Waziri wa Kilimo nchini Tanzania Hussein Bashe/ Picha: Ikulu Tanzania

Tanzania imezindua mnada wake wa kwanza wa chai kama njia ya kuboresha uwekezaji na uzalishaji mapato kupitia sekta hiyo.

Mwishoni mwa mwezi Oktoba, bodi ya Chai Tanzania ilifanya mkutano na washikadau mbalimbali wa mnada wa zao hilo jijini Dar es salaam kwenye makao yake makuu kama juhudi za kuweka mipango ya kufanikisha shughuli ya mnada.

Waziri wa Kilimo Tanzania Hussein Bashe, ameeleza mnada huo kuwa "safari ambayo imekua ngumu sana iliyojaa hofu na mashaka mengi."

"Mnada huu utakua na majukwaa mawili, soko la moja kwa moja na mnada, tutasajili mikataba yote ya soko la moja kwa moja kwa ajili ya kupata taarifa sahihi na uwazi wa bei ili kumlinda mkulima," Bashe alisema.

Zoezi hilo la mnada wa chai linatarajiwa kuhudhuriwa na wateja wa chai kutoka ndani na nje ya Tanzania.

"Hadi kufika Juni mwakani, chai yote ya Tanzania itapita mnadani, na hatutaruhusu uingizwaji wa chai ndani ya nchi kwa matumizi ya ndani, ili kulinda soko." Waziri Bashe aliongeza.

Siku ya Jumamosi wikli hii, bodi ya chai Tanzania ilifanikiwa kuandaa zoezi la uonjaji chai ikitaja kuwa mikakati ya kufanikisha mnada wa kwanza wa kihistoria wa chai nchini Tanzania, siku ya kihistoria ya mnada wa kwanza wa chai nchini humo.

Mnada huo unatarajiwa kupigwa jeki na urahisishaji wa usafirishaji wa chai hadi ughaibuni kupitia ushirikiano wa Bodi ya chai Tanzania na mamlaka ya Bandari nchini Tanzania (TPA) kwani chai kutoka mnada huo itapewa kipaumbele kufika masoko ya nje haraka iwezekanavyo.

TRT Afrika