Trevor Noah ni mtoto wa mama mzaliwa Afrika Kusini na baba mzungu wa Uswizi-Mjerumani. / Picha: Reuters

Mchekeshaji maarufu mzaliwa wa Afrika Kusini, anayeishi Marekani, Trevor Noah atapokea takriban Dola milioni 1.7 za Marekani ili kuitangaza Afrika Kusini na kuwavutia watalii katika masoko muhimu.

Mkataba huo umefichuliwa baada ya kamati ya Bunge kuhusu utalii kuuliza maswali juu ya ada hiyo na kuongeza kwamba Noah alitarajiwa kulipwa Dola Milioni 1.7 kwa tangazo la video ya dakika 5 linalotangaza Afrika Kusini kwenye masoko muhimu ya kimataifa.

Mwenyekiti wa kamati ya utalii Tandi Mahambehlala alitoa wito wa kusitishwa kwa mkataba wa Trevor Noah na hata kuulinganisha mkataba huo wa Noah na mpango tata wa bilioni 1 wa kufadhili kampeni ya matangazo inayohusishwa na timu ya soka ya Tottenham Hotspur.

Hata hivyo, Waziri wa Utalii Afrika Kusini Patricia de Lille aliiondolea serikali lawama akifafanua kuwa kiasi hicho cha Randi Milioni 33 za Afrika Kusini ni malipo kutoka kwa TBCSA, kampuni ya kibinafsi, na kwamba hakuna fedha za serikali zitakazotumika katika mradi huo.

Barazala kibinafsi la Biashara ya Utalii la Afrika Kusini (TBCSA) limethibitisha kufanya mazungumzo na mtumbuizaji huyo mzaliwa wa Afrika Kusini, Trevor Noah akiwemo miongoni mwa wasanii wengine mashuhuri nchini humo ili kuitangaza Afrika Kusini katika masoko muhimu duniani.

"Hii inaambatana na azma ya sekta ya Utalii ya kukuza watalii wanaowasili nchini hadi milioni 15.6 ndani ya muongo ujao. Lakini hii ni kutokana na makubaliano yatakayofikiwa hatimaye juu ya mkakati wa pamoja, mpango huo utafadhiliwa vikamilifu na TBCSA.

"TBCSA imekuwa katika mazungumzo na mcheshi maarufu Trevor Noah na wasanii wengine, ili kushirikiana nasi katika kampeni ambazo zitaleta uwepo mpana kwa Afrika Kusini kwenye masoko ya kimataifa," Tshivhengwa alisema.

TBCSA ni shirika linalowakilisha sauti ya pamoja ya biashara katika sekta ya ukarimu, usafiri na utalii nchini Afrika kusini ambayo inamilikiwa na wafanya boashara binafsi.

TRT Afrika
Tovuti hii hutumia vidakuzi. Kwa kuendelea kuangalia tovuti hii, unakubaliana na utumizi wa vidakuziSera ya Vidakuzi
Kubali