Mamlaka ya Nyumba ya Rwanda inasema kuwa asilimia ya paa zilizotengenezwa kutokana na asbesto zimeondolewa nchini.
Serikali ilisaidia kuondolewa kwa takriban mita za mraba milioni 1.4 (asilimia 82.4) za kuezekea za asbesto kutoka katika majengo ya umma na ya kibinafsi nchini humo kufikia Oktoba 31, kulingana na Mamlaka ya Nyumba ya Rwanda.
Mamalka hii inasema kuwa jumla ya asilimia 81.8 ya majengo ya serikali hayana paa za asbesto tena wakati asilimia 83 ya nyumba za makaazi na taasisi za kibinafsi hazina asbesto tena.
Juhudi za kuondoa paa za asbesto nchini Rwanda zilianza Oktoba 2009.
"Tunawahamasisha watu kubadili fikra zao. Wanapaswa kuelewa kwamba si vigumu tena kuondoa asbesto kwa sababu mafundi wengi wamefunzwa. Wanaweza kuchukua nafasi ya asbesto na karatasi za chuma za bei nafuu. Si jambo tunalohitaji wafanye kwa siku moja," amesema mratibu wa mradi wa kuondoa asbesto, Mathias Ntakirutimana,
Kwa nini asbesto ni hatari?
Asbesto ni jina linalopewa kundi la madini ya nyuzinyuzi asilia yanayostahimili joto na kutu.
Kwa sababu ya sifa hizi, asbesto imetumika katika bidhaa za kibiashara kama vile vifaa vya kuzuia moto, breki za magari, na vifaa vya ubao wa ukuta.
Nyuzi ndogo ndogo za asbesto huingia kwenye hewa zinaweza kuingia kwenye mapafu na kubaki humo kwa muda mrefu.
Asbesto ina nyuzi nyuzi nyingi na nyuzinyuzi hizo ndogo hupumuliwa kwa urahisi ambapo zinaweza kunaswa kwenye mapafu.
Wataalamu wa afya wanasema asbesto huongeza hatari ya kupata saratani kama ya mapafu na uzazi.
Shirika la Afya Duniani , WHO linasema kuwa takriban watu milioni 125 ulimwenguni wanakabiliwa na asbesto mahali pa kazi.
Takriban nusu ya vifo vinavyotokana na saratani ya kazini vinakadiriwa kusababishwa na asbesto. Kwa kuongezea, inakadiriwa kuwa vifo elfu kadhaa kila mwaka vinaweza kuhusishwa na asbesto nyumbani.