokrasia nyuma ya chaguzi hizi unaweza ndio unaopelekea matokeo, mwitikio zaidi ya yote uimara wa mashirikiano ya kikanda.