Mamlaka ya udhibiti wa usafiri wa barabarani Tanzania imeongeza nauli za mabasi zinazotozwa kwa wasafiri wanaotumia njia mbalimbali katika nchi hio ya Afrika Mashariki.
Siku ya Jumatatu, Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Nchi Kavu (LATRA) ilipandisha nauli kwa asilimia 17 hadi 30, ikianza kutumika Desemba 8.
LATRA ilisema imepitia na kurekebisha nauli hizo kutokana na gharama kubwa za uendeshaji kwa wamiliki wa mabasi.
Mamlaka hiyo ilisema ilikutana na waendeshaji wa usafiri mwezi Oktoba, na kukubaliana kuhusu nauli mpya katika mazingira ya bei za juu za mafuta.
Waendeshaji walikuwa wamependekeza ongezeko la juu la nauli
Nauli ya chini kwa wasafiri, ambayo ilikuwa shilingi 500 za Kitanzania ($0.20), sasa itakuwa Tsh600 ($0.24).
Mabasi yanayosafiri kati ya miji mikubwa na maeneo ya vijijini yatatoza kati ya asilimia 17 na 19 zaidi.
Mabasi yanayounganisha vituo vikuu vya mijini kama vile Dar es Salaam na Mwanza, Arusha na Dar es Salaam, kati ya mingine, yatatoza ada ya ziada ya kati ya asilimia 20 hadi 30.
LATRA ilifichua katika taarifa kwamba waendeshaji wa mabasi walikuwa wamependekeza ongezeko la nauli kati ya asilimia 48 na 79%, lakini mamlaka hiyo ilikataa pendekezo hilo, ikisema ni la juu kupita kiasi.
Baadhi ya vitu vya kuzingatia
"Mapitio ya nauli yamezingatia mambo kadhaa, si bei ya mafuta pekee. Mengine ni gharama za mtaji, gharama za matengenezo ya gari, gharama za bima, tozo za LATRA, kodi ya mapato, na upungufu wa thamani ya gari," alisema Mkurugenzi Mkuu wa LATRA Habibu Saluo siku ya Jumatatu.
Nchini Tanzania, na kwa ujumla katika eneo la Afrika Mashariki, wakati wa msimu wa sikukuu za mwisho wa mwaka, watu husafiri sana kuungana na wapendwa wao.
Nauli za mabasi huwa juu zaidi katika kipindi cha Novemba, Desemba na Januari kutokana na ongezeko la idadi ya wasafiri.
Nchini Kenya, kwa mfano, nauli za mabasi huongezeka hadi mara tatu wakati wa mwisho wa mwaka.