Wataalamu kadhaa wanadai kuwa mazao yanayokuzwa katika maabara huchangia matatizo ya kiafya / Photo: Reuters

Na Coletta Wanjohi

Uamuzi wa serikali ya Kenya wa kurejesha uhandisi jeni wa vyakula yaani GMO, umezua mjadala mkubwa juu ya wasiwasi wa afya katika nchi hiyo ya Afrika, ambapo takribani watu milioni tano na laki nne wanakabiliwa na uhaba mkubwa wa chakula kufuatia ukame mbaya zaidi katika miongo minne.

Mnamo Oktoba mwaka jana, serikali ya Rais William Ruto iliondoa marufuku iliyokuwepo kwa zaidi ya muongo mmoja dhidi ya kulima na kuagiza chakula kilichozalishwa kwa GMO katika nchi yenye wakaazi zaidi ya milioni 54.

Moses Kuria, Waziri wa Biashara wa Kenya, alitetea uamuzi huo wenye utata.

"Tumeamua kimakusudi kuruhusu GMO kuingia nchini hadi tujiridhishe kuwa tuna mahindi ya kutosha," Kuria alisema mnamo mwezi Oktoba .

Marufuku ya GMO bado ipo huku serikali ikipelekwa mahakamani

Hatua hiyo ya serikali inakabiliwa na changamoto za kisheria, na angalau kesi tatu zinasikilizwa na mahakama nchini Kenya na moja iko mbele ya Mahakama ya Afrika Mashariki yenye makao yake makuu jijini Arusha nchini Tanzania.

Biodiversity and Biosafety Association ya Kenya, ni mojawapo ya mashirika ambayo yameishitaki serikali ya Kenya kwa kujaribu kuondoa marufuku hiyo.

"Serikali ilifanya uamuzi bila mashauriano ya umma," anaelezea Anne Maina, mratibu wa shirika la Biodiversity and Biosafety Association of Kenya.

"Mwaka 2015 tulienda mahakamani tena, na uamuzi ambao ulitolewa na mahakama ni kwamba kabla ya GMO kuingizwa nchini lazima kuwe na ushirikishwaji sahihi wa umma, elimu na uelewa wa umma ila jambo hilo halijatokea."

Lakini uchunguzi wa hivi majuzi wa shirika lisilo la faida linaloitwa ‘Route for Food’ unaonyesha asilimia 57 ya Wakenya hawako tayari kutumia mazao ya GMO kutokana na matatizo ya kiafya ambayo yameathiri sekta hiyo duniani kwa miongo kadhaa.

Asilimia 43 iliyobaki walisema hawana shida nayo. Shirika la kibinadamu linaloitwa ‘The International Rescue Committee’ inaonya kuwa zaidi ya watu milioni 11 - ikiwa ni pamoja na watoto, wanawake wajawazito na mama wanaonyonyesha - watakabiliwa na utapiamlo nchini Kenya mwaka huu wa 2023.

Zao la ubunifu

Jamii za wafugaji katika maeneo 23 yaliyo athiriwa na hali ya ukame wamepoteza zaidi ya mifugo milioni mbili na laki nne katika miezi michache iliyopita. Ukame wa sasa ulioanza mnamo 2020 unachukuliwa kuwa mbaya zaidi katika miaka 40.

Mimea ya GMO huzalishwa katika maabara ikiwa na sifa maalum, kama vile upinzani dhidi ya ukame au wadudu. Wanasayansi wanakili kuwa wanachukua jeni ya mbegu ya mmea na kuiingiza kwenye DNA ya zao hilo.

Kisha mmea huo hukuzwa katika maabara ili kuhakikisha kuwa umechukua sifa inayolengwa kabla ya kupandwa kwenye bustani za miti, kisha kupandwa tena katika mashamba madogo ili kufanyiwa majaribio kabla ya kupandwa kwa wingi.

Sehemu ya wakulima na wanamazingira wananukuu tafiti za kisayansi ambazo zinadai kuwa mazao yanayokuzwa katika maabara huchangia matatizo ya kiafya na kimazingira, ikiwa ni pamoja na mabaki ya dawa kwenye mimea.

Mahindi ni chakula muhimu kwa wengi nchini Kenya 

Helen Kahaso Dena wa kikundi cha kampeni ya mazingira inayoitwa ‘Greenpeace Africa’ anasema kuwa Wakenya watapoteza udhibiti wa mfumo wao wa chakula kwa kupitisha mazao ya GMO.

"Mara GMO inaporuhusiwa, inamaliza utamaduni wa zamani wa kupanda mbegu…Wakulima watalazimika kununua mbegu kutoka kwa makampuni ya kimataifa ambayo mengi yana miliki haki za kipekee za mbegu hizi za GMO….hivyo kimsingi, tunakabidhi mfumo wetu wa chakula kwa mashirika ya kimataifa," Dena anaiambia TRT Afrika.

Kilimo ndio uti wa mgongo wa uchumi wa Kenya, kikiajiri karibu asilimia 80 ya Wakenya, wengi wao wakiwa katika maeneo ya mashambani. Uzalishaji mdogo unawakilisha takriban asilimia 75 ya pato lote la kilimo nchini.

