Benki ya Maendeleo ya Afrika inasema ujenzi wa njia ya SGR yenye urefu wa kilomita 651 kati ya Tanzania na Burundi itagawanywa katika sehemu tatu. / Picha: Reuters

Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) imeidhinisha mkopo wa dola milioni 696.41 kwa ajili ya ujenzi wa awamu ya pili ya reli ya kiwango cha kawaida ya Tanzania-Burundi-DR Congo (SGR).

Ujenzi wa reli yenye urefu wa kilomita 651 utagawanywa katika sehemu tatu: Tabora-Kigoma (kilomita 411) na Uvinza-Malagarasi (kilomita 156) nchini Tanzania; na kipande cha Malagarasi-Musongati (kilomita 84) nchini Burundi, kama ilivyosemwa na AfDB katika taarifa yao ya Jumanne.

"Mradi huu wa reli ya kiwango cha kawaida utaunganishwa na mtandao wa reli uliopo nchini Tanzania, ukiwezesha ufikiaji wa bandari ya Dar es Salaam."

Jumla ya kilomita 400 za miundombinu ya reli tayari zimejengwa nchini Tanzania kutoka Dar es Salaam hadi Dodoma tangu kuanza kwa awamu ya kwanza ya mradi huo.

'Kufungua maeneo ya kiuchumi'

Sehemu iliyobaki kutoka Dodoma hadi Tabora inajengwa.

Benki ya Maendeleo ya Afrika itatoa dola milioni 98.62 kwa Burundi kama misaada na dola milioni 597.79 kwa Tanzania kama mikopo na dhamana.

Gharama ya jumla ya mradi huo - nchini Tanzania na Burundi - inakadiriwa kuwa karibu dola bilioni 3.93, kwa mujibu wa taasisi hiyo ya kifedha ya Afrika.

"Mtandao wa reli ya SGR utafungua na kuunganisha maeneo muhimu ya usindikaji wa kiuchumi, viwanda, Depo ya Kontena za Ndani (ICDs), na vituo vya watu kando ya korido kuu. Hii itaboresha upatikanaji na kuendeleza shughuli za kiuchumi," walisema AfDB.

TRT Afrika