Na
Sylvia Chebet
Gabon imekuwa nchi ya hivi karibuni zaidi barani Afrika kukumbwa na mapinduzi baada ya wanajeshi wa Walinzi wa Rais kumuondoa Rais Ali Bongo madarakani Jumatano asubuhi. Saa kadhaa baadaye, wanajeshi hao walioasi walimteua Jenerali Brice Clotaire Oligui Nguema, mkuu wa walinzi kuwa kiongozi mpya wa nchi.
Jeshi lilijitokeza mara tu baada ya Rais aliyepinduliwa Ali Bongo kutangazwa mshindi wa uchaguzi wa urais uliokumbwa na utata nchini humo akitarajia kuanza muhula wake wa tatu madarakani kwa miaka 7.
Alikuwa madarakani tangu 2009. Mpinzani mkuu wa Bongo kwenye uchaguzi huo alikuwa Albert Ondo Ossa ambaye aliungwa mkono na wagombea wengine kadhaa wa upinzani ambao waliungana siku chache kabla ya uchaguzi.
Upinzani ulikuwa umekataa matokeo ya uchaguzi huo kuwa ya udanganyifu. Waangalizi pia walikashifu uchaguzi huo kwa kuwa haukuwa wa uwazi baada ya mtandao kuzimwa na vyombo kadhaa vya habari vya kimataifa kupigwa marufuku.
'Wachache sana walifikiria' Licha ya kuwepo kwa malalamiko kuhusu uchaguzi huo, kuondolewa kwa Bongo muda mfupi baada ya kutangazwa ushindi wake, kulikuwa kwa haraka na jambo ambalo halikutarajiwa kwa mujibu wa baadhi ya wachambuzi wa masuala ya kisiasa.
'Wachache sana walifikiria'
"Ni watu wachache sana wangeweza kufikiria kwamba tungeishia kwenye mapinduzi. Na hii inatokana na ngome ya familia ya Bongo na mfumo wa Bongo na mitambo ya utawala nchini Gabon, mitambo ya uchaguzi, lakini pia vyombo vya usalama. ," Remadji Hoinathy, mtafiti Mkuu katika Taasisi ya Mafunzo ya Usalama Afrika alisema.
Ali Bongo Ondimba, 64, amehudumu kwa mihula miwili tangu aingie madarakani mwaka 2009 baada ya kifo cha baba yake, Omar, aliyetawala nchi hiyo kwa miaka 42.
Kumekuwa na kutoridhika kwa madai ya ufisadi na utawala mbovu chini ya ukoo wa kisiasa wa Bongo ambao umetawala taifa hilo lenye utajiri wa mafuta la Afrika ya Kati kwa takriban miaka 56.
Haraka sana
Muda wa mapinduzi, kufuatia kutangazwa kwa matokeo ya uchaguzi yaliyopingwa sana, na kasi ambayo hali iliendelea inaonyesha kuwa mapinduzi yalipangwa mapema," alisema Joseph Siegle, mkurugenzi wa utafiti katika Kituo cha Afrika cha Mafunzo ya Kimkakati.
Hii si mara ya kwanza kwa Ali Bongo kukumbwa na ugumu huu kila inapofikia Uchaguzi. Mnamo Januari 2019, kikundi cha wanajeshi walioasi walijaribu kumpindua lakini walizidiwa nguvu haraka na jaribio hilo likashindwa. Miaka mitano baadaye, wanajeshi sasa wamefanikiwa kumuondoa katika kiti cha juu.
Bongo, ambaye aliugua kiharusi mwaka 2018 na kutembea na fimbo, amewekwa chini ya kizuizi cha nyumbani na viongozi wa mapinduzi. Wajumbe kadhaa wa baraza lake la mawaziri na familia pia wamezuiliwa.
Familia ya rais imekuwa ikishutumiwa kwa ufisadi uliokithiri na kutoruhusu utajiri wa mafuta wa nchi hiyo kuwapunguzia na kuwapa ahueni kwa raia wa katika nchi ya watu milioni 2.3 pekee.
Utajiri dhidi ya umaskini
Koloni la zamani la Ufaransa ni mwanachama wa OPEC, lakini utajiri wake wa mafuta umejilimbikizia mikononi mwa wachache. Mapato ya mauzo ya mafuta ya Gabon yalikuwa dola bilioni 6 mnamo 2022, kulingana na Utawala wa Habari wa Nishati wa Marekani.
Watu tisa wa familia ya Bongo, wakati huo huo, wanachunguzwa nchini Ufaransa, na baadhi wanakabiliwa na mashtaka ya awali ya ubadhirifu, utakatishaji fedha na aina nyingine za rushwa, kulingana na Sherpa, NGO ya Ufaransa inayotetea uwajibikaji.
Wachunguzi walikuwa wamehusisha familia hiyo na zaidi ya $92 milioni katika mali nchini Ufaransa, ikiwa ni pamoja na majengo mawili ya kifahari huko Nice, kundi hilo lilisema.
Wakati huo huo, karibu 40% ya Wananchi wa Gabon wenye umri wa miaka 15 hadi 24 hawana ajira kulingana na utafiti wa 2020 wa Benki ya Dunia.
"Leo tunaweza tu kuwa na furaha," John Nze kutoka Gabon aliambia shirika la habari la AP, na kuongeza: "Hali ya zamani ya nchi ililemaza kila mtu. Hakukuwa na kazi. Ikiwa Wananchi wa Gabon wana furaha, ni kwa sababu walikuwa wakiumizwa chini ya Uongozi wa Familia ya Bongo".
Gabon ni nchi ya sita katika Afrika ya Kati na Afrika Magharibi kukumbwa na mapinduzi tangu 2020. Unyakuzi huo wa kijeshi unakuja takribani mwezi mmoja baada ya rais aliyechaguliwa kidemokrasia wa Niger Mohamed Bazoum kuondolewa madarakani na walinzi wake.
Mapinduzi hayo yameibua wasiwasi juu ya utawala na viongozi wa kikanda kujaribu kutatua migogoro hiyo.