Kenya inasema wafanyabiashara wa kati yaani madalali katika biashara ya kahawa ndiyo sababu kuu ya wakulima kupata mapato duni kutoka kwenye sekta hiyo.
“Tutaziba pengo kati ya mkulima na mnunuzi wa kahawa. Pesa hizo zinazokwenda kwa wafanyabiashara wa kati zitawanufaisha wakulima wetu. Haitakuwa rahisi, lakini tutafanya hivyo,” naibu wa rais Rigathi Gachagua ambaye alikutana na wakulima wa kahawa amesema kwenye mtandao twitter yake.
“Pamoja na wakulima wa hahawa, tulikubaliana kuwa vyama vya ushirika vina mchango mkubwa katika biashara ya kahawa ,” Gachagua amesema.
Sekta ya kahawa inachangia vikubwa kwenye mapato ya Kenya.
Mauzo kutoka kwa kahawa yalifika hadi dola za Marekani 245,790,037 mnamo 2022. Kahawa hukuzwa katika kaunti 32 nchini Kenya na huajiri takriban watu milioni 6 moja kwa moja na kwa njia zisizo za moja kwa moja.
Je, serikali ina mawazo yapi ya kuongeza mapato kwa wakulima?
Alfred Kombudo katibu mkuu wa biashara nchini Kenya anasema kuboresha mapato kutokana na kahawa kunawezekana.
"Hatuuzi hata zaidi ya tani zinazodizi laki nne na tuna uwezo wa kufanya mara kumi ya hiyo kwa kuboresha ubora na wingi," anasema Kombundo.
"Tunahitaji kuondoa kahawa yetu kutoka kwa soko la bidhaa na kuifanya kuwa bidhaa maalum, ambayo tayari iko," anaongezea Kombundo, "Katika shindano la kimataifa asili mia 99 ya kahawa yetu inakidhi vigezo vya chapa maalum."
Anasisistiza kuwa kuna umuhimu wa kuhakikisha kuwa kazi ya kukutana na wanunuzi wanaokuja na mikataba yao kufanywa kwa njia sawa itasaidia huku miundombinu kuwekwa imara kwenye upande wa masoko .
Serikali imejipa changamoto ya kuhakikisha kuwa kuna viwanda ambavyo vitasaidia wakulima kuboresha mazao yao ya kahawa, kama vile viwanda vya kufungasha.
Na cha muhimu zaidi ni kwamba uwezo wa usambazaji wa kahawa hasa nje ya nchi unafaa kuboreshwa ili kahawa ya Kenya ipate kununuliwa zaidi.