Tanzania na Indonesia: Mikataba ya kibiashara iliyosainiwa baina ya Rais Samia na Joko Widodo, Dar

Tanzania na Indonesia: Mikataba ya kibiashara iliyosainiwa baina ya Rais Samia na Joko Widodo, Dar

Tanzania na Indonesia: Mikataba iliyotiwa saini baina ya Marais Samia na Widodo Dar Es Salaam
Indonesia na Tanzania  zinalenga kutimiza uwezo wa kibiashara wa nchi hizo mbili. Picha: Ikulu Indonesia

Mazungumzo ya pande mbili kuhusu biasahra kati ya Tanzania na Indonesia kufuatia ziara ya kihistoria ya rais wa Indonesia Joko Widodo, ambaye ni kiongozi wa kwanza wa Indonesia kutua nchini Tanzania kwa zaidi ya miongo mitatu, imetajwa kuwa yenye ufanisi kwenye sekta ya kibiashara.

Jopo la mawaziri kwenye msafara wa Rais Widodo nchini Tanzania ilijumuisha Waziri Mratibu wa Masuala ya Bahari na Uwekezaji Luhut Binsar Pandjaitan; Waziri wa Mambo ya Nje Retno Marsudi; Katibu wa Baraza la Mawaziri Pramono Anung; Waziri wa Nishati na Rasilimali Madini Arifin Tasrif; na Balozi wa Indonesia katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Tri Yogo Jatmiko huku ikonekana kama mbinu ya kufufua ushirikiano wa zamani wa kibiashara kati ya mataifa hayo.

Kwa mujibu wa taarifa kutoka kwa Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Tanzania, Zuhura Yunus, nchi hizo mbili zimeafikiana kuinua ushirikiano kwenye nyanja za kilimo, nishati, madini, mafuta na gesi, uvuvi na utalii, viwanda, na kilimo.

Kwa upande wa Ikulu ya Indonesia, Rais Jokowi alieleza kuwa ushirikiano kwenye muundo wa maendeleo unajumuisha pia sekta ya kilimo nchini Tanzania.

"Moja ya mipango ya maendeleo ni kufufua Kituo cha mafunzo ya kilimo kwa wakulima wa vijijini (FARTC) kilichopo Mkindo mkoani Morogoro, Tanzania," alisema rais Widodo.

Hatua hiyo imepokewa vyema na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mh. Samia Suluhu Hassan ambaye amekaribisha ukarimu huo wa Indonesia wa kufufua shughuli za mafunzo kwenye taasisi hiyo ya Kilimo huku akisifia mchango wa kituo katika uzalishaji wa wakulima na wataalam wa kilimo kwa jumla tangu uanzilishi wake mnamo 1996 na Serikali ya Indonesia.

Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan na mgeni wake Rais wa Jamhuri ya Indonesia Joko Widodo. Nchi hizo mbili zimetia saini hati 7 za Makubaliano (MoUs). Picha: Ikulu Indonesia

Ushirikiano katika sekta ya afya

Rais wa Indonesia, Jokowi ameongeza kuwa Indonesia imejitolea kushiriki katika maendeleo ya usalama wa afya ya Tanzania.

"Kampuni za dawa za Indonesia zitauza nje bidhaa zao za kwanza nchini Tanzania kama njia ya kuchangia kutimiza mahitaji ya bidhaa za dawa nchini Tanzania,” alisema Rais huyo.

"Indonesia inasaka kuongeza uwekezaji nchini Tanzania, ikiwa ni pamoja na kupitia kampuni ya serikali ya Indonesia ya mafuta na gesi ya Pertamina, usimamizi wa kitalu cha Mnazi Bay na usindikaji wa gesi asilia kuwa kemikali na mbolea,"

Kwa upande mwingine Waziri wa Mambo ya Nje, Retno Marsudi alisema katika mkutano huo mdogo, Rais wa Tanzania alieleza nia yake ya kujifunza kutoka Indonesia, hasa kwa maendeleo ya sekta ya mawese, na kuhusu maendeleo ya miundombinu na viwanda vya chini.

Mwenyeji wa mkutano huo, Mama Samia, ameongeza kuwa ushirikiano wa Indonesia hasa kwenye uzalishaji wa mafuta ya kula, inaoana na azma ya Tanzania ya kukomesha uagizaji wa mafuta kutoka nje ya nchi, suala ambalo limeligharimu fedha nyingi za kigeni.

TRT Afrika