Mji mkuu wa Uturuki Istanbul unaandaa mkutano wa 9 wa kimataifa wa Halal na maonyesho ya 10 ya Jumuiya ya ushirikiano wa Kiislamu (OIC) Halal Expo, matukio mawili makuu ya bidhaa na huduma zinazozingatia miongozo ya Kiislamu, inayojulikana kama Halal.
Hafla hizo zilianza rasmi siku ya Alhamisi kwa kushirikisha kampuni 500 mashuhuri kutoka nchi 45.
Mkutano huo unatarajiwa kuvutia zaidi ya wageni 40,000, wakiwemo 10,000 kutoka nje ya nchi.
Mkutano huo unajumuisha mada kama vile mnyororo ya ugavi halal, ufadhili wa ushiriki katika uchumi halal, uwekaji tarakimu na uvumbuzi katika uchumi halal wa kimataifa.
Matukio hayo ya siku nne yanafanyika chini ya kauli mbio: "Lango la Uchumi Halal Ulimwenguni: Kufunua Uwezekano."
Waziri wa Biashara wa Uturuki Omer Bolat alieleza siku ya Alhamisi katika mtandao wa X, kwamba uchumi halali ni muhimu kwa kuzingatia biashara ya nje ya Uturuki huku uchumi halali ukipanda hadi kufikia $10 trilioni.
Biashara ya Uturuki na nchi za Kiislamu
Akizungumza siku ya Alhamisi kwenye hafla ya ufunguzi, Waziri Omer Bolat alisema sehemu ya biashara ya Uturuki na nchi za Kiislamu ilipanda kutoka 11% hadi 26% katika miongo miwili iliyopita.
Rais Erdogan wa Uturuki ametuma ujumbe wa video kwenye mkutano huo wa 9 wa Halal duniani.
"Lengo letu ni kuongeza kiwango hiki hadi kufikia 35% ifikapo 2028," alisema Bolat.
Ihsan Ovut, katibu mkuu wa Taasisi ya viwango na metrolojia kwa nchi za Kiislamu (SMIIC), alisisitiza umuhimu wa ushirikiano endelevu na hatua za pamoja ili kuunda viwango katika sekta hiyo.
Emre Ete, makamu wa rais wa Baraza la Mkutano wa Halal Ulimwenguni, alisisitiza kwamba sekta ya halal inapendelewa sio tu na Waislamu bali pia na vikundi vya watumiaji kutoka nyanja zote za maisha, pamoja na bidhaa na huduma zake za kuaminika na zenye afya.
Ete alibainisha kuwa soko la halal limezidi $7 trilioni na linakadiriwa kufikia $ 10 trilioni katika miaka mitano ijayo.
Umuhimu wa mfumo wa usimbaji wa kutosha kwa bidhaa za halali
Asad Sajjad, Mkurugenzi mtendaji wa baraza la maendeleo la Halal la Pakistan, alisisitiza kwamba ukosefu wa mfumo wa kutosha wa usimbaji ni shida kwa sekta ya halal.
Kama tu ilivyodokezwa na ripoti ya uchumi wa Halal ya OIC, Uturuki, Indonesia, na Malaysia zimefanikiwa kupata nafasi kati ya wauzaji 20 wanaoongoza wa bidhaa za halal.
Mkutano huo unatoa fursa nzuri kwa uwekezaji, uzalishaji na uuzaji nje miongoni mwa nchi za OIC kwa kuunda jukwaa la ushirika na kuonyesha uwezo wa soko kutokana na mahitaji makubwa ya watumiaji wa bidhaa za halal.