Kampuni hiyo ilionyesha majuto kwa "kutokuelewana" na ikasisitiza "heshima yake ya kina kwa kila mtu". / Picha: Instagram/@zara

Wakiwa wamekabiliwa na wito unaoongezeka wa kususia, kampuni ya mitindo ya Hispania, Zara, imeondoa kampeni yake tata ya matangazo iliyohusisha mifuko ya maiti baada ya kuzua hasira mtandaoni kutokana na kufanana kwake na eneo la vita la Gaza.

Wakizungumzia utata huo siku ya Jumanne, Zara - ambayo inamilikiwa na Inditex ya Hispania, muuzaji mkubwa zaidi wa mitindo duniani - ilikanusha madai hayo lakini hata hivyo iliondoa picha hizo tata kutoka kwenye tovuti yao.

"Kwa bahati mbaya, baadhi ya wateja walijisikia kukwazwa na picha hizi, ambazo sasa zimeondolewa, na wakaona kitu ambacho kiko mbali na kilichokusudiwa wakati zilipotengenezwa," ilisema taarifa ya Zara iliyochapishwa mtandaoni.

Katika moja ya picha hizo, mwanamitindo anayeonekana kuwa na upungufu wa damu anashikilia kile kinachoonekana kuwa mwili uliofungwa kwenye plastiki begani mwake, wakati katika nyingine umbo lililofunikwa linaonekana chini ya miguu yake huku akisimama kwenye seti inayoonyesha vipande vya vifusi, kuta zilizovunjika na dalili zingine za uharibifu.

Mwanzoni mwa vita vya Gaza, Inditex ilisema ilikuwa inafunga kwa muda maduka yake 84 ya Zara nchini Israeli hadi ilani nyingine. Picha: Instagram/@zara

"Heshima ya kina kwa kila mtu"

Kampeni hiyo ilizua hasira kali kwenye mitandao ya kijamii ambapo wengi walisema ilikuwa inafanya mzaha kwa makusudi uharibifu Gaza ambapo Israeli imefanya mashambulizi makali tangu Oktoba 7.

Ujumbe mmoja kwenye X, uliweka picha ya mama wa Kigaza akimkumbatia mwanae aliyefunikwa kwa kitambaa cheupe, huku watumiaji wengi wakiita kususia kampuni hiyo.

Kwa kujibu, Zara ilisema kampeni yake ya matangazo "ilipangwa mwezi Julai na kupigwa picha mwezi Septemba".

Wazo lao, kama ilivyosema, lilikuwa kuwasilisha "mfululizo wa picha za sanamu zisizokamilika katika studio ya mchongaji na ilibuniwa kwa lengo la pekee la kuonyesha mavazi yaliyotengenezwa kwa mikono katika muktadha wa kisanii".

Ilieleza masikitiko kwa "kutoelewana" huko na kurudia "heshima yake kubwa ni kwa kila mtu".

Mwanzoni mwa vita vya Gaza, Inditex ilisema inafunga kwa muda maduka yake 84 ya Zara nchini Israeli hadi itakapotangazwa tena.

AFP