Umuhimu wa mahindi

Mahindi ni chakula kikuu nchini Kenya na hupatikana kwenye meza za chakula kama kifungua kinywa, chakula cha mchana na cha jioni kwa njia tofauti. Inatumika kama mahindi ya kuchemsha, haswa mara tu baada ya misimu ya mavuno.

Nafaka pia hukaushwa na kusagwa kutengeneza unga. Mojawapo ya chakula maarufu nchini ni ugali au sima, ambao unaliwa kwa mboga au nyama.

Shirika la utafiti wa kilimo na mifugo la Kenya (KALRO) linasema kuwa tani 11 za mbegu ya mahindi ya GMO iliyoidhinishwa ziko tayari kusambazwa kwa wakulima mwaka wa 2023 na kupandwa kwenye ekari 500,000 kama mradi wa majaribio.

Hii itafungua njia ya biashara ya mahindi ya GMO kwa makampuni binafsi. Aina tatu za mahindi zimejaribiwa na zinasubiri kibali cha baraza la mawaziri kwa ajili ya kusambaza nchi nzima.

Wakenya wanasemaje ?

Hata hivyo Wakenya wananonyesha wazi kutoridhishwa na mipango ya serikali.

Mary Wesonga, mwenye umri wa miaka 41, mama wa watoto watatu katika jiji la Nakuru, anapanga kujitosa katika ukulima mdogo ili kuepuka ulaji wa mahindi ya GMO yanapoingia sokoni.

Daima amenunua mahindi kwenye soko bila wasiwasi wowote.

"Nataka kupata kipande cha shamba na kupanda mahindi yangu, ili nisiwe na matumizi ya mahindi haya yaliyobadilishwa jeni. Wanasema si nzuri,” Wesonga anaiambia TRT Afrika.

Anaweka matumaini yake kwa watu wanaokodisha ardhi yao kwa wastani wa dola 100 za marekani kila mwaka.

Maeneo kadhaa nchini Kenya yameathiriwa na ukame na hii imefanya serikali kutafuta suluhu ya haraka kwa mazao ya GMO  

Jirani yake Millie Khalai, 63, anakubali. Kwa miongo kadhaa, bustani yake ndogo imemzalishia mboga na mahindi yanayohitajika na familia yake ya watu watatu - anaishi na wajukuu wake wawili.

"Hivi ndivyo wazazi wetu walitufundisha, kulima mahindi na maharagwe yetu wenyewe na kupanda tena mbegu za mavuno ya awali," Khalai anaiambia TRT Afrika.

Shamba lake la mahindi humpa magunia matatu ya mahindi kila mwaka na hutenga nafaka bora kwa msimu ujao wa kupanda.

“Nilisikia kwenye redio kuwa mahindi wataleta ni ya kupitia GMO, hivyo nina mahindi yangu ninayolima kutokana na mbegu za asili. Sitahitaji kula hiyo ya serikali . Sitaki mahindi hayo,” anasema.

Mjadala huo hata umegeuka wa kisiasa, huku kiongozi wa upinzani nchini Kenya Raila Odinga akiikashifu serikali kwa kile anachoita uamuzi wa "takataka".

Shirika la chakula na kilimo la Umoja wa Mataifa, UNFAO, pia limeelezea shaka juu ya ufanisi wa hatua hiyo.

“Kutokana na gharama ya mbegu za mahindi zisizobadilika, kukosekana kwa njia za kutosha za kugawa mbegu, na ukosefu wa motisha za kiuchumi kwa wakulima wadogo wa kulima mahindi hayo, kwa sasa kuna uwezekano mdogo kwamba teknolojia hiyo ingetumika kwa njia endelevu na wakulima wadogo wa mahindi barani Afrika,” shirika la FAO ilisema.

Suluhu ya haraka

Shirika la KALRO, hata hivyo, lMpa inasisitiza kuwa mazao ya GMO ni salama. "GMOs zimekuzwa kwa karibu miaka 30 bila matatizo ya afya yaliyothibitishwa," mkurugenzi mkuu wa KALRO Eliud Kireger anasema.

"Kisayansi, GMO imethibitishwa kuwa salama kwa chakula, malisho na mazingira na kwa sasa imeidhinishwa kwa kilimo katika nchi zipatazo 70 duniani kote," anaongeza.

Mara tu itakapotolewa, Kenya itaungana na nchi kama Afrika Kusini, Ethiopia, Misri, Sudan, Burkina Faso, Malawi, Nigeria, Ghana na Eswatini ambazo zimeruhusu matumizi ya uhandisi jeni wa vyakula.

Wataalamu wanasema serikali lazima itafute njia zingine za "suluhisho salama" ili kuhakikisha usalama wa chakula nchini Kenya.

"Kama tunataka kurekebisha hili, lazima tuhakikishe kuwa tunawapatia wakulima maji kwa sababu hilo ndilo tatizo," Dena wa Greenpeace anasema.

“Wakulima wengi wanategemea kilimo cha kutegemea mvua, kila kunapokuwa na mvua hakuna chakula. Ikiwa tutatafuta marekebisho ya haraka, tutakuwa na marekebisho ya haraka sasa. Lakini nini kitatokea katika miaka miwili au mitatu ijayo?” Dena anaongeza.

Mpaka sasa bado Kenya haiwezi kuingiza mazao yatokanayo na GMO nchini humo mapaka pale mahakama itakapo toa maamuzi ya mustakabali wa mazao hayo yanayo zalishwa maabara.