Kenya yamuomboleza mwanamuziki Ally B aliyeaga dunia, Pich: Ally B.

Taarifa za kifo cha mwanamuziki huyo zilithibitishwa muda mfupi baada ya kupelekwa katika Hospitali ya Rufaa ya Pwani, Makadara Mombasa baada ya hali yake ya afya kuzorota.

Ally B alizaliwa mjini Mombasa na alianza rasmi kazi ya usanii mnamo 2005, kabla ya jina lake la Ally B kupata umaarufu zaidi na kujulikana kuanzia 2006.

Kipaji cha mwanamuziki huyo kilijulikana akiwa shule ya msingi ya Khadija Primary mjini Mombasa na kuhitimisha masomo yake shule ya sekondari ya katika kaunti ya Machakos, nchini Kenya.

Kilichowaunganisha wengi katika kumpenda Ally B kwa pamoja ni kipaji na ustadi wake wa kuchanganya nyimbo kutoka lugha za kimijikenda na lugha ya Kiswahili.

Miongoni mwa nyimbo zake maarufu ni Take you home, Kadzo, Ziki La Nazi, Maria, Naona Raha, Bembea, Silali - Ally B ikiwa pamoja na kufanya collabo na mwanamziki Size 8 kwa wimbo wa Silali, na ngoma iliyovuma ya Genye Genye aliyoimba na Masauti na ngoma ya Umenganga kupitia ushirikiano na Beka the Boy.

Mwanamuziki Ally B. Picha: Ally B

Ally B, pia alishiriki kwenye utunzi wa wimbo maarufu wa 'KWANGU 254' aliyoimba na wanamuziki Bahati, Bwana DNA, Collo, Size 8, Suzzana Owiyo, na Wahu

Rais William Ruto amewaongoza Wakenya kumuomboleza msanii huyo marufu.

"Ninaungana na washikadau wa muziki kuomboleza kifo cha Ally B, mwanamuziki ambaye alitumia talanta yake kukuza umoja na maelewano katika jamii yetu. Ali Khamisi Mwanguli aliandika ujumbe wake wa amani ndani ya mioyo yetu, na tutabeba wimbo huo wa maana milele. Mungu awape faraja familia yake, marafiki na mashabiki waliojitolea," Rais Ruto aliandika kwenye mtandao wa X.

Mwimbaji huyo amekuwa jina tajika katika sherehe za kitaifa nchini Kenya zikiwemo za hivi karibuni.

Huo umemfanya kuonekana kwenye majukwaa na viongozi kutokana na vibao vyake vya kizalenda, umoja, na maendeleo.

Ally B akiwa na rais William Ruto hapo awali. 

Waziri wa Jinsia, Utamaduni, Sanaa na Urithi. Aisha Jumwa naye ametuma rambi rambi zake kufuatia kifo cha msanii huyo.

"Nimepokea taarifa za kusikitisha za kufariki kwa mwanamuziki maarufu wa Pwani Ally B,kwa huzuni kubwa. Marehemu Ally B daima ataheshimiwa kwa umahiri wake katika muziki wa Pwani. Amekuwa ishara ya mwendelezo na urithi wa kitamaduni wa watu wa Pwani." alisema.

Mchango wake wenye talanta katika sanaa hii utaishi katika kumbukumbu zetu milele. Huruma na rambirambi zangu za dhati huenda kwa familia ya karibu na mkoa mzima.

Aidha, msanii huyu Ali Khamisi maarufu Ally B alijaribu bahati yake kwenye uchaguzi mkuu wa 2017 nchini humo aliposaka kiti cha mwakilishi wa wadi, Kisauni, Mombasa bila mafanikio.

Gavana wa kaunti ya Mombasa nchini humo Abdulswamad Shariff Nassir ametumia ukurasa wake wa Facebook kumuomboleza.

"Nimepokea kifo cha ghafla cha mwanamuziki Maarufu Ali B kwa huzuni. Ninatoa salamu zangu za rambirambi kwa familia yake, marafiki na jamii Ya Mombasa kwa ujumla. Ali b atakumbukwa kwa mchango wake katika sanaa kupitia muziki wake na utu wake wa joto. Hakika Sisi Ni wa Mwenyezi mungu, na kwake yeye tutarejea," Ally B alisema.

Mwanamuziki ambaye pia ni mwanasiasa maarufu nchini Kenya, Jaguar pia alitumia ukurasa wake wa X kuandika ujumbe wake wa kumuomboleza Ally B.

Msanii maarufu Nyota ndogo waliyeimba na Ally B kwenye wimbo wa Ni wangu, alimuomboleza kwa hisia na uchungu kutumia ukurasa wake wa facebook.

My friend Ali b. Nimekataa kukuposti maana nilikua nimekataa kuamini kua umeniacha mimi beste yako.dadaako yani urafiki wetu mpaka tulishukiwa tunatembea pamoja.alib nimelia sana nimeshindwa kujizuia hata mbele za wateja wangu.mbele yako nyuma yetu.mwenyezi MUNGU aiweke roho yako pema peponi.

Nyota Ndogo

Mtangazaji maarufu wa programu za mziki Afrika Mashariki Mzazi Willy M. Tuva ambaye anajulikana kwa ushirikiano na wanamuziki, alijiunga na taifa na hata sekta n zima ya muziki kumuomboleza msanii huyo.

Mzazi Willy M. Tuva alitumia ukurasa wake wa Facebook kuandika ujumbe wake.

Nashindwa kuamini. Wengi tulikuthamini. Imebidi urudi kwa Manani. Pumzika kwa Amani. #RIPAllyB INNA LILLAHI WA INNA ILAYHI RAJI’UN

Mtangazaji maarufu wa programu za mziki Mzazi Willy M. Tuva

Huzuni zimegubika tasnia ya muziki nchini Kenya iliyoanza mwezi wa Novemba na taarifa za kifo cha Ally B, ambaye amekuwa katika tasnia ya mziki kwa takriban miongo miwili.

TRT Afrika